Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mabasi 84 yapata leseni za muda, 60 yashindwa

32592 Mabasi+pic Tanzania Web Photo

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam. Wakati ongezeko la wasafiri wanaokwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya sherehe za mwisho wa mwaka likitarajiwa kujitokeza kuanzia wiki hii, Mamlaka ya Udhibiti na Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), imetoa vibali 84 vya mabasi madogo vya muda.

Vibali 84 kwa ajili ya magari hayo ya ziada vinalenga kuondoa changamoto ya usafiri inayoweza kujitokeza hasa mikoa ya Kaskazini.

Imezoeleka kila inapofika mwishoni mwa mwaka idadi ya abiria wanaosafiri kwenda mikoa mbalimbali huongezeka, hivyo kusababisha adha ya usafiri.

Ofisa leseni kutoka Sumatra, Habiba Tambaza alisema jana kuwa shida ya usafiri kwa sasa hakuna na wamejipanga kukabiliana nayo endapo itajitokeza. “Hadi sasa tumetoa leseni kwa magari 84 ambayo tayari yameshakaguliwa na kujiridhisha kuwa yamekidhi vigezo kwa ajili ya safari za mikoani,” alisema.

Mwananchi lilifika katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam jana na kushuhudia abiria wakisafiri bila usumbufu huku idadi ya magari ikiwa imeongezeka.

Hata hivyo, Tambaza alisema, “Tumeongeza magari kwa kutoa leseni (hizo) za muda zilizoambatana na masharti ikiwemo viwango vya nauli.”

Katika kuhakikisha hakutokei mwingiliano wa wasafirishaji katika utoaji wa huduma, alisema utaratibu wa magari yaliyopewa leseni za muda utaanza kwa mabasi hayo ya muda kupakia abiria baada ya mabasi yote yanayokwenda njia husika kuwa yamepakia na kuondoka.

Akizungumzia ukaguzi wa mabasi, mkaguzi wa kikosi cha usalama barabarani wa Jeshi la Polisi, Ibrahim Samwix alisema zaidi ya magari 60 yamezuiwa kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema baadhi ya sababu ni pamoja na umri wa gari kuwa mrefu, ubora wa gari na dereva kutokuwa na uzoefu wa kuendesha safari ndefu za mikoani.

Mmoja wa wasafiri aliyezungumza na Mwananchi, Frank Urassa alisema ni vyema mamlaka husika zikasimamia suala la nauli akikumbuka kipindi kama hiki mwaka jana zilipanda huku usafiri ukiwa wa shida.

“Nililipa Sh35,000 kwenda Moshi na magari yalikuwa hayapatikani, lakini leo nimeshangaa nimelipa nauli Sh28,000 ambayo ni ya kawaida na mabasi yapo,” alisema Urassa.



Chanzo: mwananchi.co.tz