Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maamuzi ya Serikali kuhusu ushuru wa Maziwa

6b66291e583b7dbaea14ce954196cf9f.png Tanzania kuja na utatuzi ushuru wa Maziwa kwa nchi za EAC

Tue, 3 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Tanzania imezihakikishia nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa inafanyia kazi ushuru wa maziwa unoalalamikiwa kuwa kikwazo kwa nchi hizo kufanya biashara ya bidhaa hiyo nchini.

Imeelezwa kuwa, baada ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Kenya na kutoa maelekezo ya kuondolewa vikwazo vya biashara, kulifanyika kikao mkoani Arusha kwa lengo la kuondoa vikwazo vya biashara na ushuru wa maziwa uliokuwa na changamoto katika ufanyaji biashara.

Mwanasheria wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Edwin Bantulaki amesema kuwa, baada ya kuelezwa changamoto hizo, Wizara ya Biashara kwa kushirikiana na bodi hiyo walifanya tathmini ya ushuru huo unaotozwa kwa nchi zote zinazoingiza maziwa nchini na kuangalia athari na faida za tozo hiyo.

Alisema hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Uganda kupitia barua yake ya Julai 19, mwaka huu iliyoandikwa na Waziri wa wizara hiyo, Frank Tumwebaze kuzilalamikia Tanzania na Kenya kuwa na vikwazo vya kuingiza bidhaa za maziwa kutoka nchi hiyo.

Alisema tangu mwaka jana, Uganda ilifanya jitihada kuuza bidhaa za maziwa katika nchi hizo lakini ilipata wakati mgumu kutokana na vikwazo katika ushuru licha ya kufanya majadiliano na viongozi wa nchi hizo bila mafanikio.

Katika barua yake kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, Profesa Adolf Mkenda, alisema Tanzania hutoza Sh 2,000 ambazo ni changamoto kwa nchi hiyo kuuza maziwa nchini.

Tumwebaze alilalamikia asilimia 1.75 ya ushuru na Sh 30, 000 (takribani Sh 46,000 za Uganda) kama tozo ya maombi katika Bodi ya Maziwa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa bidhaa zote za maziwa.

“Licha ya ukweli kuwa majadiliano mengi yamefanyika kati ya Uganda na Tanzania na kupewa ahadi ya kuondoa lakini haikutekelezwa ikiwamo ada ya Sh 2,000 inayotozwa na wizara,” alisema Tumwebaze.

Akielezea hatua zilizochukuliwa katika suala hilo la kodi za maziwa, Bantulaki alisema tayari wamepeleka mapendekezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ili kuangalia suala hilo na kuzitaka nchi za Kenya na Uganda kuwa na subira.

Alisema changamoto hiyo ilielezwa hata kwa wafanyabiashara wa Kenya na kuanza kufanyiwa kazi kwa kuanzia katika kikao kilichofanyika Arusha na kuafikiana katika kupunguza tozo hiyo lakini wakakubaliana kubadili sheria katika miezi mitatu.

“Malalamiko haya yameishafikia wizara na yanaendelea kufanyiwa kazi hivyo ni vema Kenya na Uganda na nchi nyingine kuwa na subira wakati serikali inafanyia kazi na itakuja na majibu mazuri katika kuwezesha kufanya biashara,” alisema

Chanzo: www.habarileo.co.tz