Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maagizo ya Waziri Ummy kwa halmashauri zote nchini kuhusu Machinga

8a0f41560fa9968c0db73cee6339c693 Maagizo ya Waziri Ummy kwa halmashauri zote nchini kuhusu Machinga

Wed, 22 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amesema wanaanzisha Idara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwenye halmashauri zote nchini itakayokuwa na Dawati la Machinga.

Ummy alisema jana kuwa wizara pia imeanza kuifufua Idara ya Uendelezaji wa Miji na Vijiji ili kuwabana maofisa mipango miji.

Alisema hayo mjini Morogoro kwenye mkutano na wamachinga wakati wa uzinduzi wa vibanda kwenye eneo la Soko Kuu la Chifu Kingalu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara , Profesa Kitila Mkumbo , Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando, Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood na madiwani.

Ummy alisema Dawati la Machinga litatatua changamoto au kero zinazokabili kundi husika. “Namshukuru Waziri Profesa Mkumbo kwa kuniwezesha kwa vile mambo haya yameshapita na sasa tunasubiri hatua ya mwisho ili kuweza kuwa na idara hii mahususi “ alisema na kubainisha kuwa kutakuwa na maofisa biashara wawili.

Alisema mmoja atasimamia ukusanyaji mapato na mwingine atapitia maeneo ya halmashauri yenye fursa za uwekezaji, viwanda na biashara. Alisema Tamisemi inaandaa mwongozo wa namna ya kuwapanga na kusimamia biashara ya wamachinga nchini.

“Wizara inandaa mwongozo utakaotolewa ndani ya wiki mbili au tatu, wa mikoa na halmashauri zote nchini wa jinsi ya kuwapanga na kusimamia biashara za wamachinga kote nchini,” alisema Ummy.

Aliagiza halmashauri ziimarishe mifumo ya mawasiliano baina ya serikali, wadau na wafanyabiashara wadogo kwa kuwa na vikao mara kwa mara. “Kwa hili ninaelekeza angalau kila halmashauri kukutana mara mbili kwa mwaka na wadau hawa hasa wamachinga na pia kuwa na Machiga Day (Siku ya Machinga) ili kupeana elimu ya kushirikiana, “ alisema Ummy.

Aliusifu uongozi wa Mkoa wa Morogoro hasa manispaa hiyo kwa kujenga vibanda vya kisasa vya machinga na akasema umekuwa mfano wa kuigwa na mikoa mingine.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Shigella alimuagiza Mkuu wa Wilaya, Msando kufanya kazi ya kuwapanga wafanyabishara hao na alitoa wiki moja agizo hilo litekelezwe.

Msando alisema vimejengwa vibanda 788 kwenye maeneo ya kudumu sokoni hapo kwa kufuata mistari na kupewa majina ya viongozi wa kitaifa ambao ni Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa na baadhi ya viongozi maarufu wa mkoa huo wakiwemo machifu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz