Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maagizo manane ya Mavunde kwa viongozi kuhusu sekta ya madini

MAVUNDEEEEEE Maagizo manane ya Mavunde kwa viongozi kuhusu sekta ya madini

Thu, 28 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanza. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ametoa maagizo manane kwa maofisa madini wa mikoa na watendaji wa wizara hiyo ili kuongeza ufanisi, utendaji kazi na mchango kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 9.8 mwaka 2022 hadi asilimia 10 mwaka 2025.

Akizungumza katika kikao kazi na watendaji hao, Mavunde alimuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Kheri Mahimbali kufunga ving'amuzi (GPS) kwenye magari ya maofisa madini wa mikoa ili kubaini maofisa watoro kazini, wanaoshinda ofisini na wanaokwenda kutatua changamoto za wananchi.

Pia, aliwaagiza maofisa na madini wa mikoa yote nchini kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, misingi na sheria, kushirikiana, kudhibiti mianya ya utoroshaji wa madini na kutokuwa chanzo cha migogoro katika maeneo yenye migodi, huku akionya kuwa ofisa atakayebainika kuwa chanzo cha mgogoro wowote hatasalia katika nafasi yake.

Maagizo mengine ni kuacha fitina, majungu na uchonganishi kwa kufanya kazi kwa upendo, umoja na ushirikiano, kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa wakisimamia kanuni, taratibu na sheria.

Pia, aliwataka kushirikiana na vyombo vya dola na kikosi kazi cha wizara hiyo ili kuzuia utoroshaji madini unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu, akidai wameanza tabia hiyo baada ya kuona mabadiliko ya viongozi kwenye wizara hiyo.

"Ofisa madini tutakupima kwa kutumia malengo tuliyokuwekea (KPI), tutawapima kwa namna ambavyo mtakwenda kufanya kazi katika maeneo yenu ya kazi. Ukiwa sekta binafsi unapimwa utendaji kazi wako kwa kuangalia asilimia ya kazi uliyoifanya, ndivyo tutakavyokuwa tunafanya," alisema Mavunde.

"Tunakwenda kuboresha mfumo wetu wa ufuatiliaji taarifa za makusanyo, utusaidie kuona mwelekeo wa makusanyo yetu na kila asubuhi nitakuwa naangalia ni ofisa gani amesimamia makusanyo vizuri na ambaye analegalega. Anayefanya vizuri atapandishwa na ambaye atasuasua atatupisha."

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Madini nchini, Profesa Idris Kikula alitaja changamoto zinazokwamisha tume hiyo isifikie lengo katika mchango wa wizara kwenye Pato la Taifa kuwa ni utoroshaji madini unaofanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Profesa Kikula alidokeza kuwa hadi Septemba 24, mwaka huu tume hiyo ilikuwa imekusanya zaidi ya Sh160 bilioni, sawa na asilimia 18.9 ya lengo la kukusanya Sh882 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/24.

"Kikao hiki kitatoa mwelekeo wetu na menejimenti imejiandaa kupokea maoni na ushauri au maelekezo ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza juhudi ili kufikia lengo la sekta ya madini kuchangia asilimia 11 kwenye Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025," alisema Profesa Kikula.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali alisema wakati sekta ya madini ikipangiwa kukusanya maduhuli ya Sh1 trilioni kwa mwaka wa fedha 2023/24, tume hiyo inatakiwa kukusanya Sh882 bilioni katika maduhuli hayo.

"Utekelezaji wake unaendelea na tunaamini tunazingatia weledi, na kusimamia kanuni na sheria ili kufikia lengo hilo. Tutahakikisha watendaji na maofisa madini katika mikoa hawatakuwa vikwazo katika kufikia lengo hilo," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live