Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa kufanyika Arusha

Maadhimisho Ya Wiki Ya Huduma Za Fedha Kitaifa Kufanyika Arusha Maadhimisho ya wiki ya huduma za fedha kitaifa kufanyika Arusha

Wed, 15 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Wizara ya fedha inatarajia kuadhimisha wiki ya huduma za fedha kitaifa ifikapo November 20-26 mwaka huu Jijini Arusha huku ikiwa inakusudia ifikapo mwaka 2025 takribani asilimia 80 ya wananchi wawe wamepata uelewa wa masuala ya fedha.

Aidha imetoa wito kwa Washiriki waliohusika na utoaji wa elimu kwa Umma katika Maadhimisho ya kwanza ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa kuendelea kutoa elimu ili kuwezesha watanzania wengi zaidi kuwa na uelewa wa masuala ya elimu ya fedha na kujikwamua kiuchumi.

Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Charles Mwamwaja ameeleza hayo leo November 15,2015 Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo katika ukumbi wa wizara hiyo wiki hiyo ya huduma za fedha inalenga kuwafikia wadau mbalimbali wakiwemo watumishi wa umma,wanafunzi,wakufunzi,wanawake,vijana na wenye mahitaji maalumu.

Amesema elimu kwa umma ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya fedha wa mwaka 2020/21-2029/30 na kwamba wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi watashiriki na wanaendelea kualikwa kushiriki katika maadhimisho haya ikiwa ni pamoja na Wizara,idara na wakala wa Serikali ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania pamoja Zanzibar.

“Njia mbalimbali zitakazotumika katika kutoa elimu ya fedha kwa umma ni machapisho(vipeperushi na mabango madogo),uandishi wa insha,gari la matangazo,semina,maonesho ya bidhaa za fedha,majukwaa ya kidigitali(mfano,simu za kiganjani),mitandao ya kijamii,vyombo mbalimbali vya habari(Tv,Radio,Magazeti)pamoja na burudani;”amesema.

Ametaja malengo ya wiki ya huduma za fedha kuwa ni kujenga uelewa na weledi kwa umma katika matumizi sahihi ya huduma za fedha zinazotolewa ili kujenga uchumi na kuondoa umaskini,kuimarisha ufanisi wa masoko ya fedha kupitia elimu ya fedha,kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha na kutoa elimu ya kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha.

Malengo mengine ni kuwezesha wananchi kusimamia vizuri rasilimali fedha,kuwezesha wajasiriamali wadogo kuongeza ujuzi na matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao,kuimarika kwa utamaduni wa kujiwekea akiba,kukopa na kulipa madeni na kuongeza kwa mchango wa sekta ya fedha kwenye ukuaji wa uchumi.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa wiki ya huduma za fedha unatarajiwa kuwa na matokeo chanya kwa mtu binafsi,kaya,jamii na taifa kwa ujumla kwa kuongezeka kwa idadi ya watu wenye kiwango cha ufahamu wa elimu ya fedha na maarifa juu ya upatikanaji na utumiaji wa bidhaa na huduma rasmi za kifedha,kuimarika kwa uelewa na matumizi ya masoko ya fedha.

“Kupitia wiki ya huduma tutaweza kusogeza huduma za fedha karibu zaidi na wananchi,kuimarisha matumizi ya huduma hizo pamoja na kupata maoni na ushauri wa kuboresha huduma hizo,kuwawezesha watumiaji wa huduma za fedha kuelewa haki na wajibu wao,kuwawezesha wananchi kupata maarifa kuhusu namna bora ya kusimamia vizuri rasiliamali fedha pamoja na kuwaunganisha wajasiriamali,”ameeleza

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi idara ya Uendelezaji wa Sekta ya fedha Dionisia Mjema ameeleza kuwa fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta hiyo ni pamoja na kukuza na kuimarisha biashara kwa wananchi na kupata maarifa na uelewa wa masuala ya fedha na hivyo kuwezesha kujenga utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.

“Kutokana na utafiti wa Finscope wa mwaka 2023 inaonesha nchini Tanzania ni asilimia 53.8 tu ya nguvu kazi wanatumia huduma rasmi za fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizo na kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za uchumi ambazo zingewezesha kuchangia katika kukuza pato la taifa," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live