Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ma-RC wapewa jukumu kuubadili sura Ushirika

11987 Pic+jafo Ma-RC wapewa jukumu kuubadili sura Ushirika

Sun, 12 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KUTOKANA na shughuli za Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuhamishiwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), wakuu wa mikoa nchini wamegizwa kujipanga kubadili sura ya ushirika nchini.

Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jafo, alipofungua kikao kazi kati yake na wakuu hao kujadili masuala mbalimbali ya ushirika.

Alisema serikali imeamua kuhamishia shughuli hizo TAMISEMI kwa asilimia 100, ili kuleta ufanisi katika ushirika, hivyo wakuu hao wanatakiwa kufahamu idadi au vyama vya ushirika vilivyoko kwenye maeneo yao.

“Mhakikishe mnafahamu udhaifu ulioko ndani ya vyama hivyo na kuhakikisha mnaweka mikakati itakayofanya ushirika uwe na sura tofauti na ushirika wa sasa.

"Siku zote lengo la mabadiliko yoyote ni kuleta ufanisi, hivyo ni imani yangu kwa usimamizi wa wakuu wa mikoa utakuwa na mabadiliko makubwa ya ufanisi uonekane uko tofauti, na kujibu changamoto ambazo zinaukabili ushirika kwa sasa,” alisema.

Jafo alisema hatua ya kuhamisha Tume ya Ushirika kwenda TAMISEMI imechukuliwa baada ya kubainika kuwapo upungufu mwingi wa kimuundo kwa sasa.

“Katika kutimiza wajibu wake wa kuwahudumia wananchi, kupeleka uchumi mbele katika maeneo mbalimbali ambayo tume hii imekuwa ikifanya kazi yake ndiyo yamekuja mabadiliko haya na ina maana kuwa wakuu wa mikoa ndiyo wasimamizi wakubwa wa ushirika katika mikoa yao," alisema.

Alisema kutokana na muundo wa sasa, ilikuwa ni vigumu kwa mkuu wa mkoa kuingilia kati ushirika inapobainika kuwapo dosari na hata warajis wa mikoa walikuwa hawajibika ipasavyo kwa wakuu wa mikoa.

“Tume hii sasa inafanya majukumu yake chini ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ni vyema wakuu wa mkoa wawe na nguvu ya kisheria ya kusimamia ushirika katika mikoa yao. Mkuu wa mkoa aone atafanya nini kwa lengo kuwahudumia wananchi waliojiunga katika ushirika,”aliagiza.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Joseph Nyamhanga, alisema wakuu hao watajengwa uwezo katika sheria ya ushirika na utendaji wa vyama vya ushirika pamoja na masuala ya kuzingatia katika uendeshaji vyama vya ushirika.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi, alipongeza uamuzi huo wa serikali na kusisitiza kwa nguvu ya kisheria waliyopata, watahakikisha wanasimamia ushirika kwa karibu na kutoa onyo kwa wabadhirifu wa ushirika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live