Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MSCL yaeleza mikakati ya kuboresha usafiri wa majini

MSCL yaeleza mikakati ya kuboresha usafiri wa majini

Sat, 7 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) nchini Tanzania imesema Serikali imetumia Sh152 bilioni katika miradi minne ambayo kukamilika kwake kutaongeza ufanisi wa shirika hilo na kupunguza gharama za usafiri katika maeneo ambayo wanatoa huduma.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa MSCL, Eric Hamissi amesema hayo leo Jumamosi Desemba 7, 2019 alipozungumza na waandishi wa habari.

Amesema kati ya fedha hizo, Sh89.7 bilioni ni kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya (MV Mwanza Hapa kazi tu) ambayo ujenzi wake ulianza Januari 2019 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24.

Amesema ujenzi wa meli yenye uwezo wa kupakia abiria 1,200, tani 400 za mzigo, magari madogo 20 na malori matatu, ni ahadi waliyokuwa wamepewa wananchi kwa zaidi ya miaka 23 baada ya kuzama MV Bukoba, kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 50.

Mradi mwingine ni ukarabati mkubwa wa meli ya MV Victoria ambao unagharimu Sh22.8 bilioni na haikuwahi kufanyiwa matengenezo kama hayo tangu ilipoundwa mwaka 1960, hivi sasa mradi huo umefikia asilimia 65.

"Vilevile ukarabati wa meli ya MV Butiama nayo inafanyiwa ukarabati ambao unagharimu Sh4 bilioni. Meli zote hizi zinabadilishiwa injini, jenereta, rangi, mabati yaliyochoka viti na kuweka mifumo ya kidijitali ya kuongozea vyombo hivyo," amesema Hamissi.

Mradi mwingine ni ujenzi wa Cherezo ambao unagharimu Sh36 bilioni. Utahudumia meli yenye uzito wa tani 4,000 ambao hivi sasa umekamilika kwa asilimia 68 na unatarajiwa kukamilika Machi 2020.

Hamissi amesema hivi sasa MSCL ina jumla ya meli 14 na boti ya utalii moja lakini zinazofanya kazi ni meli nne tu ambazo ni ML Wimbi, MT Sangara, Mv Umoja na MV Clarias.

Chanzo: mwananchi.co.tz