Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

MCHUCHUMA: Mradi waisubiri Serikali kwa miaka 4

43656 PIC+MRADI MCHUCHUMA: Mradi waisubiri Serikali kwa miaka 4

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kampuni ya Tanzania China International Mineral Resource Ltd (TCIMRL) inayoendesha mradi wa Mchuchuma na Liganga, imesema hadi sasa imeshindwa kuanza kazi kwa kuwa haijapata motisha iliyoahidiwa na Serikali.

Hivi karibuni, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alitoa siku 30 kwa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), lililoingia makubaliano na TCIMRL, kupitia na kurekebisha matatizo yaliyopo baina yao au kufuta leseni yao. Alisema TCIMRL inadaiwa na Serikali dola 375,000 za Kimarekani (sawa na Sh840 miloni) kama mrabaha.

“Leseni ya Mchuchuma na Liganga ni miongoni mwa mambo yanayolitia aibu Taifa hili. Mradi huu umekuwa ukizungumzwa kwa miaka kadhaa, lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika,” alisema Waziri Biteko.

Mkataba wa mradi huo wa uchimbaji wa chuma na ufuaji wa umeme ambao thamani yake imeelezwa kuwa dola 3 bilioni za Kimarekani (sawa na Sh7 trilioni), ulisainiwa mwaka 2011 kwa makubaliano kuwa Serikali itakuwa mbia kwa asilimia 20.

Lakini inaonekana kuna mambo bado hayajawekwa sawa ili mradi huo uanze kutekelezwa, kwa mujibu wa mahojiano ya Mwananchi na TCIMRL.

“Mabadiliko ya Sheria ili tuweze kupewa msamaha yalifanyika mwaka 2015. Kama tungepewa wakati huo, mradi wa umeme Mchuchuma uliokuwa unakamilika kwa miaka mitatu ungekuwa tayari unafanya kazi na wa Liganga wa miaka minne sasa ingekuwa umefika asilimia 90,” alisema Eric Mwingira, kaimu ofisa mtendaji wa TCIMRL.

Mwingira alisema walihitaji msamaha wa ushuru wa forodha kwa vifaa na mizigo watakayo ingiza kwa ajili ya utekelezaji wa mradi, pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) kwa mafuta watakayotumia. Kampuni hiyo inahitaji msamaha huo kwa miaka 10 ya mwanzo licha ya uhai wa mradi kuwa ni miaka 50 hadi 100.

Alisema mwaka 2014 walisaini mkataba na Serikali kuwa itawapa msamaha huo, lakini ilibidi yafanyike mabadiliko ya sheria ambayo yalifanyika mwaka 2015, yakiruhusu Serikali kutoa msamaha wa kodi na motisha kwa wawekezaji wa kimkakati ambao uwekezaji wao ni juu ya Dola 300 milioni (sawa na Sh701.8 bilioni).

Mwingira aliongeza kuwa kampuni mama ya Sichuan Hongda bado ina matumaini kuwa mradi huo utafanyika na mpaka sasa dola milioni 70 zishatumika kwa utafiti wa mradi, athari za mazingira, kulipia leseni na gharama nyingine za maandalizi.

“Tangu 2015 tumekuwa tukifanya mazungumzo na Serikali ili kuanza utekelezaji wa mradi huo, lakini hadi sasa hakuna majibu ya matumaini wala Waziri wa Fedha hajachapisha katika Gazeti la Serikali kuonyesha kwamba Serikali imekubali msamaha huo ili tuwe huru kisheria kuanza uwekezaji kwa kuwa hatuwezi kufanya hivyo bila uhakika,” alisema Mwingira.

Kuhusu tuhuma za waziri wa madini kuwa kampuni hiyo hailipi mrabaha, alisema kisheria hawapaswi kulipa kwani bado hawajaanza shughuli za mgodi, lakini wanalipia leseni kila mwaka.

Alipoulizwa Meneja wa Mipango na Utafiti wa TIC, Tibende Njoku alisema hawezi kuzungumzia masuala ya msamaha wa kodi kwa kuwa mradi huo bado haujafikia hatua ya uwekezaji hivyo haupo mikononi mwao. Hata Kamishina wa Madini, Mulabwa David alisema kuwa jambo hilo halipo mikononi mwake labda waulizwe NDC ambao jitihada za kuwapata ziligonga mwamba.



Chanzo: mwananchi.co.tz