Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lindi wavuna bilioni 108/- mauzo ya ufuta

60a301ecbab00dc0831df3c241f48fd3 Lindi wavuna bilioni 108/- mauzo ya ufuta

Tue, 19 Jul 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkoa wa Lindi umejipatia Sh bilioni 108 zinazotokana na mauzo ya ufuta katika minada minane iliyoendeshwa na vyama vikuu vya ushirika vya mkoa huo tangu msimu wa ufuta uanze mwaka huu.

Vyama hivyo ni vya Lindi Mwambao na Chama Kikuu cha Ushirika cha wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale (RUNALI)

Akizungumza katika mnada wa nne wa Runali, Kaimu Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Lindi, Cecilia Sostenes alisema fedha hizo zinatokana na mauzo ya tani zaidi ya 33,000 za ufuta katika minada mitano ya Lindi Mwambao na mitatu ya Runali.

Alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 69 zimeingizwa katika akaunti za wakulima na nyingine zimefanya malipo ya tozo mbalimbali za maghala, vijiji, halmashauri, serikali kuu na wasafirishaji.

Cecilia alisema mpaka sasa ofisi yake haijapata malalamiko ya malipo na yanaenda vyema, hivyo aliwataka wakulima watumie fedha hizo vyema kwa maandalizi ya msimu wa korosho na kujiwekea akiba.

Alisema serikali imeleta pembejeo za ruzuku katika korosho lakini moja ya kuwezesha tija ni kuwa na shamba safi, hivyo fedha wanazopata katika ufuta zinafaa kuwekezwa katika kilimo cha korosho.

Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa Runali, Hashimu Abdallah alisema wakulima wa chama hicho wameingiza Sh bilioni 30 katika minada mitatu ya kwanza ambapo waliuza tani 11,500.

Mkulima wa Kijiji cha Kiparamtua ambako mnada huo umefanyika wilayani Nachingwea, Maria Daudi alisema hajawahi kuona bei iliyopendeza ya ufuta kama hiyo ya mnada wa nne na kuwataka wakulima wenzake kuendelea kulifanya soko kunawiri na kujiandaa kwa msimu mwingine.

Mkulima mwingine wa Kijiji cha Kiparamtua, Halmashauri ya Nachingwea, Rabia Ndauka alisema ameridhishwa na mwenendo mzuri wa minada kwani inawakomboa wakulima katika umaskini na kuanza kuona kilimo chake ni biashara na kinaweza ‘kumtoa mtu’.

Mwenyekiti wa Runali, Oddas Mpunga pamoja na kueleza kwamba amefarijika na matokeo ya mnada huo kwa wenye tija kubwa zaidi kuliko safari iliyopita, aliwataka wakulima kutumia bei hiyo nzuri waliopata mwaka huu kwa kujiwekea akiba ya chakula, kusafisha mashamba na kutumia vizuri ruzuku ya pembejeo iliyotolewa na serikali.

Katika mnada huo wa nne kwa chama Kikuu Runali uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Kipara Mtua katika Amcos ya Kifama, kilo 2,736,110 ziliuzwa huku kampuni 20 zikishiriki mnada huo. Mahitaji yalikuwa kilo 5,370,421.

Aidha katika mnada huo wakulima walikubali kuuza ufuta wao kwa bei ya juu ya Sh 3,140 na bei ya chini Sh 3,087.

Miongoni mwa kampuni zilizosaka zabuni za kununua ufuta ni S&Q, SM holding, Agro Pulses, HS Impex, Tanzania China, Vallency Agro, Dorman, Afrisian, Mvungi, RBST na Iscon.

Chanzo: www.habarileo.co.tz