Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Leseni zaidi ya 500 za madini kufutwa

Zaidi Singida inatajwa kuwa na wawekezaji wengi wanao chipukia wa madini

Sun, 20 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri wa Madini Dk.Lemomo Kiruswa ameagiza kufutwa kwa leseni za utafiti wa madini zaidi ya 500 ambazo hazifanyiwi kazi wilayani Iramba mkoani Singida.

Wito huo umetolewa kwa wamiliki wa leseni za madini pamoja na wenye leseni za utafiti wa madini ambao hawazifanyii kazi kwa nchi nzima ambao wametakiwa wajiongeze na kuanza mara moja kuzifanyia kazi kabla ya wizara hiyo haija chukua hatua za kuwafutia.

Dk.Kiruswa alitoa agizo hilo jana wakati akifungua kongamano la wadau kujadili fursa na changamoto kwenye sekta ya madini lililoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda mkoani Singida.

Alisema Wilaya ya Iramba ina jumla ya leseni 694 za uchimbaji mdogo lakini ni leseni 102 pekee ndizo zinazofanya kazi, leseni za uchimbaji wa kati zikiwa tano (MLs) ambapo nne ni za Kampuni ya Sunshine ya Kichina ya Mining Ltd ambayo imeanza kuzalisha tangu Desemba 2021 na hadi kufikia Januari 2022 imeweza kuzalisha kilo 23.4 za dhahabu yenye ubora wa juu.

Alisema kutokana na uzalishaji huo Serikali kuu ilipata jumla ya Sh.200 Milioni ikiwa ni mrabaha na ada ya ukaguzi na Halmashauri ya Iramba ilipata Sh.10 Milioni ambapo pia ina leseni za utafiti wa dhahabu na almas (13) na leseni za uchenjuaji wa dhahabu 26.

Alisema kufuatia leseni hizo kutofanya kazi Waziri Kiruswa aliiagiza Tume ya Madini kuanza zoezi la kuzifuatilia ili utaratibu wa kuzifuta uweze kufanyika na kuwapatia watu wengine wenye nia ya kufanya kazi na Serikali iweze kupata mapato.

Aidha Dk. Kiruswa alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkuu wa wilaya hiyo Suleiman Mwenda kwa kuwa wa kwanza mkoani hapa kuandaa kongamano la namna hiyo na akaomba na mkoa nao ufanye hivyo jambo litakalosaidia kuwaunganisha wadau wote wa sekta ya madini mkoani hapa.

"Niseme ukweli tu kuwa wewe Mwenda ni DC pekee ndani ya Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla kufanya kongamano kubwa la namna hii lenye lengo la kuinua uchumi wa wananchi wa Iramba na Taifa kwa ujumla" alisema Kiruswa.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda akitoa taarifa ya uchimbaji wa madini katika wilaya hiyo alisema akiwa msimamizi mkuu wa masuala ya uchumi na maendeleo hasa katika sekta ya madini alisema mchango wa mapato yatokayo na madini katika wilaya hiyo ulikuwa mdogo sana.

"Kwa mwaka 2018/2019 mapato yaliyotokana na madini yalikuwa ni Sh.15 Milioni na mwaka 2020/2021 baada ya kutembelea kwenye migodi ili kujionea kazi za uchimbaji na changamoto zilizopo mapato yaliyopatikana ni Sh.66 Bilioni" alisema Mwenda.

Alisema lengo lao ilikuwa ni kukusanya Sh.80 Milioni lakini hawakuweza kulifikia kutokana na sababu mbalimbali lakini katika mwaka huu wa 2021/2022 wamepanga kufikia makusanyo ya Sh.100 Milioni na kuwa watayafikia mafanikio hayo iwapo utafanyika ushirikiano na wananchi wa wilaya hiyo na wadau wa sekta ya madini kujua fursa zitokanazo na madini.

Alisema Wilaya ya Iramba ambayo tangu ukoloni ilijulikana kuwa na utajiri mkubwa wa madini ambapo mgodi wa kwanza ulianzishwa miaka 1909 Sekenke ambapo hadi leo uchimbaji wa madini unaendelea katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2022 jumla ya gramu 1,037,000 (sawa na tani 1.1) zenye thamani ya Sh.109.5 zimezalishwa ambapo kodi ya Serikali kuu ni Sh.7.69 Bilioni ikiwa ni mrabaha na ada za ukaguzi.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Iramba imeweza kukusanya jumla ya Sh.328.4 Milioni ikiwa ni ushuru wa huduma uliotokana na uzalishaji huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Javan Diamonds Project (JDP) inayojishughulisha na Utafiti wa Almasi, Javan Bidogo ambaye pia ni mmiliki wa mradi wa utafutaji wa Almasi katika Kijiji cha Mbelekese kilichopo wilaya humo akitoa taarifa ya mradi huo kwenye kongamano hilo alisema kampuni yao ambayo ni ya wazawa imejikita kufanya utafiti wa Almasi katika wilaya za Ikungi na Iramba tangu mwezi Machi mwaka juzi na kuwa wapo katika hatua nzuri ya utafiti.

“Tumefanya uvumbuzi katika baadhi ya miamba inayokuwa na Almasi jumla yake ipo 13 na kati ya hiyo tisa ni mikubwa ambayo tumekuwa tukiifatilia sana,”. alisema Bidogo.

Bidogo alisema kwa hivi sasa wamechukua sampuri ya udongo na kuanza kuziosha kwenye mtambo wao uliopo kwenye mradi ili waweze kuziona Almasi zote ambazo zipo kwenye udongo huo ambao wameuchukua kutoka maeneo mbalimbali wilayani Ikungi na Iramba.

Bidogo akizungumza kiutaalamu na umahiri wa juu huku akionesha uzoefu wa masuala yote ya uchimbaji wa almasi alisema kazi wanayoifanya kuyabaini madini hayo si nyepesi kwa kuwa hayaonekani kirahisi ambapo hutumia gharama kubwa na changamoto wanayokabiliana nayo vifaa (mitambo) ambayo inagharama kubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live