Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Latra: Hatupangi nauli za bodaboda, bajaj

82c6b99f58c460855ed26f885c798724 Latra: Hatupangi nauli za bodaboda, bajaj

Mon, 9 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra) imesema haina jukumu la kuzipangia nauli pikipiki maarufu bodaboda, bajaji na taksi kwa kuwa huo ni usafiri wa kukodi.

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe alisema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLEO jana.

Alisema kanuni na sheria zinatamka wazi kuwa, bajaji na pikipiki ni kwa ajili ya kukodiwa kwenda maeneo ambayo mabasi hayafiki.

“Ukweli ni kwamba hairuhusiwi bajaji, pikipiki, taksi na gari yoyote ya kubeba abiria chini ya 15 kupiga debe. Kanuni za uchumi zinakataa kutumia chombo kidogo kusafirisha abiria wengi kwa wakati mmoja,” alisema Ngewe.

Alisema pamoja na kuwapo kwa kanuni na sheria, wapo baadhi ya watu wanaona kwa kuwa Latra haipo kila mahali, wanageuza vyombo vyao vya usafiri kubeba abiria kama daladala.

Pia alisema kuna utafiti unaondelea wa kutaka bajaj na taksi zifungwe mita za nauli na utafiti huo unatarajiwa kukamilika mwaka huu wa fedha.

“Hatua tuliyofikia ni kufanya majaribio hizo mita zinafanyaje kazi, tukimaliza majaribio na kujiridhisha kwamba zinaweza kuanza, tutawashirikisha wenye bajaji na taksi ili tuje na utaratibu mzuri watawekaje mita hizo,” alisema Ngewe na kuongeza:

“Kwa hiyo tumalize kwanza utafiti wetu tujue mita gani ziko bora na gani hazifai, tumeshawashirikisha watu wanaoweza kutengeneza mita nchini nadhani ni wale wanaotengeneza mita za Tanesco, tumeshakuwa na mazungumzo nao muda mrefu kama wanaweza kutengeneza mita ambazo ni maalumu kwa nauli za bajaji na taxi.”

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Latra, Salum Pazzy alisema kwa kuwa bodaboda na bajaji ni usafiri wa kukodishwa kama ilivyo taksi, utaratibu uliopo wa nauli ni wa makubaliano kati ya mtu anayekodi usafiri huo na mtoa huduma.

Alisema mamlaka hiyo haipangi nauli za usafiri huo kwa sababu una asili ya starehe na nguvu ya soko ndiyo inayoamua kiwango cha nauli kati ya mteja na mtoa huduma.

Pia alisema bodaboda na bajaji hawaruhusiwi kukaa kituoni kuita abiria au kupigia debe kama daladala na ndiyo maana hata mamlaka haiwapangii nauli.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live