Serikali imetoa zaidi ya Sh 21 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kimkakati hususan mpunga.
Mbunge wa Jimbo la Kyela Mkoa wa Mbeya, Ally Mlaghila amesema leo Jumanne, Septemba 26, 2023 wakati akizungumza na Wananchi wa vijiji vya Isuba na Bwato Kata ya Ndobo katika ziara yake ya kijiji kwa kijiji, kata kwa kata ya kueleza utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2020.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu nimeomba miradi mbalimbali ya Maendeleo hususan elimu ,maji, miundombinu ya barabara sambamba na utekelezaji wa sera ya afya ya ujenzi wa vituo vya afya na Zahanati,”amesema.
Amesema ujenzi wa skimu ya umwagiliaji utasaidia kuondokana na changamoto ya wakulima kutegemea msimu wa mvua na badala yake kutumia fursa hiyo kuongeza tija hususan kwa vijana wasio na ajira.
“Watanzania tumuombee Rais kwani anayofanya makubwa katika uwekezaji kwenye kilimo kwa vijana na hata sekta ya elimu kwa miaka ya nyuma watoto wakimaliza elimu ya msingi walikuwa wakipelekwa kukimbia mgambo au kuvua samaki mto Lufilyo ”amesema.
Katika hatua nyingine amesema Serikali imeelekeza kila halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya barabara yakiwepo magari ya ukaguzi kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji.
”Ndugu zangu uwepo wa miradi hiyo utakuwa fursa kwa vijana kupata ajira na kupunguza malalamiko sambamba na utekelezaji wa mradi wa kituo cha kusambaza umeme kupitia chanzo cha mto busela ambao utafungua fursa za kiuchumi.
“Rais amenionea huruma amesema mwanangu jimboni kwako kuna changamoto ya kukatika katika kwa nishati ya umeme sasa ni vyema kuwepo kituo kitakachotunza na kusambaza kwa wananchi ili kusaidia kuboresha shughuli za kiuchumi,”amesema.
Diwani wa Kata ya Ndobo, Ambakisye Njelekela ameeleza nafasi yake kuwa hatarini katika uchaguzi Mkuu 2025 kufuatia kilio cha wananchi kukosa kivuko (kiteputepu) kinacho onganisha vijiji vya pembezoni ambako zinapatikana huduma za kijamii iwepo za mazishi na nyumba za ibada.
“Mbunge nakuomba nisaidie kuhusu ujenzi wa kivuko hicho na wakati mgumu kwenye uchaguzi Mkuu 2025 wananchi kiu yao kubwa ni umeme na kivuko kwani msimu wa masika kumekuwepo na changamoto ya mafuriko,” amesema.
Ombi hili halikuungwa mkono na Mbunge Mlaghila , huku akieleza msimamo wake wa kutokuwa tayari kudanganya wananchi kuwa atajenga kivuko hicho kwa kuwafurahisha mwisho wa siku aje kulaumiwa.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi, CCM, Richard Kilumbo amesema lengo la ziara ya Mbunge ni kueleza wananchi namna Serikali ilivyotekeleza miradi ya maendeleo katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake.
Amesema wananchi wanapaswa kutambua kwa kipindi cha miaka mitatu Serikali imefanya mambo makubwa ikiwepo maji, barabara, elimu na afya lengo ni kuona huduma muhimu zinawafikia kwa wakati.
Mkazi wa Kijiji cha Isuba, Anastazia Kyusa ameomba Serikali kujenga mifereji ya kupitisha maji ya mvua pembezoni mwa miundombinu ya barabara ili kuwaepusha na hadha ya mafuriko ya mara kwa mara katika msimu wa masika.