Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa mchongo wa ubuyu, maisha ya chuo yanasonga

15884 Kwa+mchongo+pic TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Achana na kilio cha wanafunzi wengi hasa wa vyuo vikuu kukosa fedha za kujikimu, wapo wanaotumia fursa zilizopo kwenye taasisi hizo za elimu kujilipa mshahara kabla hawajaajiriwa.

Wapo wengi na katika Chuo cha Biashara (CBE) yupo Neema Misaji (25) aliyehitimu stashahada ya masoko akijiandaa kwa masomo ya shahada mwaka huu.

Kama zilivyo familia nyingi, yeye pia alikuwa hana uhakika wa kupata fedha kutoka kwa wazazi wake lakini hiyo ikawa chachu ya kutafuta cha kufanya.

“Uchumi wa wazazi wangu ulinifanya nitafute biashara inayoweza kuniingizia fedha kulingana na mazingira ya chuo ili kuwapunguzia mzigo kwa kujilipia ada na matumizi mengine,” anasema binti huyo anayeuza ubuyu.

Anasema alianza kama utani akiwa na mtaji wa Sh36,000 miaka miwili iliyopita, lakini kadri siku zinavyosogea biashara yake inazidi kukua. Alianza ili kujiongezea kipato kukidhi mahitaji ya chuo lakini sasa hivi anafanya na mambo mengine pia.

Wakati anaanza, anasema alinunua ndoo ndogo ya ubuyu uliotengenezwa aliufungasha na kupata glasi 60 alizoziuza kwa Sh1,000 kila moja. Alipouza awamu mbili aliongeza mtaji akaanza kuchukua ndoo tatu za ubuyu unaouzwa kwa bei ya jumla.

Kutokana na kuipenda biashara yake anasema huwa anatamani kuuza ubuyu kila anapokuta mkusanyiko wa watu.

Mbali na mikusanyiko, Neema anasema huwa anahudhuria maonyesho, anatumia mitandao ya kijamii kuuza ubuyu kwa wanafunzi wenzake pamoja na maduka yanayouza bidhaa tofauti.

“Kila ninapotembea huwa nashika kopo la ubuyu mkononi. Nikipita madukani huwaonjesha na wanaovutiwa huniruhusu kuweka bidhaa yangu, inapoisha hunipigia simu nipeleke mwingine,” anasema Neema.

Jambo hilo anasema limekuwa likimuongezea wateja kutoka sehemu mbalimbali za jiji tofauti na alivyofikiria. “Sasa hivi nimeacha kununua rejareja badala yake naagiza ubuyu mweupe kutoka Dodoma kisha nautengeneza na kuuza jumla kwa wafanyabiashara wengine,” anasema Neema.

Kutoka Dodoma, anasema hununu ndoo kubwa kwa Sh1,500 ila akiutengeneza huuza kwa Sh50,000 au Sh30,000 kwa ndoo ndogo.

“Zamani tulikuwa tukinunua ndoo kubwa kwa Sh1,000 lakini kwa sasa imepanda na huwa naagiza ndoo kubwa 10 kwa mwezi lakini inategemea mahitaji. Kuna wakati huwa yanaongezeka zaidi ya hapo,” anasema Neema. Kutokana na biashara hiyo Neema anaweza kupata faida kuanzia Sh200,000 kwa wiki laikini kama angekuwa anauza ubuyu huo muda wote, anasema angepata mara mbili yake.

Anasema pamoja na biashara hiyo kumsaidia kuweka mambo yake sawa, bado anataka kuendelea kusoma na mwaka huu anatarajia kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza.

Mbali na kuuza ubuyu, Neema anauza mafuta ya kula ya alizeti, vikoi vya kimasai na viatu vya kike ambavyo hushona na kubuni urembo wa aina tofauti.

“Nikitaka kuanzisha biashara mpya naitafutia mtaji wake ili iweze kujiendesha na kuzalisha faida,” anasema Neema.

Kwa sasa anao vijana wawili wanaomsaidia kuuza bidhaa zake hasa wakati akiwa darasani lakini anaamini, endapo biashara itakua zaidi ya hapo, upo uwezekano wa kuajiri wengi zaidi watakaosaidia kusambaza bidhaa zake.

Chanzo: mwananchi.co.tz