Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuzagaa chupa za rangi kwaikera Ofisi Makamu wa Rais

Eaea661e0e67c0322544c5a67361e4da.jpeg Kuzagaa chupa za rangi kwaikera Ofisi Makamu wa Rais

Sun, 28 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KUZAGAA mitaani kwa chupa za rangi zinazotumiwa na kampuni mbalimbali za vinywaji, kumekuwa hali inayoifanya Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), kupanga kukutana na wazalishaji wa chupa hizi ili kutafuta suluhisho.

Tofauti na chupa nyingine, hususani za maji ambazo ni nadra kuzagaa mitaani baada ya matumizi, chupa za rangi zinazohifadhi vinywaji kama juisi, haziokotwi kutokana na kilichoelezwa kuwa hazina soko kwa wanaosindika upya.

Mmoja wa waokota chupa, Asumta Haule anayefanya shughuli hizo maeneo ya Tabata Barakuda na Vingunguti jijini Dar es Salaam, kisha kuzipeleka Tabata Chang’ombe au Vingunguti kuziuza kwa wanunuzi wa jumla, ameliambia HabariLEO kuwa, wanunuzi hao hawataki chupa za rangi.

Mmoja wa wanunuzi wa chupa za jumla wa Tabata Chang’ombe, alisema wenye viwanda vya kusaga chupa hizo wanasema ni gharama kubwa kwao kusaga chupa za rangi ikilinganishwa na chupa za kawaida.

“Wenye viwanda wanadai kuwa chupa za rangi zimekuwa zikiwagharimu fedha nyingi kuzisaga kwa kuwa kwanza, wanapaswa kuziondoa rangi kabla ya kuzisaga hivyo hata sisi tunaonunua chupa kutoka kwa wakusanyaji hatuzinunui ndiyo maana unaona zinazagaa mitaani,” alisema.

Akizungumza na gazeti hili, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Mwita Waitara, alisema ofisi yake inazo taarifa za kukithiri kwa chupa hizo na kuwa taratibu zinaendelea kukutana na wazalishaji.

Alisema wazalishaji wa bidhaa wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kama zinaathari kwa mazingira, wanashiriki kudhibiti.

Alisema, wizara inatambua na kupongeza jitihada zinazofanywa na wakusanyaji wa chupa za kawaida. Waitara alisisitiza kuwa ofisi yake itakutana na wazalishaji wa chupa za rangi kujadiliana namna watakavyoshiriki kuziondoa mitaani.

“Ofisi yangu imeshaanza kuwasiliana na wazalishaji wa chupa za plastiki zenye rangi ili kuona ni kwa kiasi gani wanaweza kushiriki kuziondoa mtaani, na niwatoe hofu wananchi kuhusu tatizo hilo,” alisena Naibu Waziri Waitara.

Miongoni mwa maeneo ambayo gazeti hili limeshuhudia kuzagaa kwa wingi kwa chupa hizo ni katika Ufukwe wa Coco ambako Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay, Harrison Lukosi, alisema hali hiyo inachangiwa na idadi kubwa ya watu wanaoenda Jumamosi na Jumapili katika eneo hilo.

Alikiri kuwa wanaokusanya chupa zilizotumika hawapendelei zenye rangi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz