Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuporomoka uzalishaji almasi nchini kwaacha sintofahamu

Al,masi TANANIA.jpeg Kuporomoka uzalishaji almasi nchini kwaacha sintofahamu

Wed, 18 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Uzalishaji wa madini ya almasi nchini umeonekana kuporomoka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kutokana na sababu tofauti, ripoti ya Tume ya Madini imeeleza.

Si uzalishaji tu, hata shughuli za utafiti wa madini hayo zimepungua katika mikoa ya Tabora na Singida baada ya mwekezaji kushindwa kulipa kodi ya pango ya baadhi ya vitalu alivyokatia leseni.

Uzalishaji wa madini hayo unaporomoka wakati Serikali ikijivunia ukuaji wa mchango wa madini katika pato la Taifa uliotoka asilimia 3.8 mwaka 2014, asilimia 5.2 mwaka 2019 na asilimia 6.4 mwaka 2020 huku lengo ikiwa ni asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Takwimu za Tume ya Madini Tanzania (TMC), mwaka 2018/19, uzalishaji ulikuwa karati 415,122.91, mwaka 2019/20 ulikuwa karati 308, 489.73 ikilinganishwa na karati 50,013.98 mwaka jana, sawa na anguko la asilimia 88.

Anguko hilo limesababisha pia kupungua kwa mrabaha na ada ya ukaguzi kutoka Sh15.57 bilioni mwaka 2018/19, mwaka 2019/20 (Sh8.9 bilioni) hadi Sh1.27 bilioni mwaka 2020/21.

Anguko hilo lilisababisha pia kupungua kwa Mrabaha na Ada ya ukaguzi kutoka Sh15.57bilioni mwaka 2018/19, mwaka 2019/20 Sh8.9bilioni kabla ya kuporomoka hadi Sh1.27bilioni mwaka jana.

Advertisement Mapato hayo yalitokana na almasi zenye thamani ya Sh222 bilioni, mwaka 2018/19 (Sh128 bilioni) kabla ya kushuka hadi Sh18 bilioni mwaka jana.

Uzalishaji unaoangaziwa katika ripoti hiyo ni wa migodi mikubwa ya Al-Hilal na Williamson Diamonds Limited (WDL) mkoani Shinyanga.

Sababu za kushuka

Kushuka kwa uzalishaji huo kumetokana na sababu kuu mbili za ongezeko la gharama, kwa mujibu wa Yahya Samamba, kaimu katibu mtendaji wa TMC.

Samamba alisema mgodi wa Al-Hilal umeanza marekebisho ya mtambo wa uchenjuaji unaotumia gharama kubwa katika uzalishaji ikilinganishwa na kiwango cha alamsi kinachopatikana.

“Walisitisha uzalishaji kwa kuandika barua tangu mwaka 2018 na walieleza kufikia Juni mwaka huu, changamoto ilikuwa ni teknolojia ya mtambo wao kukosa ufanisi wa kuchuja vizuri madini na ilitumia gharama kubwa kupata madini kidogo, sasa ukarabati umekamilika na wataanza uzalishaji tena,” alisema.

‘Pili, mgodi wa WDL pia kwa miaka mitatu uzalishaji wake ulishuka sana kutokana na mazingira ya kifikia almasi kwenye miamba, ni kawaida kutokea kwenye shughuli za uchimbaji, sasa wameanza kupata kiwango kikubwa ndio maana unaona uzalishaji umeanza kuongezeka mwaka jana.”

Alisema katika robo ya kwanza mwaka huu migodi hiyo ilizalisha karati 154,989.08, zenye thamani ya Dola 56,190,035.

“Hatukupata chochote tangu Septemba 2019 ila Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliendelea kuchukua kodi zao,” alisema.

Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini (TMC), Venance Kasiki anaongeza sababu nyingine ya changamoto za Uviko-19 zilizoathiri bei ya madini hayo baada ya kushuka kutoka dola 300 kwa karati hadi dola 100 katika soko kubwa la Ubelgiji.

“Kwa hiyo baada ya kushuka bei ikabidi wapunguze uzalishaji kwa sababu gharama za kuzalisha zilionekana kubwa na ikaonekana ni hasara,” anasema Kasiki.

Hata hivyo, Ripoti ya Mwaka wa Fedha wa 2021 ya Kampuni ya Petra Diamond (PDL.L), inaeleza kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya bei ya almasi, PDL ilianza mipango ya kurejesha uzalishaji ili kuruhusu kuanza upya uzalishaji katika mgodi huo mapema mwaka huu.”

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mgodi huo uliochangia asilimia mbili ya uzalishaji wa migodi minne inayomiliki PDL kwa mwaka 2020, ulikuwa kwenye uangalizi na matengenezo katika mwaka wa 2021.

Mgodi huo uligunduliwa na Dk John Williamson mwaka 1940 kabla ya kusajiliwa mwaka 1942 na Serikali ya kikoloni ukiwa na mtaji wa pauni 200,000.

Hata hivyo sababu za kuporomoka kwa uzalishaji zimeibua wasiwasi kwa watafiti na wafuatiliaji wa madini hayo.

Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang anaeleza umuhimu wa kujiridhisha katika sababu zinazotolewa ili kuepuka mazingira ya ukwepaji wa kodi.

“Ni kweli teknolojia inahitajika kutokana na tabia ya mashapo ya almasi kusogea chini zaidi ya miamba, lakini si jambo la kushtukiza, ni taarifa zinazotakiwa kuelezwa mapema kutokana na picha za miamba zilivyoonekana kwenye utafiti.

Kwa hiyo Serikali inatakiwa kujiridhisha ili kuepuka hasara,” anasema Olang.

Hasara hiyo inaweza kuonekana kwa mwekezaji kufanya udanganyifu wakati wa kurejesha gharama za uzalishaji.

Hofu ya NRGI inachagizwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Ukaguzi wa Ufanisi unayoishia Machi 31 mwaka huu iliyoeleza TMC inakabiliwa na uchache wa rasilimali, hususani wafanyakazi au vifaa vya kuwezesha utekelezaji wa kaguzi za kifedha na mapitio ya kodi.

Ripoti inafafanua katika kaguzi zilizofanyika 2019/20 na 2020/21, hazikuzidi asilimia 20 ya kampuni za madini zilizokaguliwa kwenye vipengele vya gharama za uchunguzi, masuala yanayojibiwa na ofisa wa TMC.

Katika migodi hiyo, tuna maofisa wakazi wanaoshuhudia kila siku gharama za uendeshaji. Pili, hakuna mgodi unaoingiza vifaa vipya bila kuieleza TMC. Tatu, kila baada ya miaka miwili kuna timu ya wakaguzi wa fedha, kodi na ushirikishwaji wazawa hutembelea migodi hiyo, kwa hiyo tumekuwa tukijiridhisha bila shaka,” anasema Kasiki akijibu wasiwasi huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live