Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kupata mtaji kutoka makundi ya mtandaoni kwa ajili ya uwekezaji

18323 Pic+mtaji TanzaniaWeb

Fri, 21 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Upatikanaji wa mtaji ni miongoni mwa changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wengi hasa wadogo.

Mara nyingi, biashara kadhaa zimekufa muda mfupi baada ya kuanzishwa kutokana na kushindwa kupata mtaji wa kutisha kukabili ushindani uliopo, miongpni mwa sababu nyingi zilizopo.

Mtaji kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara ni changamoto kubwa hasa kwa wajasiriamali vijana na wanawake ingawa kuna njia mbalimbali za kuupata.

Njia hizo ni pamoja na kujichangisha kwenye makundi ya watu (crowdfunding) hasa kupitia mtandao wa intaneti ambayo ni njia mpya hasa barani Afrika.

Kutokana na upya wake Afrika na Tanzania ikiwamo, wadau wa uchumi walikutana na kuijadili katika kongamano la kimataifa kuhusu nchi zinazoibukia kiuchumi lililofanyika Chuo Kikuu Mzumbe tawi la Dar es Salaam.

Katika kongamano ambalo lilikishirikisha Chuo Kikuu cha Agder cha nchini Norway, mada mbalimbali zilijadiliwa ili kuongeza uelewa wa wahudhuriaji.

Kati ya mada kuu zilizotolewa ni inayohusu makundi ya watu kama namna mpya ya kupata fedha kwa ajili ya uwekezaji. Jopo la wataalamu kutoka Tanzania, Norway, Uingereza na kwingineko lilijadili mada hii kwa kirefu.

Upatikanaji wa fedha

Njia ya kupata fedha kutoka makundi ya watu sio mpya. Kinachofanyika katika dunia ya leo ni kupata fedha hizi kwa kutumia mitandao. Tovuti maalum huanzishwa kwa ajili hii. Mwenye wazo la biashara huliweka katika jukwaa husika kama vile Indiegogo au Kickstarter.

Baada ya wazo husika kuwekwa jukwaani, wanaovutiwa na kupendezwa nalo huchangia kadiri ya uwezo na matakwa yao. Hii huwezesha watu wengi kuchangia kiasi kidogo kidogo hatimaye kupatikana fedha zitakazokidhi mtaji wa biashara husika.

Huweza kuwa ni fedha kwa ajili ya kukuza na kulea wazo la biashara, kuanzisha biashara au kuendeleza na kupanua biashara. Fedha huweza kuchangwa kama msaada, mkopo au hisa.

Kwa Tanzania, ukusanyaji wa fedha kwa njia hii upo zaidi katika shughuli za kijamii mfano harusi au msiba ingawa wapo wanaochangiana kwa ajili ya sherehe za kipaimara, unyago au jando.

Ni bahati mbaya kuwa njia hii haitumiki sana kupata fedha za uwekezaji ambao unaweza kuchangia kubadili hali ya kiuchumi wa jamii husika baada ya mradi ambako fedha zitaelekezwa kushamiri.

Jukwaa

Kufanikiwa kukusanya fedha kwa njia hii ya makundi ya watu ni lazima kuwepo jukwaa maalumu kwa ajili hiyo katika mtandao tena kwa tovuti maalumu.

Waanzilishi na wasimamizi wa jukwaa huratibu namna ya kufikisha wazo la biashara katika jukwaa na kukusanya fedha husika na namna ya kumfikia mlengwa. Kwa namna majukwaa yanavyofanya kazi kwa kasi kikubwa fedha huweza kukusanywa kwa njia za kielektoniki kama vile kupitia kadi maalumu za benki au mitandao ya simu za mkononi.

Kati ya majukwaa yanayofahamika duniani kwa ajili hii ni pamoja na Indeogogo na Kickstarter. Ni muhimu kuanzisha kampeni katika jukwaa linaloheshimika, linaloweza kukutanisha wadau wengi kadiri ya kiasi cha fedha kinachotafutwa na sababu ya kutafuta fedha hizi.

Haitakuwa sahihi kwa mfano kutafuta fedha za ufadhili katika jukwaa la mtaji la biashara. Zipo tovuti maalumu kwa ajili ya ufadhili.

Kampeni

Kupata fedha mtandaoni huhitaji mambo mengi kabla ya kufanikiwa ambayo ni pamoja na kuanzisha na kuendesha kampeni ili kuwafikia wachangiaji wengi zaidi.

Kutegemeana na aina ya biashara inayotafutiwa fedha, kampeni inaweza kufanywa mara moja na kufanikiwa au mara nyingi kadri itakavyoonekana inafaa. Kabla ya kufanya kampeni husika ni muhimu kwa wahusika kufahamu mambo ya msingi kuhusu majukwaa ya fedha za uwekeazaji.

Ni muhimu kuwa na uelewa mkubwa wa biashara inayotafutiwa fedha ikiwa ni pamoja na mpango biashara husika. Pamoja na mambo mengine, mpango biashara utaonyesha kiasi cha fedha kinachotafutwa na matumizi yake.

Kila baada ya kampeni moja ni muhimu kufanya hesabu za kiwango cha mafanikio ambacho mara nyingi huwekwa katika asilimia. Kinaweza kuanzia asilimia sifuri hadi 100.

Kufanikiwa

Yapo mambo mengi yanayoweza kuchangia kampeni ya kupata fedha kupitia makundi ya watu mtandaoni kufanikiwa au kutofanikiwa. Haya ni pamoja na aina ya biashara inayotafutiwa mtaji, jukwaa linalotumika, kampeni zinavyoendeshwa na, utayari na uwezo wa wanajukwaa.

Mengine ni imani na uaminifu wa wadau kwa anayetaka kupata fedha husika, uhusiano, umbali kijiografia, mila na desturi kati ya wanajukwaa kwa upande mmoja na anayetafuta fedha kwa upande mwingine.

Hata hivyo, utafiti unahitajika kujua ni nini hasa husababisha kufanikiwa kwa njia hii ya kupata fedha za uwekezaji katika mazingira ya aina mbalimbali.

Tanzania

Njia ya kupata mtaji kupitia makundi ya watu bado ni ngeni Tanzania, hata hivyo, njia hii sio ngeni kwenye shughuli za kijamii kama vile harusi na msiba.

Kuna haja kubwa ya kufanya utafiti katika eneo hili na kutoa elimu na msukumo katika jambo hili. Juhudi na msukumo wa wadau tofauti unahitajika pia ili jamii zianze kuwawezesha wenye mawazo chanya yatakayosaidia kupunguza umasikini nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz