Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kupanda bei ya bidhaa: Tanzania kupanga viwango vipya ya kodi

Bei Za Bidhaa 4.crdownload Bidhaa nyingi zimepanda bei mara baada ya mafuta kua adimu katika soko la dunia

Thu, 14 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati bei za bidhaa mbalimbali ikiwemo petroli na dizeli zikiendelea kupanda, Serikali ya Tanzania imesema itahakikisha bei hizo zinakuwa himilivu kwa kupanga viwango vipya vya kodi ili kuwapunguzia maumivu wananchi.

Kupanda kwa bei ya bidhaa kwa kiasi kikubwa kumesababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, jambo lililoibua changamoto ya mabadiliko ya bei za bidhaa na soko la dunia na kupanda kwa gharama za usafirishaji.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha bei ya bidhaa zinazozalishwa nchini zinakuwa himilivu wakati ikiendelea kufanya tathmini kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi ili kuona namna ya kuleta unafuu.

Pia, Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi hususan wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa ili kupanga viwango vipya vya kodi vitakavyoleta unafuu kwa mlaji kama vile kupunguza kodi ya baadhi ya bidhaa.

Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo Aprili 13, 2022 wakati akihitimisha mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2022/202 ambapo Bunge limepitisha kwa kauli moja bajeti hiyo.

Serikali itaendelea kuhakikisha inaimarisha uzalishaji wa bidhaa za viwandani hasa bidhaa za chakula zinazoingizwa kwa wingi kutoka nje ikiwemo ngano, mafuta ya kula na sukari kwa kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na kutoa vivutio stahiki.

Mbali na hatua hiyo, kiongozi huyo amesema Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa uwekezaji wa ndani kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali ili kukabiliana na aina hii ya mtikisiko wa kiuchumi.

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imetakiwa kuendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali kwenye soko na kuchukua hatua stahiki sambamba na kusimamia vema mfumo wa kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo usioridhisha wa bei za bidhaa sokoni.

“Vilevile, ninazielekeza Mamlaka na Taasisi za Serikali zilizopewa dhamana ya kusimamia mienendo ya masoko ya bidhaa kutekeleza wajibu huo kikamilifu na kwa umakini mkubwa sambamba na kudhibiti vitendo vya upandishaji holela wa bei za bidhaa nchini,” amesema Majaliwa katika hotuba yake.

Amekemea vitendo vya baadhi ya wazalishaji na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kuamua kupanga bei, kufanya mgomo, kukubaliana katika manunuzi na kuzuia uzalishaji, mbinu ambazo wakati mwingine zimekuwa chanzo cha kupanda kwa bei ya bidhaa.

“Wale wote watakaobainika kufanya michezo hiyo, hatutosita kuwachukulia hatua za kisheria,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania waendelee kuwa wamoja na wafanye kazi kwa bidii ili kuufanya uchumi wa Taifa kuwa shindani na wa viwanda kwa maendeleo ya watu.

“Serikali kwa upande wake itaendelea kuhakikisha hakuna uhaba wa bidhaa nchini wakati ikiliangalia vizuri suala la bei na kuona namna ya kutoa unafuu kwa wananchi,” amesema.

Kwa mujibu wa bei mpya za rejereja kwa mwezi Aprili 2022 zilizotangazwa wiki iliyopita na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), mafuta ya dizeli yamepanda kwa zaidi ya Sh250 kwa lita huku petroli ikipanda kwa zaidi ya Sh300 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live