Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Alhaj Abubakar Kunenge ameeleza Nia ya mkoa huo ni kuendelea kufungua mtandao wa miundombinu bora ya barabara inayoakisiana na kasi ya uwekezaji iliyopo mkoani humo.
Aidha, ameeleza, nia ya mafanikio hayo itawezekana endapo kutakuwa na mazingira wezeshi ikiwemo kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji na migogoro ya ardhi.
Akifungua, kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika mjini Kibaha na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Pwani, Kunenge alieleza kuwa, mtandao wa miundombinu bora unatoa fursa kwa wawekezaji, kurahisisha usafiri kwa jamii na kufungua mkoa kiuchumi.
Hata hivyo, alisema mazingira wezeshi yakiimarika na kupunguza migogoro ya ardhi itaisaidia kuinua maendeleo na mkoa kuendelea kuwa kimbilio la wawekezaji.
"Tumechoka migogoro ya wakulima na wafugaji hili ni jambo ambalo kama hatutaliondoa vikwazo vitaendelea kubaki pale pale," Tumeona dhamira ya Rais wetu kufungua mkoa wetu ,hivyo ni wajibu wetu sisi kuangalia barabara zenye tija ,tuangalie mkoa wetu kwa ujumla wake ,tunajua nchi yetu ina vipaombele vingi, lazima tupendekeze miradi yenye hoja ,na inayokubalika yenye kuwagusa wananchi na tija kiuchumi,"
"Tunatakiwa tuwe na hoja inaringanishwa na mikoa mingine, barabara zinasaidia kugusa maisha ya wananchi na kukuza uchumi Lakini ukipata barabara inayogusa wananchi na uchumi inakuwa na tija zaidi "alifafanua Kunenge.
Nae Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoani Pwani (TANROADS) Mhandisi Baraka Mwambage alieleza mpango wa kazi unaoendelea 2022-2023 kwa kutekeleza miradi yenye thamani ya Bilioni 47.022 kutoka Bilioni 41 ya kipindi kilichopita.
Pamoja na hilo ,kuna maelekezo ya Serikali ya kupendezesha miji na mikoa ambapo kazi inaendelea kwa baadhi ya maeneo ikiwemo Kisarawe-Minaki, Mafia-Kilindoni, Bagamoyo Mjini,Kibaha-Chalinze-Segera,Vikindu-Mkuranga, Ikwiriri-Nyamwage.
Baraka alieleza maelekezo ya kazi ya kupunguza msongamano kuboresha barabara ya Mailmoja eneo la ATM-Pichandege, Vikindu-Kisemvule, miradi ya maendeleo Jumla ya Bilioni 23 kwa ajili ya ukarabati na wamefikia asilimia 60 ya utekelezaji.
"Ipo miradi ya kimkakati Kibaha-Chalinze-Ngerengere, Daraja la WAMI ambalo limekamilika, Chalinze-Utete hii ni barabara ambayo ni maelekezo ya mh.Rais"
Baraka alitaja nyingine ni kutoka Kibaha -Mapinga yenye km.14 za umaliziaji ambayo ipo hatua ya mwisho ya manunuzi na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu, barabara ya Mkuranga-Kisiju, Vigwaza hadi Kwala eneo la uwekezaji na ile ya Utete -Nyamwage.
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Muharami Mkenge aliipongeza, TANROADS na TARURA kwa kazi kubwa zinazofanyika na kusisitiza barabara ya Makofia- Mlandizi japo utekelezaji ufanyike kwa awamu.