Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuna majukumu tofauti kwa Serikali, sekta binafsi uchumi wa viwanda

20771 Pic+viwanda TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Leo, kampuni ya Mwananchi Communication, pamoja na mambo mengine, imeandaa mijadala unaozungumzia uchumi wa viwanda. Mjadala huu utafanyika katika mdahalo mkubwa, wa wazi.

Makala haya yanatoa mchango wa mwandishi katika mjadala huu nje ya ukumbi, yakijikita kuainisha majukumu ya Serikali na yale ya sekta binafsi kuelekea uchumi wa viwanda.

Katika kujadili majukumu ya wadau mbalimbali katika uchumi kwa ujumla na viwanda kimahususi, historia ni muhimu. Duniani kote, Serikali huwa na majukumu kadhaa.

Majukumu haya hubadilika kutegemeana na muktadha wa wakati husika baina ya yanayotekelezwa na Serikali na yale ya sekta binafsi. Kwa maana hiyo, kwenye viwanda kuna mabadiliko tangu uhuru wa mwaka 1961 hadi leo.

Mwaka 1961 hadi 1967

Historia ya uchumi wa Tanzania inaonyesha mara baada ya uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, iliendelea na mfumo wa uchumi iliorithi kutoka kwa wakoloni.

Katika ujumla wake, uchumi ulimilikiwa na sekta binafsi. Hii ilikuwa ya wageni waliomiliki njia kuu za uzalishaji mali kama vile mashamba, migodi, benki na posta.

Majukumu makuu ya Serikali yalikuwa kuipanga nchi iliyokuwa imeshinda harakati za kudai uhuru. Serikali ilijikita kutoa huduma na bidhaa za umma. Pia ilitoa mipango ya uchumi kama ule wa mwaka 1964.

Mwaka 1967 hadi 1980

Mabadiliko makubwa ya majukumu ya Serikali na sekta binafsi katika uchumi wa Tanzania yalikuja kwa kasi kubwa mwaka 1967. Huu ni wakati lilipozaliwa Azimio la Arusha.

Jambo kuu katika azimio hili ni utaifishaji wa njia kuu za uchumi. Serikali ilichukua jukumu la kupanga, kumilili na kuendesha njia kuu za uchumi. Takriban mashirika ya umma 400 yalianzishwa katika sekta mbalimbali vikiwamo ya viwanda.

Serikali ilijihusisha moja kwa moja kumiliki na kuviendesha viwanda vilivyotaifishwa. Pia ilianzisha viwanda vipya. Ilikuwa ni enzi ya uchumi hodhi wa serikali.

Katika kipindi hiki, sekta binafsi haikuwa na nafasi kubwa katika uchumi katika viwanda. Tofauti na hali ya miaka ya 1961 hadi kabla ya Azimio la Arusha, sekta binafsi iliwekwa pembeni.

Serikali ilishika hatamu katika uchumi. Hivyo jukumu kuu la uchumi wa viwanda lilikuwa mikononi mwake. Jukumu hili liliendelea hadi katikati ya miaka ya 1980.

Mwaka 1980 hadi 2015

Katikati ya miaka ya 1980 kuelekea mwanzoni mwa miaka ya 1990 majukumu ya Serikali na sekta binafsi katika uchumi yalibadilika. Yalikuwapo mageuzi makubwa, mengi na yaliyofika mbali katika utawala na uongozi wa uchumi.

Serikali ilikumbatia uchumi wa soko ambapo sekta binafsi ilitambuliwa kama injini ya ukuaji wa uchumi. Ni katika kipindi hiki ulifanyika ubinafsishaji wa mali zilizokuwa zimetaifishwa mwaka 1967.

Katika mageuzi haya na mabadiliko ya majukumu, Serikali ilijielekeza kuweka mazingira mazuri, rafiki na ya kuvutia uwekezaji na, uanzishaji na uendeshaji biashara.

Majukumu ya Serikali yalibadilika kutoka kumiliki na kuendesha uchumi moja kwa moja na kuwa muwezeshaji kisera, sheria na udhibiti. Serikali ilihama kutoka kufanya biashara na uwekezaji hadi kuwezesha biashara na uwekezaji.

Katika kipindi hiki, uchumi hodhi wa Serikali ulikwisha na kuruhusu ushindani wa soko unaojumuisha zaidi sekta binafsi huku yenyewe ikisimamia pasiwepo ubepari uliopitiliza ukaharibu maisha ya wananchi wanaopaswa kunufaika zaidi.

Majukumu ya sekta binafsi yalikuwa kumiliki na kuendesha uchumi kwa kumiliki njia zilizotaifishwa mwaka 1967 ambazo sasa zilirudi mikononi mwao. Hivyo majukumu ya kuanzisha na kuendesha viwanda yalikuwa kwa sekta binafsi.

Hili lilikuwa kote; nje na ndani ya nchi; vidogo kabisa, vidogo, vya kati au viwanda vikubwa. Katika sekta binafsi, wote walipaswa kufanya hivyo iwe kwa waliomiliki biashara rasmi hata zisizo rasmi.

Pamoja na mambo mengine, sekta hii ilikuwa na jukumu la kuendesha viwanda vilivyobinafsishwa na kuanzisha vingine vipya kukidhi mahitaji yaliyokuwapo.

Mwaka 2015 hadi sasa

Azma mpya ya kuwa na uchumi wa viwanda inatoa sura mchanganyiko kuhusu majukumu ya Serikali na yale ya sekta binafsi sasa hivi. Kimsingi, mitizamo ya falsafa ya uchumi Tanzania ni ileile ya tangu katikati ya miaka ya 1980.

Bado ni uchumi unaoendeshwa na sekta binafsi huku Serikali ikiwa na majukumu ya kuwezesha kisera, kisheria na kiudhibiti. Hata hivyo kuna mitizamo kuwa majukumu ya Serikali yanataka kuegemea zaidi kama ilivyokuwa kati ya mwaka 1967 hadi katikati ya miaka ya 1980.

Kumekuwapo mwingilio wa moja kwa moja wa Serikali kusukuma azma ya uchumi wa viwanda. Tofauti na majukumu ya miaka ya katikati ya 1980 hadi 2015, Serikali inajihusisha zaidi katika uchumi wa viwanda.

Kwa mfano, inatoa miongozo ya viwanda gani na vingapi vijengwe wapi. Katika uchumi wa sekta binafsi, nguvu za soko hutoa uamuzi huu.

Cha kufanya

Tanzania ina bahati ya kuwa na vipindi ambapo Serikali na sekta binafsi zina majukumu tofauti. Ni muhimu kufanya tathmini ya kina kuhusu nini kiliwezekana na kina hakikuwezekana katika utekelezaji wa majukumu haya tofauti.

Mtizamo mpana ni kila sekta ifanye kila inachoweza kufanya vizuri zaidi. Serikali inapaswa kkufanya uwezeshaji na sekta binafsi imiliki na kuendesha viwanda. Hata hivyo, pale soko linaposhindwa Serikali iingilie kurekebisha mambo.

Chanzo: mwananchi.co.tz