Mhadhiri wa Fedha, Uhasibu na Kodi wa Chuo cha Serikali za Mitaa Dodoma, Charles Matekele amesema madhara ya kufungia biashara ni kupoteza mapato serikalini, kodi hata ajira.
Amesema inapunguza mzunguko wa fedha mtaani, akitolea mfano wa kodi ya ongezeko la thamani na hata kwa wananchi kupoteza ajira.
Matekele ameyasema hayo leo Jumatano Agosti 23, 2023 wakati akichangia mjadala wenye mada isemayo ‘Mamlaka kufungia biashara ni suluhu kwa wanaokiuka utaratibu, nini kifanyike?
Matekele amesema kwa upande wa faida ni kuwakumbusha wafanyabiashara uwepo wa sheria na taratibu zinazopaswa kufuatwa.
“Ni fundisho kwa wafanyabiashara kuweza kukumbuka, uwepo wa sheria zinazotakiwa kufuatwa ili kuepusha hayo yote,” amesema.
Amesema cha kufanywa ili kuzuia hayo yote ni wafanyabiashara wote kufuata kanuni na taratibu ikiwemo kulipa kodi kwa wakati pamoja na kuwa na leseni stahiki.
“Kila mwenye biashara aweze kuwa na mshauri wa kodi ambaye atamsaidia mambo yote ikiwemo kanuni, utaratibu na sheria za kodi,” amesema Matekele.
Mbali ya kuwa na mshauri huyo, Matekele pia ameshauri wataalamu wengine kama wahasibu na wasimamizi ili kuweza kupunguza kadhia zinazoweza kujitokeza.