Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amesema kituo cha kupoza umeme cha Chalinze mkoani Pwani kitakabidhiwa rasmi Desemba 31, mwaka huu, baada taratibu za ujenzi kukamilika.
Ujenzi wa kituo hicho ulioanza Septemba 6, mwaka 2021 umefikia asilimia 84.3 na kitakuwa kinapoza umeme unaotoka katika mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 91.72.
Mradi wa JNHPP, wenye thamani ya Sh6.6 trilioni, unatarajia kuzalisha megawati 2,115 za umeme ifikapo Juni, 2024, umeme unaoelezewa kuwa utasaidia nchi kupata umeme wa uhakika sambamba na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa nishati hiyo itakayochochea shughuli za ukuaji wa uchumi nchini.
Dk Biteko ametoa kauli hiyo jana Chalinze, mkoani Pwani alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambacho ujenzi wake utakamilika mwaka huu. “Nina imani ikifika Desemba mwishoni kitakabidhiwa kwa ajili ya kupokea umeme wa Julius Nyerere. Umeme huu ukifika utasaidia kupunguza changamoto ya nishati inayojitokeza.
“Nalipongeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kusimamia vema na tumehakikishiwa na mkandarasi kuwa ikifika Novemba 30, kazi zote za msingi zitakamilika kisha kuanza majaribio,” amesema Dk Biteko.
Amesema Serikali imetoa fedha nyingi ili kuboresha sekta hiyo, lakini mwishowe Watanzania wanahitaji umeme, ndiyo maana amewaomba wawe watulivu na wavumilivu wakati maboresho mbalimbali yakiendelea kufanyiwa kazi.
“Kipindi hiki cha muda mfupi tunaendelea na taratibu zetu za ndani, ikiwemo matengenezo sambamba na kuongeza uzalishaji wa gesi asilia. Lakini Watanzania tukubaliane kwamba matatizo mengine ya umeme yanatokana na uharibifu wa vyanzo vya maji.
“Hili tunaliangalia ndani ya Serikali kuona namna bora ya kuvilinda vyanzo vyetu ili tusikwamishe shughuli mbalimbali za uchumi zinazotegemea umeme kwa kiasi kikubwa. Watanzania mnataka umeme, tupeni muda kituo chetu kimefikia hatua nzuri na kwa muda tuliopewa na Rais Samia Suluhu Hassan, tutakuwa tumefikia hatua nzuri," amesema Dk Biteko.
Mwezi uliopita, Rais Samia alimpa miezi sita Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gissima Nyamo-Hanga awe amemaliza tatizo la kukatika kwa umeme kwa kuwa yeye hataki kusikia kelele za kukatika kwa umeme, akimtaka kusimamia mchakato wa ukarabati wa mitambo unaoendelea hivi sasa.
“Najua utaweza, nakupa miezi sita, nakuangalia pale Tanesco, kazi yako ya kwanza ni kusimamia ukarabati wa mitambo, lakini baada ya miezi sita, nisisikie kelele za kukatika kwa umeme, tutasaidiana, nenda najua utaweza," alisema Rais Samia.
Hali ya umeme
Septemba 27, mwaka huu, Nyamo-Hanga aliwaambia wanahabari kwamba kuna upungufu wa megawati 400 za umeme. Lakini mapema mwezi huu, Nyamo-Hanga alisema wamepunguza hadi megawati 350 kutokana na matengenezo ya mitambo yanayoendelea kufanyika.
Katika ziara yake jana, Dk Biteko aligusia suala hilo, akisema hivi sasa wamepunguza megawati kati ya 200 hadi 300 kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na Tanesco katika kukabiliana na hali hiyo.
“Kwa mfano, Jumapili iliyopita tulishuka hadi kufikia upungufu wa megawati 150, maana yake ni kwamba hatua za muda mfupi tulizozichukua zimezaa matunda. Niseme tu, tumechukua hatua za makusudi za kupunguza upungufu wa umeme,” alisema Dk Biteko.
Ujenzi wa kituo
Meneja msimamizi wa mradi wa kituo hicho, Mhandisi Newton Mwakifwamba, alisema kituo hicho kitatumika kupoza umeme wa megawati 2,115 utakaozalishwa Julius Nyerere, huku akisema kituo hicho pia kinahusisha njia za umeme.
“Kuna njia zitaingia kusini mwa kituo chetu, kwa kuanzia tutakuwa na njia mbili, lakini baadaye tutakuwa nazo nyingine nne ili kuwezesha kupata megawati 2,115 zitakazotoka bwawani. Njia mbili za kwanza Serikali imefadhili, lakini nne zitafadhiliwa na Benki ya Exim.
“Hizi njia mbili zipo tayari, zitaingilia kusini mwa kituo hiki na kupokewa na mashine zitakazopoza umeme ili kutoharibu miundombinu. Tutaupoza kutoka msongo wa kilovoti 400 hadi 220 ili kuwezesha kuingia kwenye gridi ya Taifa,” amesema Mwakifwamba.
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), amesema mradi wa kituo hicho ukikamilika utakuwa msaada mkubwa wa upatikanaji wa umeme katika maeneo mbalimbali.