Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumbi, ‘ma-Mc’, wapambaji, ‘ma-DJ’ waanza kulipa ada

E00b20e9aaaf979114568e6d14107637.jpeg Kumbi, ‘ma-Mc’, wapambaji, ‘ma-DJ’ waanza kulipa ada

Mon, 25 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WASHEREHESHAJI katika matukio mbalimbali zikiwamo sherehe za harusi, wapambaji, wapishi, wapiga picha jongevu na mnato, wanapiga muziki, pamoja na wamiliki wa kumbi za sherehe katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, wanapaswa kulipia ada kuanzia sasa.

Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema iliyopo mkoani Mwanza, imewataka wamiliki wa kumbi za sherehe kutii sheria ndogondogo kwa kulipia ada ya kila tukio lililoanishwa utaratibu ambao umeshaanza kutumika.

Wamiliki wa kumbi wameandikiwa barua kutaarifiwa kuhusu utaratibu huo wa ukusanyaji mapato ikionesha ukumbi unaochukua watu kati ya 100 na 200 ada yake ni Sh 50,000 wenye watu 200 hadi 5000 ni Sh 100,000.

Barua hiyo iliyoandikwa na Ofisa Utamaduni wa Halmashauri, Emmanuel Kaponoke kwa niaba ya mkurugenzi, inaonesha mshereheshaji anatakiwa kulipa Sh 50,000, mpambaji, mpishi, mpiga picha za mnato na jongevu pamoja na muziki watalipa Sh 30,000 kila mmoja.

Imefafanuliwa kwamba, ili kuondoa usumbufu katika ukusanyaji wa ada hizo na kwa kuzingatia kwamba hao wote wanalipwa na mwenye sherehe ambaye ndiye huomba ukumbi wa kuendeshea sherehe yake, mwenye sherehe ndiye atakayewajibika kulipa ada hizo zote kwa halmashauri na kupatiwa kibali.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kaponoke alifafanua akisema mwenye sherehe atatakiwa kulipia Sh 270,000 ikiwa atahitaji kutumia ukumbi wa watu kati ya 201 hadi 500, na 220,000 kama atahitaji ukumbi wa kati ya watu 100 hadi 200.

"Kamwe mmiliki asiruhusu sherehe kufanyika ndani ya ukumbi wake bila mwenye sherehe kuwa na kibali cha halmashauri. Ikumbukwe kama ada hii ni kwa ajili ya kibali cha halmashauri tu na si gharama ya kukodi ukumbi,"alisisitiza.

Kaponoke alisema kwa upande wa sherehe za nyumbani, endapo ukumbi utachukua idadi ya watu kama ilivyooneshwa kwenye sheria hizo ndogo, atatakiwa pia kulipia ada na vivyo hivyo kwa watoa huduma. Alisema ada hizo ni kwa shughuli za sherehe pekee na si misiba.

Ofisa utamaduni huyo alisema wafanyabiashara hao wameshauriwa kujiunga katika vikundi na kuwasilisha majina katika halmashauri ili suala hilo lijadiliwe na Baraza la Halmashauri na hatimaye ipangwe bei/ada elekezi kwa kikundi badala ya mtu mmoja mmoja.

Alisema huo ni ushauri waliopewa wafanyabiashara hao muda mrefu, lakini hawakuwa tayari kuutekeleza kutokana na sababu mbalimbali zenye mgongano wa kimaslahi.

“Lakini sasa wameanza kujitokeza na kuomba suala hilo (la vikundi) lizungumiziwe upya,” alisema.

Hata hivyo, alisema bei elekezi ya ada ni mpaka pale vikundi hivyo vitakapokuwa vimejasajiliwa na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata).

Kwa mujibu wa Kaponoke, sheria hiyo ndogo ilianza kutekelezwa katika halmashauri hiyo Desemba mwaka jana.

Chanzo: habarileo.co.tz