Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Kuku ni kiwanda tosha’

88446fc65162cf658e24bd97a3d3cac2 ‘Kuku ni kiwanda tosha’

Wed, 16 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

‘KUKU ni kiwanda’. Hiyo ni kaulimbiu ya vijana 48, wasichana 19 na wavulana 29, waliohitimu mafunzo ya kilimo na ufugaji kwa vitendo katika Kambi ya Vijana ya Kilimo na Maarifa iliyoko katika kijiji cha Mkongo wilayani Rufiji, Pwani.

Wakisoma risala baada ya kuhitimu mafunzo ya ufugaji kuku wa kisasa, chotara na wa kienyeji wiki iliyopita, wahitimu hao wanashukuru kupata mafunzo ambayo wanasema wana hakika yatabadilisha maisha yao huku pia wakihimiza jamii kufuga kuku kibiashara na siyo kuishi na kuku.

Wanaziomba halmashauri wanazotoka za Kibaha, Kibiti, Rufiji, Kisarawe, Mkuranga na Kibaha ziwapatie maeneo ya kilimo na ufugaji na pia ziwapitie vifaranga na mitaji.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, mmoja wa wahitimu hao, Issa Malamua anayetokea Kibiti, anasema shughuli yake kubwa ni kilimo na kwamba mafunzo hayo, mbali na kumsaidia kuboresha uelewa wake wa kilimo, lakini umempa ujuzi wa ufugaji.

“Nimekuwa nikilima ufuta, korosho na mahindi. Lakini sasa nimeongeza ujuzi wa kufuga. Nilikuwa sijui tofauti katika kufuga kuku wa kisasa na wa kienyeji lakini kutokana na mafunzo niliyopata ninajua. Nimejifunza vitu vingi hususani tofauti ya namna tunavyofuga na kufuga kuku kibiashara. Sisi tunaishi na kuku wakati tunatakiwa kuwafuga kibiashara,” anasema.

Malamua ambaye ana familia ya mke na watoto wawili, anasema cha kwanza anachokwenda kufanya nyumbani ni kitoa elimu kwa familia, jamaa na marafiki kuhusu namna kufanya ufugaji wa kisasa.

Kijana huyo anasema baada ya kuhitimu mafunzo amekuwa katika mawazo makali ya namna ya kupata mtaji ili kufuga kuku chotora. Anasema mtaji anaotaka ni wa kumsaidia kujenga banda la kisasa, kununua vifaranga, chakula na dawa za kuanzia.

Mkurugenzi wa Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUGECO), Revocatus Kimario wanaoendesha kituo hicho, anasema tangu kambi hiyo imeanzishwa mwaka 2015, imeshatoa wahitimu wa kilimo na ufugaji kwa vitendo wapatao 1,461 kutoka maeneo mbalimbali, hususani ya mkoa wa Pwani.

Anasema katika mafunzo yao, asilimia 20 ndio wanayofanyia darasani lakini asilimia 80 ya mafunzo hufanywa kwa vitendo na kwamba ndani ya wiki mbili, kijana anakuwa ameshaiva.

Anasema wamekuwa wakipenda sana kutumia vitu vinavyopatikana katika mazingira ya kawaida na ndio maana hata mabanda ya kuku yaliyopo kambini, baadhi wamejenga kwa kutumia miti, udongo na nyasi.

Anasema wamekuwa pia wakitoa elimu kwa wananchi, hususani wa kijiji cha Mkongo ilipo kambi hiyo.

Kimario anasema baadhi ya vijana waliowafundisha wanaotokea katika kijiji cha Mkongo na sasa wanawatumia kuwafundisha wenzao akiwemo Daudi Mohamed anayefundisha ufugaji wa kuku chotara.

Mkurugenzi huyo anasema wamekuwa pia wakiwafuatilia wahitimu wao na kugundua kwamba wengi wamejiajiri na wachache wameajiriwa katika sekta ya kilimo na ufugaji na kwamba mafunzo waliowapa yamewasaidia kubadilisha maisha yao.

Anasema kambi hiyo ina vitalu-nyumba (green houses) saba na kwamba endapo watapata maji wataboresha zaidi mafunzo ya kilimo biashara kwa njia ya umnwagiliaji.

Akizungumzia changamoto wanazokabiliana nazo, Kimario anazitaja kuwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu, uchakavu wa trekta na kuharibika kwa gari kwenye kambi na kukosekana kwa maji ya kutosha ili kuendesha kilimo cha umwagiliaji.

“Mheshimiwa mgeni rasmi, hapa tunakaa na vijana wengi lakini hatuna gari. Ikitokea mmoja akaumwa ghafla usiku inakuwa shida kumwahisha hospitali,” anasema.

Changamoto nyingine anasema ni upungufu wa matundu ya vyoo na kukosekana kwa bwalo la kutosha la chakula.

Anasema baadhi ya vijana hupata nafasi ya kwenda Israel kujifunza kilimo lakini wanapofika kule wanakuwa hawana utaalamu wa kuendesha mitambo kwa maana ya matrekta.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo analishukuru Shirika la Chakula Duniani (FAO), ambao ndilo mdhamini mkubwa wa mafunzo katika kambi hiyo.

Halikadhalika amelishukuru Shirika lisilo la kiserikali la Cusor ambalo limewadhamini Dola 10,000 kwa ajili ya kuanzisha mkakati utakaoiwezesha kambi hiyo kuendesha kilimo cha maembe na maharagwe.

Kimario anasema wanajielekeza kwenye maembe kwa sababu viwanda vingi vya juisi vinalazimika kuagiza maembe nje ya nchi wakati yanaweza kulimwa hapa hapa nchini kisasa.

Mwakilishi wa FAO, Charles Tulahi, anawataka wahitimu hao kuunda mitandao na kuendesha kilimo au ufugaji wa kibiashara kwa umoja ili kupata mafanikio ya haraka.

Anawataka pia wahitimu hao kujiendeleza zaidi kielimu kwa sababu mafunzo hayo ya muda mfupi yatakuwa yamewapa mwanga utakaowafikisha mbali.

Anasema wakiwa na nidhamu ya kazi watafika mbali. “Kuna kijana mmoja alianza kilimo cha parachichi kwa miche minane. Lakini kwa sababu ya nidhamu na kutafuta elimu, leo hii ana ekari 40 na kwa kweli anaweza hata kuniajiri mimi kutokana na pesa anazoingiza,” anasema Tulahi.

Anasema wao FAO wataendelea kushirikiana na serikali na taasisi kama Sugeco katika kuhakikisha kilimo kinashamiri nchini ili kupambana na njaa.

Anasema kwa ushirika na Sugeco, wameanzisha pia ushirikiano na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ili kuboresha shughuli za uzalishaji kwa kupata vitu kama vifungashio na kuwezesha kilimo kuwa cha kibiashara zaidi.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Revocatus Nandi, anawahakikishia vijana waliohitimu kwamba wakajiunga katika vikundi, halmashauri ziko tayari kuwapa mikopo.

Anafafanua kwamba mikopo hiyo inatokana na asilimia 10 inayotengwa ambapo asilimia nne zinakwenda kwa vijana, nne kwa wanawake na mbili walemavu. Anasema halmashauri pia zinaweza kuwapa maeneo ya kuendesha shughuli zao za kilimo na ufugaji wakiwa katika vikundi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mafunzo hayo anaahidi serikali kupanua kambi hiyo ili kiwe kituo kikubwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Katibu Mkuu pia anaahidi kutatua baadhi ya changamoto za kituo hicho kinachoendeshwa kwa ufadhili wa FAO ikiwa ni pamoja na kuvuta maji kutoka kwenye bwawa lililo jirani na kambi.

Anaahidi pia kukitafutia kituo gari kutokana na lililopo kuharibika, kukipa kituo trekta dogo (power tiller) pamoja na pikipiki mbili.

Anawataka wahitimu hao kusambaza ujuzi walioupata kwa wengine huku akihimiza Watanzania kujikita katika kilimo cha kisasa kwani kina manufaa.

“Kwa mfano, wenzetu wa Misri wanataka mahindi ya njano tani milioni 1.5 kutoka kwetu kila mwaka. Kwa hiyo ni vyema Watanzania wakachangamkia fursa kama hizi,” anasema na kuongeza kwamba ajira milioni nane zilizoahidiwa na serikali ya Rais John Magufuli katika kipindi hiki cha miaka mitano, sehemu kubwa zitatokana na kilimo.

Anawaagiza Sugeco kukifanya kituo kujiendesha kibiashara kwa kulima na kuuza mazao na kuongeza muda wa mafunzo kutoka wiki mbili za sasa ili vijana wakitoka kambini wawe wameiva zaidi.

Chanzo: habarileo.co.tz