Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kukamilika gati namba tano chachu ya ufanisi Bandari Dar

0bea30d2f0b9ecac62b5555ff337e7d3 Kukamilika gati namba tano chachu ya ufanisi Bandari Dar

Thu, 11 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

GATI namba tano la Bandari ya Dar es Salaam limeshaanza kufanya kazi, hatua ambayo inazidi kuchagiza mchango wa bandari hiyo muhimu nchini katika kuchangia ukuaji wa uchumi.

Kuanza kufanya kazi kwa gati hilo ambalo lilikuwa ni sehemu ya mradi wa kuboresha huduma za bandari nchini, ni matokeo ya utekelezwaji wa agizo la Rais John Magufuli alilotoa kutaka kuboreshwa kwa huduma za bandari.

Uboreshaji pamoja na ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ni kubwa kuliko zote nchini ulianzia gati namba 0 maarufu kama Roll in Roll Out (Roro) na hadi sasa umefikia gati namba tano lililoanza kupokea meli za kila aina.

Ujenzi wa Gati Namba 4 na 5 ni sehemu ya mradi mkubwa wa Dar es Salaam Maritime Gateway Project (DMGP) wenye lengo la kupanua na kuboresha Bandari ya Dar es Salaam.

Tayari ujenzi wa gati maalum ya magari, Gati Namba 1 mpaka 3 umeshakamilika na gati hizo zimeshaanza kutumika.

Akizungumzia kuhusiana na gati namba tano lililokamilika na kuzinduliwa hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko anasema kutokana na ukubwa wa gati hiyo, meli kubwa na za kisasa zitahudumiwa wakati wa kushusha mizigo.

Anasema hatua hiyo itachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mapato hasa kutokana na uwezo wake wa kupokea meli nyingi na kwa wakati.

“Gati hili namba tano ni sehemu ya mwendelezo wa gati za bandari hii ambao ulianza tangu gati namba Sifuri kisha kuishia gati namba nne na leo umekamilika ujenzi wa gati namba tano. Magati mengine yote yameendelea kusaidia upokeaji wa mizigo kwa ufanisi zaidi.

Gati namba sita na saba nazo mafundi wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha zinakamilika kwa wakati na hivyo kuanza kuchangia uchumi wa nchi,” anasema.

Anasema kuwa ujenzi wa gati namba sita utakamilika kwa asilimia 100 mwezi ujao kwani kwa sasa umefikia asilimia 96 na kwamba ujenzi wa gati namba saba unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Agosti.

Katika kuhakikisha kuwa mazingira ya uingizwaji wa mizigo kwenye bandari ya Dar es Salaam unaongezewa ufanisi zaidi, Kakoko anasema, magati yote kuanzia namba tano, sita na saba yana eneo kubwa la kuhifadhia makontena kabla ya kusafirishwa.

Anasema maeneo hayo yanaweza kuhifadhi idadi kubwa ili kuhakikisha kuwa licha ya wingi wa meli kuingia bandarini hapo lakini pia kuwe na uwezo wa kuhifadhi makontena.

Licha ya uboreshwaji wa gati hiyo namba tano, gati namba sifuri ambayo inatumiwa na meli za kusafirishia magari tangu kukamilika kwake imeshahudumia meli kubwa za kisasa ambazo awali zilikuwa hazina uwezo wa kutumia bandari hiyo.

Mwandishi wa makala haya alishuhudia meli ya Jolly Titanic ikiwa imeegeshwa huku kukiwa na magari kibao yanayoingia nchini.

Akizungumzia ujio wa meli hiyo ambayo ni matokeo ya maboresho gati hilo, Kakoko anasema kuwa ilianzia kushusha mizigo yake katika bandari ya Afrika Kusini kisha Mombasa nchini Kenya na kwamba ni kati ya meli kubwa ambazo awali zilikuwa haziwezi kushusha mizigo hapa nchini.

“Lakini kutokana na maboresho hayo kwa sasa meli hiyo inaweza kushusha mzigo hapa,” anasema.

Katika kuhakikisha meli nyingine kubwa zinashusha mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, Kakoko anabainisha uwepo wa mradi wa kuchimba kina zaidi cha bahari kutoka upana wa 10.5 hadi 15.5 ili kuwezesha meli pana zaidi kupita.

Anasema mradi huo ukikamilika utawezesha meli kubwa zaidi ambazo kwa sasa haziwezi kutumia bandari ya Dar es Salaam kuweza kuitumia.

Bandari ya Dar es Salaam inategemewa na nchi kadhaa zikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa Congo na nyinginezo.

Katika muktadha huo, Kakoko anabainisha kuwa TPA wana mradi ambao utaunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na hivyo kuwezesha shehena kusafirishwa na reli hiyo itakapokamilika.

Anasema mradi huo unatazamiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.

Anasema reli hiyo itaunganishwa na maeneo yanayohifadhi makontena ili kuyasafirisha haraka kupitia reli ya kisaa kwenda mikoa mbalimbali na hadi nje ya nchi.

“Hatua hiyo itaiweka Tanzania kuwa kati ya nchi chache zenye bandari zinazosafirisha mizigo kwa njia ya reli ya kisasa, na hapo bandari itakuwa imefunguliwa zaidi njia katika kutoa hudma,” anasema Kakoko.

Anasisitiza kwamba ili shughuli za kibandari zifanye kazi kwa ufanisi, TPA imeziunganisha taasisi zaidi ya 30 za serikali kwenye mfumo wa matumizi ya teknolojia yanayomwezesha mteja kuhudumiwa bila ya kufika ofisi za bandari.

Kakoko anajigamba kuwa licha ya ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona kuathiri biashara nchi mbalimbali duniani, TPA kwa mwaka wa fedha 2019/20 imekusanya Sh bilioni 900 katika bandari zake zote nchini.

Tanzania ni moja ya nchi ambazo hazikufunga mipaka yake hususan kwenye usafiri wa maji kama zilivyofanya nchi nyingine duniani, hivyo kuifanya sekta hiyo kuendelea kuchangia pato la taifa.

Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Leornald Chamuliho, aliyeshiriki kwenye uzinduzi wa gati hiyo namba tano na kushuhudia meli ikitia nanga kwenye gati husika anasema hiyo ni ishara kuwa kazi ya Rais Magufuli ya kufungua uchumi wa nchi inazidi kupamba moto.

Anasema, kama bandari zetu zikitumika ipasavyo zitachangia zaidi ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kutokana na jiografia ya Tanzania inayoifanya kuwa nchi muhimu katika kuhudumia nchi jirani zisizokuwa na bandari.

Anasisitiza: “Nimeshuhudia ujenzi ukiendelea katika gati namba sita na saba ambapo ninataka TPA ihakikishe kuwa ujenzi unakamilika kwa wakati uliowekwa ili magati haya yaanze kuchangia uchumi.”

Anaongeza: “Nimefurahi kusikia kuwa kutokana na kukamikika kwa gati namba tano tayari kuna meli kubwa zimeshaanza kushusha mizigo. Hii inamaanisha kuwa tayari uwekezaji uliowekwa kwenye kuimarisha bandari unaanza kuzaa matunda,” anasema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz