Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kudorora uchumi wa dunia na maana yake kwa Tanzania

38259 Honest+pic Kudorora uchumi wa dunia na maana yake kwa Tanzania

Fri, 25 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Taarifa za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinaonyesha kuwa uchumi wa dunia utadorora kwa mwaka 2020.

Kudorora kwa uchumi kunapimwa kwa vigezo kadhaa kikiwamo cha ukuaji wa uchumi.

Ukuaji wa uchumi ni ongezeko la thamani ya fedha ya bidhaa na huduma zinazozalishwa katika uchumi.

Ukuaji wa uchumi wa dunia

IMF inatabiri uchumi wa dunia utakua kwa wastani wa asilimia 3.5 kwa mwaka huu na asilimia 3.6 kwa mwaka 2020 ikiwa ni punguzo la asilimia 0.2 na 0.1 kutoka katika matarajio ya Oktoba 2018.

Ukuaji katika ukanda wa sarafu ya Euro utashuka kutoka asilimia 1.8 ya 2018 hadi 1.6 kwa 2019 ikiwa ni punguzo la asilimia 0.2 kutoka makadirio ya Oktoba 2018.

Uchumi wa Marekani utakua kwa asilimia 2.5 kwa 2019 na 1.8 kwa 2020 ikiwa ni udororadi wa asilimia 0.7.

China ambayo ni karakana ya dunia itabakia katika matarajio ya awali ya ukuaji kwa asilimia 6.2 kwa 2019 na 2020.

Nchi zinazoendelea ukuaji utatoka asilimia 4.7 hadi 4.5 kwa wastani. Ikumbukwe kuwa ukuaji Tanzania unakadiriwa kuwa asilimia saba japokuwa Benki ya Dunia inasema ukuaji utakuwa chini ya asilimia hiyo.

Sababu za kudorora

Kuna sababu kadha wa kadha zinazosababisha kudorora kwa uchumi wa dunia hasa udhaifu katika uchumi wa Ulaya.

Kwa upande wa Ujerumani ambayo ndiyo moyo wa uchumi wa Ulaya, sekta yake ya magari inakumbwa na mtikisiko kwa kuwapo matakwa mapya ya kimazingira hasa katika hewa ukaa.

Italia ina mgogoro wa kibajeti na Umoja wa Ulaya.

Yote haya yanachangia katika udhaifu wa uchumi wa Ulaya. Sababu nyingine ni vita vya biashara na visasi.

Tumeona vita hivi kati ya Marekani na China; Marekani na Uturuki na kwingineko duniani. Vita na visasi hivi vinaathiri ukuaji wa uchumi kwa njia hasi na kuchochea udororaji wa uchumi.

Udororaji unatokana pia na ukuaji hafifu kuliko matarajio kama takwimu hapo juu zinavyoonyesha.

Suala la Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya linaleta sintofahamu katika uchumi wa dunia, hivyo kuweza kusababisha kutokea dhoruba ya kiuchumi kupitia katika masoko hasa ya fedha.

Vilevile sera za kibiashara zisizotabirika na zenye shaka zinasababisha faida kupungua na hata mitaji kuhama kutoka nchi zinazoendelea. Sababu nyingine ya shaka katika afya ya uchumi wa dunia ni bei za nishati ya mafuta kupanda na kushuka bila kutabirika.

Athari kwa Tanzania

Udororaji wa uchumi wa dunia una uwezo wa kuathiri nchi yoyote ulimwenguni hasa Tanzania.

Hii ni kweli kwa nchi iliyo na milango wazi na kushiriki katika masuala ya kiuchumi na kibiashara kimataifa. Masuala haya ni pamoja na biashara ya kimataifa ikiwamo mauzo na manunuzi ya bidhaa na huduma nje ya mipaka ya nchi husika.

Athari nyingine ni uwekezaji hasa wa mitaji kutoka nje, mikopo na misaada kutoka nje. Udororaji wa uchumi wa dunia huleta kusinyaa kwa biashara za kimataifa na faida zake.

Faida hizi ni pamoja na fedha za kigeni na ajira za moja kwa moja na zisizo za kudumu. Udororaji hupunguza mitaji kutoka nje na pia huweza kupunguza uwezo na utayari wa watalii kutoka nje kuja nchini.

Hii hutokea kama udororaji umewapunguzia vipato watalii watarajiwa au hata kama unatishia kufanya hivyo.

Hii ni kweli pia kwa Watanzania na mabinti wa nchi walio ughaibuni ambao hutuma fedha nyumbani.

Udororaji ukipunguza vipato vyao au kutishia kufanya hivyo, Watanzania na mabinti hawa huweza kupunguza fedha wanazotuma nyumbani.

Hali hiyo siyo tu huathiri wanufaika wa moja kwa moja wa fedha hizi bali pia nchi kwa maana ya kiasi cha fedha za kigeni kinachoingia nchini kupungua.

Nini cha kufanya

Suala la msingi ni nini cha kufanya kama nchi ili kupunguza na hata kuepuka athari za mdororo wa uchumi duniani.

Kufahamu na kukubali kuwa kuna hatari ya mdororo wa uchumi wa dunia kuathiri Tanzania ni hatua moja ya maana sana.

Baada ya hapo ni kuchukua hatua mbalimbali za kupambana na hali hii.

Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza mipango ya kukuza uchumi, kuweka na kutekeleza sera za kupunguza udororaji zaidi na kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na sera panuzi za kifedha na kikodi. Ni muhimu kufanya haya mapema kwa sababu ni afya zaidi kiuchumi kuziba paa wakati bado jua likiwaka kuliko kufanya hivyo mvua itakapoanza kunyesha.



Chanzo: mwananchi.co.tz