Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kubadilisha fedha Arusha kwenye mabenki, hoteli za kitalii

28719 Pic+fedha TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kuyafunga maduka ya kubadilishia fedha yanayokiuka sheria, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema huduma ya kubadilisha fedha jijini Arusha inapatikana katika benki za biashara na hoteli za kitalii.

Wiki iliyopita, Novemba 19, BoT kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliendesha ukaguzi wa kushtukiza kwenye maduka hayo na kubaini ukiukwaji wa sheria na utaratibu wa biashara hiyo huku wengi wakiwa hawajakidhi vigezo hivyo kutakiwa kurejesha leseni na kufunga biashara zao.

Tangu kufanyika kwa operesheni hiyo, huduma hazijarudi lakini jana naibu gavana wa BoT, Dk Bernard Kibesse alisema huduma ya kubadilisha fedha inapatikana kwenye benki za biashara, maduka ya kubadilishia fedha na hoteli za kitalii kote nchini kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuutarifu umma kuwa huduma za kubadilisha fedha za kigeni jijini Arusha zinapatikana kwenye hoteli za kitalii na benki za biashara kwa mujibu wa sheria na kanuni za Benki Kuu ya Tanzania, “ alisema Dk Kibesse. Benki hiyo iliwashukuru wakazi wa Arusha kwa uelewa na ushirikiano walioutoa kufanikisha operesheni hiyo.

Akitoa taarifa ya ukaguzi huo wiki iliyopita, gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga alisema ulikuwa ni wa tatu baada ya benki hiyo kufanya uchunguzi na kugundua uwepo wa maduka bubu mengi yanayofanya biashara ya kubadilisha fedha.

Vilevile, alikiri udhaifu uliopo ndani ya taasisi hiyo nyeti uliowaruhusu baadhi ya wafanyabiashara kutoa taarifa za uongo ili kupata leseni ya kufanya biashara ya kubadilisha fedha bila kukidhi vigezo.

Tangu siku ya ukaguzi huo mpaka leo, maduka hayo hayajafunguliwa na waliokutwa na tuhuma wamekabidhiwa kwenye vyombo vya sheria.



Chanzo: mwananchi.co.tz