Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Kuanzishwe karakana ya taifa kuchakata ngozi’

Ngoziiiii.jpeg ‘Kuanzishwe karakana ya taifa kuchakata ngozi’

Sun, 26 Mar 2023 Chanzo: Habarileo

Wahadhiri katika Taasisi ya ufundi Stadi nchini Ethiopia (TVET) wameishauri Tanzania kuanzisha karakana ya taifa ya kuchakata ngozi, ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo.

Wahadhiri hao kwa sasa wako katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Kampasi ya Mwanza, kwa utekelezaji wa programu za kubadilishana ujuzi kati ya taasisi hizo mbili.

Mhadhiri Msaidizi, Selamu Haile, aliliambia gazeti hili jana kwamba karakana ni moja ya soko kuu la ngozi kwa wafugaji.

“Nchini kwetu tunayo. Pamoja na mambo mengine, inasaidia kuzuia upotevu wa ngozi na hivyo kukuza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali,” alisema.

Alizitaka mamlaka husika nchini zitoe elimu kwa umma wakati wote, kwa wafugaji kutambua utunzaji wa ngozi mara tu baada ya kuchinja mnyama, ili zifike katika karakana zikiwa katika ubora unaotakiwa.

Alisema elimu hiyo ni pamoja na kuhakikisha ngozi haiwekwi chini/ardhini mara baada ya kuchunwa kwenye mnyama, badala yake ining’inizwe ukutani.

“Inampasa mchuna ngozi kuipaka chumvi ya kutosha ngozi hiyo, endapo hana uhakika wa kuifikisha kwenye karakana ndani ya saa mbili,” alisema Haile ambaye yuko DIT kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kutengeneza viatu vya ngozi aina mbalimbali.

Aidha, alisema haipaswi kuanikwa nje kwenye jua, kwani mionzi ya moja kwa moja inaathiri ubora wa malighafi hiyo.

Kwa upande wake, Mhadhiri Msaidizi, Loza Guadie, ambaye yuko DIT kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kutengeneza mikoba, hasa ya wanawake, alisisitiza kuwa karakana ya taifa ni muhimu kwani inachochea ukuaji wa viwanda vya bidhaa za ngozi, kutokana na kuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi.

Aliitaka serikali ihakikishe ina watafiti wa kutosha wa masoko ya bidhaa za ngozi ndani na nje, ili kufanya uzalishaji kulingana na mahitaji ya wateja.

Chanzo: Habarileo