Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Korea yawekewa mazingira mazuri ya kuwekeza Tanzania

Korea Yawekewa Mazingira Mazuri Ya Kuwekeza Tanzania Korea yawekewa mazingira mazuri ya kuwekeza Tanzania

Sat, 25 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ameeleza kuwa Serikali na wadau inaendelea kuweka jitihada katika kuboresha mazingira ya biashara baina ya Tanzania na Jamhuri ya Korea ili kuendelea kuinua kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili.

Waziri Dkt. Tax ameeleza hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Mhe. Kim, Sun Pyo mapema tarehe 24 Machi 2023 jijini Dodoma.

Dkt. Tax amemuhakikishia Balozi Kim kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na Jamhuri ya Korea ili kuwezesha biashara baina ya pande hizo mbili inaendelea kushamiri zaidi tofauti na ilivyo sasa. Dkt. Tax ameeleza baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania ni pamoja na kuendelea kutekeleza na kubuni programu zinazolenga kuongeza mwingiliano wa watu (people to people exchange) kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) za mwaka 2020, Korea iliagiza bidhaa zenye thamani ya shilingi za Tanzania bilioni 340.3 kutoka Tanzania, huku Tanzania ikiagiza bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 290.3 kutoka Jamhuri ya Korea.

Kwa upande wake Balozi Kim, Sun Pyo ameeleza kuwa Jamhuri ya Korea inaendelea kuwahamasisha watu wake kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara zinazopatikana nchini ikiwemo katika sekta ya kilimo, viwanda, ujenzi wa miundombinu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Utalii.

Takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka saba (2015-2022), Korea imewekeza nchini dola za Kimarekani milioni 18.01 katika sekta mbalimbali zikiwemo za kilimo, ujenzi na usafirishaji na uchukuzi. Uwekezaji huo unakadiriwa kuzalisha fursa za ajira zipatazo 531.

Mbali na hayo Waziri Tax ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali zinazolenga kuboresha hali ya maisha ya watu ikiwemo elimu, afya, kuendeleza uchumi wa buluu, kilimo, Teknolojia ya Habari na ujenzi wa miundombinu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live