Kongamano la Viongozi wa Biashara la Vijana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC 2022) linaloanza leo linawakutanisha wafanyabiashara vijana 2000 jijini Arusha ili kuchochea ubunifu wa biashara unaoongozwa na vijana na kukuza biashara ya nje kwa wanawake na vijana, imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mtendaji Mkuu wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), John Kalisa, kongamano hilo litawakutanisha Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye ni Mlezi wa Jukwaa la Youth Leadership Summit (YouLead) na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Dk Peter Mathuki na litafikia tamati Desemba 16, mwaka huu.
Wengine wanaotarajiwa kushiriki kongamano hilo la 6 kwa EAC, ni pamoja na Mwenyekiti wa EABC, Angelina Ngalula, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mafunzo cha Ushirikiano wa Maendeleo cha MS, Makena Mwobobia, mawaziri wakuu biashara wa nchi za EAC na watunga sera katika sekta ya umma.
“Kongamano hili litasaidia ubunifu wa biashara unaoongozwa na vijana na hivyo, kukuza biashara ya kuuza nje kwa vijana na wanawake,” alisema Kalisa na kuongeza kuwa washiriki watajadili mambo mbalimbali zikiwemo fursa kwa wanawake na vijana wajasiriamali wa biashara katika Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).
Kwa mujibu wa Kalisa, pamoja na mambo mengine, mwaka huu washiriki watajadiliana na jopo la viongozi wa biashara kuhusu fursa kwa vijana katika AfCFTA, kuangalia muktadha wa Itifaki ya Masoko ya Pamoja ya EAC na AfCFTA na kuangazia Tuzo za Biashara za Vijana za EAC (EAC-YEA).