Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kizungumkuti bei ya mafuta

Mafuta Ya Petrol Kizungumkuti bei ya mafuta

Fri, 8 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tunaishije katikati ya maumivu ya kupanda kwa bei za bidhaa muhimu yakiwamo mafuta? Ndilo swali linaloumiza kichwa cha kila Mtanzania, hususan wa kipato cha chini.

Tangu Januari, takwimu za Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji zinaonyesha kupanda bei ya bidhaa muhimu, zikiwamo nafaka kama vile ngano, mchele na maharage, mafuta ya kupikia na sukari, hali inayofanya wananchi walalame kila kona ya nchi.

Hata hivyo, Tume ya Ushindani (FCC) na Wizara ya Viwanda kabla jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hajaongeza msisitizo, imeshatoa onyo kwa wafanyabiashara wanaopandisha bei kiholela. Tayari viashiria vya ukali wa maisha vimeanza kuongezeka.

Miongoni mwa viashiria hivyo ni pamoja na tangazo la nia ya kupandisha viwango vya nauli za usafiri wa mabasi ya mikoani hata daladala.

Wamiliki wa malori yanayosafirisha bidhaa kutoka mikoani wamesema kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, nao watapandisha bei ya usafirishaji wa bidhaa.

Kutokana na mazingira hayo, baadhi ya wananchi wameonyesha wasiwasi wa kumudu maisha mapya siku za usoni kama kipato chao pia hakitabadilika.

Advertisement Pamoja na ugumu huo unaotarajiwa, wachumi wameshauri namna ya kukabiliana na hali hiyo wakisema wananchi wanapaswa kubadili mfumo wa maisha kwa kuanza kupunguza matumizi ya mafuta, sukari hata safari zisizo za msingi.

Hata hivyo, wasiwasi bado umetanda kwa wananchi. Elizaberth Ngowi, mshauri wa masuala ya uchumi mjini Moshi alisema wananchi wanatakiwa kuhifadhi vyakula na kuvitumia kwa ustaarabu kuepuka athari za kupanda kwa bei za bidhaa kutokana na ongezeko la bei ya mafuta duniani.

Mafuta ambayo ni muhimu kwa usafirishaji wa vyakula kutoka mikoani yataathiri bei hizo kwa vyakula kutoka vijijini kuingia mjini.

SOMA: Bei ya petroli yagonga Sh2,861

Licha ya Waziri January Makamba kuufuta ushuru wa Sh100 kwenye kila lita moja ya petroli, dizeli na mafuta ya taa mapema Februari, Rais Samia Suluhu Hassan alisema uamuzi huo haukuwa sahihi, kwani mapato yaliyotarajiwa ni sehemu ya bajeti, akairejesha.

Tathmini ya Serikali alisema inaonyesha hata ikiondolewa bado haitasaidia, hivyo akawataka mawaziri kuwaeleza wananchi ukweli juu ya athari za ongezeko hilo la bei ya mafuta linalochangiwa na vita ya Russia na Ukraine.

Shija Magashi, mkazi wa Geita mjini alisema kuirejesha Sh100 kumeendelea kuongeza makali ya maisha hasa kwa wafanyabiashara ndogondogo.

“Kama mfariji wa Taifa tunamuomba Rais Samia alitazame upya suala hili, awafariji Watanzania. Serikali ya Kenya kwa mfano imechukua hatua kufidia baadhi ya gharama ili kupunguza bei ya mafuta, tunamuomba mama alitazame hili kwa umakini,” alisema Shija.

Waziri Makamba

Juzi, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema kuna mambo Serikali inaweza kuyafanyia kazi kuhakikisha gharama za mafuta zinapungua na miundombinu ya bandari inakuwa rahisi katika ushushaji wa nishati hiyo ili kutoongeza gharama ya mafuta.

Alisema Serikali ina ushirikiano mzuri na Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta (Taomac) na wadau wengine kuyafanyia kazi mapendekezo waliyoyatoa.

SOMA:Waziri azungumzia mwenendo bei ya mafuta

“Tunayafanyia kazi na katika Bunge la Bajeti tutatoa taarifa na mwelekeo wa mambo mapya makubwa ya kimageuzi yatakayofanyika katika sekta hii, ikiwamo hifadhi ya Taifa. Tumeandaa waraka tutakaoupeleka kwa ajili ya uanzishaji na kanuni mpya za hifadhi ya Taifa ya mafuta ili inapotokea kama hivi basi tuwe na uwezo wa kuhimili mabadiliko haya,” alisema Makamba.

Msimamo wafanyabiashara

Wakizungumza na Mwananchi, madereva bodaboda, bajaji, magari na Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro (Akiboa) walisema kupanda kwa gharama za usafirishaji hakuepukiki kipindi hiki.

Wakati madereva wakisema hayo, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imetangaza kukutana na wadau Aprili 13 kupokea maoni ya mapendekezo ya viwango vipya vya nauli za mabasi nchini.

Wakati Latra wakisema hayo, msemaji wa Chama wa Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo amewataka abiria kujiandaa kwa ongezeko la nauli kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta duniani.

“Taboa tumeshafuata utaratibu wa kuwasilisha maombi na maelezo ya mapato na matumizi ya kampuni za mabasi kwa mwaka kwenda Latra kwa ajili ya mchakato wa nauli mpya kwa kuzingatia gharama za ununuzi, bei na thamani halisi ya mabasi kwa sasa,” alisema Mwalongo.

Mbali na hao, wafanyabiashara na wasafirishaji mkoani Kilimanjaro walisema endapo Ewura hawatatangaza nauli mpya watasitisha huduma kwa abiria.

Mwenyekiti Akiboa, Hussein Mrindoko alisema hawana nia ya kugoma ila wakishindwa kumudu gharama za mafuta watasitisha huduma za usafirishaji.

Hali ilivyokuwa jana

Baadhi ya madereva wa daladala na bajaji jana walilazimika kupandisha nauli wakidai sababu ni kupanda kwa bei ya mafuta.

Mwananchi lilishuhudia nauli kutoka Moshi mjini kwenda Bomang’ombe ikipanda kutoka Sh1,000 hadi Sh1,500, huku bajaji kutoka Moshi mjini kwenda Majengo ikipanda ikitoka Sh500 hadi Sh 1,000.

Dereva wa lori linalosafirisha bidhaa kutoka mikoani, Rashid Omary alisema Serikali ingepaswa kutafuta namna ya kufidia kunusuru upandaji wa bei ya mafuta.

“Kwa namna mafuta yalivyopanda kama kutoka Tanga hadi Dar es Salaam nilikuwa nachaji Sh400,000, sasa hivi lazima itafika Sh600,000 na wenye bidhaa nao lazima watapandisha,” alisema Rashid.

Jicho kwenye tozo

Kutokana na athari hizo, uchambuzi wa tozo zinazokusanywa na Serikali katika kila lita moja ya mafuta unaonyesha kuna uwezekano wa Serikali kuzirekebisha ili kushuka bei.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki na Wamiliki wa Vituo vya Mafuta Tanzania (Tapsoa), Tino Mmasi alishauri Serikali kutazama tozo mbili za Umeme Vijijini (Rea) na ushuru wa maendeleo ya reli kati ya Sh17.44 hadi Sh18.19.

“Miradi ya Rea imekamilika hivyo tozo zake zinaweza kuondolewa. Tozo ya reli inafanya kazi gani? Ipo tangu uhuru na hatuoni ikitumika kwenye reli, inakwenda wapi? Labda wangeitoa tu kuwasaidia wananchi,” alisema.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wauza Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alisema haoni sababu za kuondoa tozo, ushuru na ada hizo, akisema hiki ni kipindi cha mpito.

Utitiri wa tozo

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), tozo sita zinazokusanywa na Serikali ni tozo ya huduma za bandari (wharfage) ambayo ni kati ya Sh20.88 hadi Sh22.65, tozo ya ukaguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Sh1.24, ada ya Shirika la Huduma za Bandari (Tasac) Sh3.54, na ushuru wa Ewura kati ya Sh6.10 hadi Sh6.80.

Pia, kuna tozo ya Wakala wa Vipimo (WMA), Sh1 na ada ya kushughulikia masuala ya huduma za forodha Sh4.80.

Kodi nne zinakusanywa na Serikali ambazo ni ushuru wa mafuta Sh413, ushuru wa bidhaa kati ya Sh255 hadi Sh465, ada ya mafuta ya petroli Sh100 iliyokuwa imeondolewa na Serikali na ushuru wa maendeleo ya reli kati ya Sh17.44 hadi 18.19.

Tozo na gharama nyingine ni uwekaji wa vinasaba Sh14.20, kusafirisha mafuta kutoka kwenye maghala hadi sokoni kati ya Sh10 hadi Sh150, gharama za wakaguzi wa ujazo wa mafuta kati ya senti 16 hadi senti 17, tozo ya Sh5.44 hadi Sh6 kwa ajili ya Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (Osha), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Wakala wa Vipimo (WMA).

Pia kuna gharama za upotevu wa mafuta kwa njia ya hewa kati ya Sh3.49 hadi Sh6.06, kodi ya mapato asilimia 30, ushuru wa halmashauri kati ya Sh4.88 hadi Sh5.83, upakuaji wa mafuta kati ya Sh4.25 hadi Sh4.61 na tozo ya dhamana ya uagizaji wa mafuta.

Angalizo la Waziri Mkuu Majaliwa

Wakati wafanyabiashara wakieleza hisia zao, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha bei walizopandisha mara moja kuendana na uhalisia wa soko na wasitumie kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan na Kwaresma kujinufaisha.

“Nawasihi wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa muhimu kuuza bidhaa husika kwa kuzingatia gharama halisi za uingizaji, uzalishaji na usambazaji. Wale watakaobainika kupandisha bei za bidhaa muhimu bila utaratibu hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Majaliwa jana alipowasilisha hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha katika ofisi yake kwa Mwaka 2022/23 jijini Dodoma.

Majaliwa alisema Serikali imebaini uhaba na upandaji wa bei usioendana na uhalisia wa soko kwenye bidhaa za ujenzi, vyakula, nishati na pembejeo za kilimo.

“Kufuatia taarifa hizo, niliielekeza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuunda jopo la kufuatilia. Kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Tume ya Ushindani ilifuatilia mwenendo wa bei za bidhaa muhimu zinazozalishwa nchini na zile zinazotumia malighafi kutoka nje ya nchi. Serikali imechukua hatua kukabiliana na upandaji huo wa bidhaa muhimu, kutafuta vyanzo mbadala vya bidhaa na kuweka mifumo ya kusimamia masoko ya awali na minada,” alisema.

Tahadhari za kiuchumi

Dk Abel Kinyondo wa Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema njia sahihi za kuepuka athari hizo ni Taifa kuongeza matumizi ya nishati mbadala kama vile umemejua, gesi asilia na upepo kwa kupunguza matumizi ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

“Hatupaswi kushangaa, ongezeko lilianza kabla ya vita vya Ukraine. Kihistoria hili jambo huweza kusababishwa na vita, magonjwa au nyingine yoyote,” alisema Dk Kinyondo.

Profesa Wangwe alishauri Serikali kuangalia namna ya kupunguza mzigo kwa wananchi kwa kupunguza kodi. “Tunachoweza kufanya kama kuna kodi kwenye mafuta tuangalie ni namna gani tunaweza kuzipunguza, hatuna nafasi ya kucheza,” alisema.

Imeandaliwa na Kelvin Matandiko, Fortune Francis, Bakari Kiango, Tukusuma Imani, Emmanuel Msabaha (Dar), Mussa Juma (Arusha), Rehema Matowo (Geita) na Fina Lyimo (Moshi).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live