Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda kikubwa cha sukari kujengwa Songea, mkataba wasainiwa

Kiwanda Kikubwa Cha Sukari Kujengwa Songea, Mkataba Wasainiwa Kiwanda kikubwa cha sukari kujengwa Songea, mkataba wasainiwa

Wed, 24 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkataba wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari chenye thamani ya shilingi bilioni 500 ambacho kinajengwa katika Kijiji cha Magwamila Kata ya Lilai Muhukuru wilayani Songea mkoani Ruvuma umesainiwa kwenye ukumbi wa Mkuu wa Wilaya Songea Januari 23, 2024.

Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile amesema mkataba huo ni makubaliano ya awali baina ya viongozi wa Kijiji cha Magwamila na wawakilishi wa Songea Sugar Limited ambayo ni tawi la kiwanda cha Kagera Sugar ambao hivi sasa wamewekeza nchini Uganda na wameamua kuanzisha tawi la kiwanda hicho mkoani Ruvuma .

“Mkataba umeshuhudiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na wawakilishi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania Kanda ya Nyanda za Juu Kusini chenye makao makuu yake jijini Mbeya’’.alisisitiza DC Ndile.

Ndile amewataka wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla kujiandaa kuupokea uwekezaji wa kiwanda kikubwa cha sukari katika Katika Kijiji cha Magwamila.

Amesisitiza kuwa wawekezaji hao wanatarajia kuweka zaidi ya bilioni 500 katika kiwanda hicho, ambapo kiwanda kitazalisha tani zaidi ya laki moja kwa mwaka.

Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitaweza kuzalisha umeme ambao utaweza kuuzwa kwenye grid ya Taifa, pia kitazalisha mafuta aina ya ethane ambapo amesema kuwepo kwa kiwanda hicho kitaleta manufaa makubwa katika wilaya ya Songe ana Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Kwa upande wake Mchumi Mwandamizi wa Bodi ya Sukari Tanzania Joshua Mhando ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.

Naye Mwakilishi wa Mwekezaji wa kiwanda hicho, Kapil Dave ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuweka utaratibu mzuri wa uwekezaji ambapo ameahidi kufanya uzalishaji wenye tija na wenye kuleta maendeleo chanya.

Eneo la uwekezaji wa kiwanda cha sukari linatarajiwa kuwa na ukubwa wa hekta 30,000 kati ya hizo hekta 22,000 zitakuwa kwa ajili ya kilimo cha miwa na hekta 8,000 kwa ajili ya ufungaji wa mitambo ya kiwanda, barabara za ndani, maghala, makazi ya watumishi, ujenzi wa huduma za kijamİi.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wawekezaji kufika kuwekeza mkoani Ruvuma ambako kuna fursa nyingi za uwekezaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live