Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda chaiomba Serikali ya Tanzania kuongeza kodi uagizaji vyuma nje ya nchi

70657 Pic+vyuma

Sat, 10 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mkuranga.  Kampuni ya Lodhia Group inayotengeneza bidhaa za chuma na plastiki  imeiomba Serikali ya Tanzania kuongeza kodi ya vyuma vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi kutoka asilimia 25 ya sasa hadi asilimia 35 ili kulinda viwanda vya ndani.

Akizunguza leo Ijumaa Agosti 9, 2019 wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani wakati wa ziara ya wajumbe wa mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), mkurugenzi wa kampuni hiyo, Sailesh Pandit amesema kutokana na kodi ndogo makandarasi wamekuwa wakiagiza vyuma nje kwa wingi na hivyo kuvikosesha masoko viwanda vya ndani.

“Kuna changamoto ya masoko kwa sababu makandarasi wanaagiza vyuma kutoka nje ya nchi kwa sababu wamepewa msamaha wa kodi,” amesema Pandit.

Amebainisha kuwa kwa sasa kiwanda hicho kinazalisha tani 10,400 kwa mwezi ambapo kati ya hizo tani 2,000 wanauza nje ya nchi.

Amesema kutokana na kusuasua kwa masoko kampuni hiyo hufanya kazi kwa saa nane kwa siku, lakini lengo lao ni kuzalisha kwa saa 24.

“Tunajaribu kutafuta masoko ya nje na kwa sasa tumeuza nondo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tunaajiri watu 600, kama tukipata soko la uhakika tutafanya kazi kwa saa 24 tunaweza kuajiri watu 1,200,” amesema Pandit.

Pia Soma

Akizungumzia changamoto hiyo, mhandisi wa viwanda kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Kamara Gombe aliyeongoza ujumbe wa wageni wa SADC amesema wameshapokea maombi ya wenye viwanda na wanayafanyia kazi.

 “Maombi hayo tumeyachukua na Serikali inaendelea kuyafanyia kazi kwa sababu wazalishaji wote wanazalisha takribani tani 200,000 kwa mwaka wakati mahitaji ni karibu tani 300,000.”

“Sasa hatuwezi kuongeza kabla ya kuziba pengo. Lakini kama wanasema uwezo sisi tunayafanyia kazi na baadaye tunaamini mambo yatakuwa mazuri,” amesema.

Ziara hiyo pia ilihudhuriwa na mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Filbert Sanga na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo

Chanzo: mwananchi.co.tz