Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda chabanwa kwa kuzalisha mbolea isiyosajiliwa

4fc1dd08e62da0069ebadb83748bee95 Kiwanda chabanwa kwa kuzalisha mbolea isiyosajiliwa

Fri, 28 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amesikitishwa na kitendo cha kiwanda cha mbolea za maji cha Isacha Feeders Intertrade cha Moshi mkoani Kilimanjaro kuzalisha bidhaa za mbolea ambazo hazisajiliwa na kuthibitishwa ubora wake kwa wakulima.

Akiwa katika ziara ya kukagua viwanda vya mbolea nchini jana Katibu Mkuu huyo alijionea bidhaa za mbolea ya maji iitwayo “Booster II” ikiwa katika ghala la kiwanda cha Isacha Feeder –Njoro Manispaa ya Moshi na kubaini kuwa haijasajiliwa na mamlaka za udhibiti ubora nchini.

“Sijafurahishwa na utendaji kazi wa kiwanda hiki cha mbolea cha Isacha kuona mbolea inayozalishwa haijasajiliwa na Shirika la Viwango (TBS ) pia haina ‘Barcode’, hali inayohatarisha mazao ya wakulima na afya za walaji,”alisema.

Taarifa ya kiwanda hicho cha mbolea ya maji imeonesha kilianzishwa mwaka 2016 kikizalisha mbolea ya maji ambazo zinauzwa kwenye maduka mbalimbali nchini bila kuwa na usajili wa ubora toka TBS.

Kutokana na hali hiyo, Kusaya ameagiza wamiliki wa kiwanda hicho kwenda ofisini kwake Dodoma Septemba 3,2020 ili kujieleza kwa nini serikali isichukue hatua za kukifunga kiwanda hicho hadi wakamilishe taratibu za usajili ili kulinda wakulima na uharibifu unaoweza kujitokeza endapo mbolea hiyo ikikosa ubora.

Kutokana na hali hiyo Kusaya ametoa maagizo matano, mmiliki wa kiwanda hicho kuwasilisha taarifa inayoonesha tangu mwaka 2016 wamezalisha kiasi gani cha mbolea na wameuza wapi, wawasilishe uthibitisho wa cheti cha kuendesha kiwanda toka BRELA na TBS.

Agizo la tatu mmiliki wa kiwanda aeleze kwa nini kiwanda hakina bango la utambulisho na hakijulikani na uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro mahala kilipo na kiwanda hicho kiwasilishe taarifa ya ulipaji kodi serikalini tangu kilipoanza kazi mwaka 2016 hadi sasa.

“Mkija Dodoma nataka mje na taarifa kamili kuhusu uhalali wa kiwanda hiki kuwa na sifa za kuzalisha mbolea inayokwenda kutumika na wakulima ili kuishawishi serikali kuwa mnastahili kuendelea ka kazi, ”alisisitiza.

Kusaya alisema akirejea Dodoma atawaalika Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Mapato (TRA), TBS, BRELA na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) wajadili hatua za kuchukua dhidi ya viwanda ambavyo vinakiuka taratibu za uzalishaji mbolea nchini.

Naye Msimamizi wa kiwanda hicho cha Isacha Feeder -Njoro, Rajab Juma alisema kiwanda hicho kinazalisha lita 17,000 za mbolea ya maji kwa mwaka ambapo lita moja huuzwa kwa bei ya Sh 2,000 kwa wakulima.

Awali Katibu Mkuu huyo alitembelea kiwanda cha mbolea ABM cha Tanga kuona hali ya uzalishaji na kukuta kiwanda hicho kikizalisha chokaa kilimo chini ya uwezo wake kutokana na changamoto ya mtaji.

Akizungumza na waandishi wa habari kiwandani hapo Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Aubray Maimu alisema wanazalisha tani 5,000 za chokaa kilimo kati ya lengo la tani 10,005 kufikia mwaka 2021.

“Mgodi wetu wa Zange Mkulumuzi hapa Kange Tanga una mawe ya chokaa zaidi ya tani milioni 25 inayotesheleza uzalishaji wa mbolea ya chokaa kwa wakulima,” alisema.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dk Stephano Ngailo mahitaji ya mbolea nchini ni tani 664,000 wakati uzalishaji katika viwanda vyote 12 umefikia tani 38,000 pekee kwa mwaka.

Chanzo: habarileo.co.tz