Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda cha tangawizi kuanza rasmi uzalishaji

Tangawizi Myamba Kiwanda cha uchakataji Tangawizi kazini

Sat, 19 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakulima wa tangawizi wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kiwanda kinachochakata zao hilo kufunguliwa nchini Tanzania.

Kiwanda cha uchakataji tangawizi cha Mamba Myamba kilichopo Same mkoani Kilimanjaro, chenye uwezo wa kuzalisha tani 10 za tangawizi kwa siku kitaanza uzalishaji rasmi mwanzoni wa mwezi April, 2022.

Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Emmanuel Loi alipokuwa akifanya mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) hivi karibuni alisema kufuatia uzalishaji wa awali na majaribio ambayo yamefanyika yametoa matokeo chanya ya mafanikio makubwa ambapo kiwanda kimeweza kuzalisha tani 10 kwa saa 24.

Katika kiwanda hicho kuna maabara ya kuthibitisha ubora wa tangawizi inayochakatwa, “ili kujiridhisha na kuhakikisha ubora tunaozungumzia kuwa ni wa uhakika, kiwanda kimewekeza kwenye vifaa vya kimataifa vya maabara vyenye ubora wa kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki.”

Kwa mujibu wa Loi, kiwanda hicho ambacho ambacho ni ubia kati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumshi wa Umma (PSSSF) na Chama cha Wakulima wa Tangawizi Same kimeajiri jumla ya wafanyakazi 24 kwa ngazi mbalimbali.

Tangawizi hutumika kama kiungo katika kuongeza ladha, harufu na kuchangamsha katika vinywaji (kama soda, juisi, vilevi) na vyakula mbalimbali kama mikate, biskuti, keki, nyama za kusaga, achari.

Pia hutumika katika viwanda vinavyotengeneza madawa ya tiba mbalimbali kama dawa za meno, kikohozi, tumbo na muwasho wa ngozi na vipodozi.

Mwenyekiti wa Vyama vya Ushirika vya Wakulima wa Tangawizi, Mbaraka Kibinga, amesema wanashirikiana na uongozi wa kiwanda kuhakikisha masoko yanapatikana.

“Kwa utafiti uliofanyika tumegundua manufaa yake katika mwili, tangawizi ni zao linalohitajika kwa kwa kiwango kikubwa sana,” amesema Kibinga.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, tangawizi ikisindikwa utapata unga, mafuta maalum (essential oils).

Tangawizi iliyovunwa huweza kumenywa, kukatwa na kukaushwa juani au mara nyingine huchovywa katika maji yaliyochemka kwanza na ndipo kukaushwa au hukamuliwa mafuta.

Pia tangawizi husindikwa na kuhifadhiwa kwenye chupa zikiwa zimechanganywa na sukari au chumvi.

“Soko la tangawizi lipo ndani na nje ya nchi, kiasi kikubwa kinauzwa nchini. Bei yake ni kati Sh300 hadi Sh1,500 kwa kilo kutegemeana na msimu,” imeeleza Wizara ya Kilimo kuhusu zao hilo.

Tanzania inazalisha zaidi ya aina 30 za viungo ikiwemo karafuu, pilipili kali, tangawizi, mdalasini, pilipili manga, iliki, mchaichai na vanila. Viungo hivi vina faida nyingi zikiwemo za kuimarisha afya na pia vinatumika kama dawa mbadala.

Hata hivyo, bado wakulima hawajafaidika inavyotakiwa na kilimo cha viungo kwa sababu ya njia duni za uzalishaji na kushindwa kulitumia vizuri soko la kimataifa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live