Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda cha sukari chabanwa kuajiri wazawa

Sukarisssssssssss Kiwanda cha sukari chabanwa kuajiri wazawa

Wed, 15 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeutaka uongozi wa Kampuni ya Mkulazi inayojenga Kiwanda cha Sukari Mbigiri kuhakikisha ujenzi wa kiwanda hicho unakamilika kwa wakati na kuajiri wataalamu wazawa kutoka Mkoa wa Morogoro na mikoa mingine ya jirani.

Akizungumza baada ya kamati hiyo kukagua mashamba ya miwa na ujenzi wa kiwanda hicho cha sukari Mwenyekiti wa kamati hiyo Fatuma Taufiq amesema kuwa licha ya kutoa ajira kwa wazawa lakini pia kukamilika kwa kiwanda hicho kutasaidia kutapunguza upungufu wa sukari nchini unaosababisha kupanda kwa sukari mara kwa mara.

"Kamati imekagua ujenzi wa kiwanda na mashamba ya miwa tunaamini mpaka mwezi Julai kiwanda hiki kitakuwa kimeanza uzalishaji, msisitizo wetu kwenye suala la ajira hakikisheni vijana wanaozunguka maeneo haya ya kiwanda na mikoa ya jirani kama Morogoro, Dodoma na Pwani wanapewa kipaumbele," amesema Fatuma.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ambaye alikuwa mwenyeji wa ziara ya kamati hiyo amesema kuwa kiwanda hicho kinajengwa kwa ubia wa Shirika na Hifadhi la NSSF ambalo limewekeza hisa ya asilimia 96 pamoja na Jeshi la Magereza kupitia shirika lake la uzalishaji mali ambalo limewekeza kwa asilimia 4.

Profesa Ndalichako amesema kuwa kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa kimegharimu Sh344.47 bilioni gharama ambayo itajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, uandaaji mashamba na mambo mengine yanayohusu kiwanda hicho.

"Wazo la ujenzi wa kiwanda hiki ni la muda mrefu lakini mwezi Julai 2021 Rais Samia Suluhu Hassan aliamua kwa vitendo kusimamia wazo hili na hivyo ndipo ujenzi ulipoanza, hivyo tunamshukuru Rais Samia kwa maono na utayari wake wa kuendeleza viwanda hapa nchini," amesema Prof. Ndalichako.

Hivyo amesema kuwa kama wizara watakakikisha lengo la Rais Samia linatimia ili kiwanda hicho kiweze kufanya kazi na hivyo kupunguza uhaba wa sukari nchini.

"Nautaka uongozi wa kampuni hii ya Mkulazi kuhakikisha ujenzi unakwenda kwa kasi na viwango vinavyotakiwa, ikifika Julai mwaka huu tutaileta tena kamati hii na kama Serikali tusingependa kusikia sababu zinazochelewesha ujenzi huu," amesema Prof. Ndalichako.

Awali akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho cha Mbigiri mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho Selestine Some amesema kuwa kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kuchakata miwa tani 2,500 kwa siku na kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka.

Some amesema kuwa fedha zilizotolewa hadi sasa kama mtaji ni Sh263.60 bilioni ambapo kiasi cha Sh19.38 ni thamani ya ardhi na Sh127 bilioni ni fedha taslimu kwa ajili ya kazi ya kilimo cha miwa.

Pia miundombinu ya kilimo cha miwa, ujenzi wa majengo, ununuzi wa vifaa vya kilimo, uendeshaji wa kampuni na kiasi cha Sh117.57 bilioni ni kwa ajili ya ununuzi wa mitambo ya kiwanda cha sukari na gharama ya kutoa mitambo hiyo bandarini na kusafirisha.

Amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho kwa sasa umefikia wastani wa asilimia 89 na kwamba mbali ya ujenzi wa kiwanda lakini pia ujenzi wa bwawa kubwa la kuhifadhia maji inaendelea ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita za ujazo 3.5 milioni na ujenzi huo unatarajia kukamilika Julai mwaka huu.

"Zao la muwa linahitaji maji na kwa kuweka tahadhari ya ukame tumeamua kujenga bwawa hili ambalo litasaidia katika umwagiliaji na mahitaji mengine ya uzalishaji wa sukari kiwandani," amesema Some.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live