MKUU wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo amewataka wafugaji wa mikoa ya Kanda ya Mashariki inayoshirikisha Dar es Salaam , Tanga , Morogoro na Pwani kutumia fursa ya kuuza mifugo kwenye kiwanda cha nyama kinachotarajia kufunguliwa mwezi huu.
Ndikilo alisema hayo juzi wakati wa kumkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ,Profesa Paramagamba Kabudi , kufungua maonesho ya wakulima , wafugaji na wavuvi Kanda ya Mashariki katika viwanja vya Mwalimu Julias Kambarage Nyerere mkoani Morogoro.
Alisema, wafugaji wa mikoa ya kanda hiyo watakuwa na fursa ya kuongeza kipato chao cha kiuchumi kwa kuuza mifugo hasa ng'ombe na mbuzi katika kiwanda hicho ambayo kimejengwa Kibaha kwa ajili ya kuchinja ng'ombe na mbuzi.
Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng'ombe 1,000 na mbuzi 4,500 kwa siku.
Kwa upande wa zao la Korosho ,aliwataka wakulima wa zao hilo kuandaa mashamba yao kwa kuyasafisha na kupuliza dawa ili kuondokana na changamoto zilizojitokeza msimu uliopita kwa korosho zilizoangua chini kuharibika kutokana na mvua nyingi zilizokuwa zilizonyesha.