Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda cha mabehewa kujengwa Tanzania

43740 Pic+mabehewa Kiwanda cha mabehewa kujengwa Tanzania

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikidhamiria kuinua uchumi kwa kutumia miundombinu ya usafirishaji, kiwanda cha kutengeneza mabehewa kinatarajiwa kuanzishwa nchini Tanzania.

Kiwanda hicho kitakachojengwa Mkoani Pwani, pamoja na kutengeneza mabehewa mapya pia kitahusika na ukarabati wa ya zamani.

Mkurugenzi wa Kampuni za Kiluwa Group, Mohamed Kiluwa ambao ndiyo watekelezaji wa uwekezaji huo kwa kushirikiana na Kampuni ya Afrika Kusini ya Jambo, akizungumza mwishoni mwa wiki nchini Afrika Kusini, amesema kiwanda hicho kinalenga kusaidia uimarishaji wa usafiri wa reli.

Amesema kiwanda hicho kitakuwepo katika eneo la uwekezaji la Kiluwa Free Processing Zone mkoani Pwani na utekelezaji wa mradi huo utakuwa katika awamu tatu na kila moja itatoa ajira 980.

“Hiki tunachotaka kukifanya hakijawahi kufikiriwa na wengi, lakini kitaleta tija katika uchumi wa nchi, tunafahamu tunapoelekea ni Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati. Tutahitaji mbinu bora za usafirishaji malighafi na bidhaa, reli ni njia rahisi na salama kusafirishia mizigo,” amesema .

Kwa mujibu wa Kiluwa,  wakazi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki watakuwa sehemu ya wanufaika kwa kuwa baadhi ya mizigo itakwenda katika nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika.

“Ifahamike tumetenga kiasi cha Dola za Marekani Milioni 150, kwa ajili ya kukamilisha mradi huu ambao utaleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya viwanda nchini pamoja na usafirishaji,” amesema Kiluwa.

Naye mwakilishi wa Kampuni ya Africa Jambo Group, Marthinus Christian Landman amesema  wameamua kuwekeza Tanzania kwa sababu wanajua ni eneo muhimu linalokua kwa kasi kiuchumi kutokana na malengo makubwa yaliyowekwa na serikali.

“Siku zote mfanyabiashara anaangalia eneo ambalo atanufaika, tunaangalia zaidi faida kabla ya kukamilisha mikataba, tumejiridhisha kwa sasa Tanzania ni sehemu sahihi na salama kiuwekezaji kwa sababu Rais,  John Magufuli amedhamiria kuona watu wanafanya kazi, hakuna rushwa,” amesema Landman.



Chanzo: mwananchi.co.tz