Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kiwanda cha kusindikiza maziwa chaanzishwa Katavi

Mtindi Clip Data (600 X 303) Kiwanda cha kusindikiza maziwa chaanzishwa Katavi

Fri, 25 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ofisa Mifugo wa Mkoa wa Katavi, Zediel Mhando amesema licha ya mkoa kuzalisha takribani lita milioni 26.5 za maziwa kwa mwaka, changamoto wanayokabiliwa nayo ni kuyaongezea thamani maziwa hayo

Mhando ametoa kauli hiyo leo Februari 25 wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kusindika maziwa cha MSS kilichopo halmashauri ya Nsimbo mkoani hapa, ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Tixon Nzunda alikuwa mgeni rasmi.

“Kwa sasa wafugaji wana changamoto ya ukosefu wa soko la maziwa huku uzalishaji ukiwa mkubwa, maziwa mengi wanamwaga hasa yale ya jioni, kwasababu hakuna kituo cha kukusanyia.

“Mkakati wetu kwakushirikiana na halmashauri na wadau, tumewashirikisha katika mpango wa mkoa kuhakikisha tunaiinua sekta ya mifugo hasa kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya mifugo,” amesema.

Amesema jitihada za mkoa zimefanikisha kumpata muwekezaji Maliki Salum aliyeunga mkono kuanzisha kiwanda hicho cha MSS ambaye atakuwa mkombozi kwa wafugaji na kitakuwa kiwanda cha maziwa pekee mkoani Katavi.

“Yale maziwa yaliyokuwa yanamwagwa hayatamwagwa tena yatafikishwa kiwandani, kitakuwa na uwezo wa kuchakata zaidi ya lita 1000 kwa saa moja, tunatarajia mwezi Mei, 2022 kianze kufanya kazi,” amesema.

Advertisement Kwa upande wake mmiliki wa kiwanda hicho, Maliki Salum ambaye pia ni mfanyabiashara wa kituo cha kuuza mafuta ya dizeli na petroli katika eneo hilo amesema ameamua kuanzisha kiwanda hicho baada ya kuiona fursa hiyo.

“Nimeiona fursa ya maziwa kwasababu mkoa hauna kiwanda, hapa barabarani yanapita maziwa zaidi ya lita 5,000 kwa siku yanakwenda wapi? Watu wanakunywa maziwa siyo safi na salama,”

“Mitambo tumeagiza India tutaanza na bidhaa tatu, tutajikita kwenye maziwa fresh na mtindi safi na salama pamoja na mafuta ya samli baadaye tutaongeza bidhaa nyingine,” amesema Salum.

Naye Katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi sekta ya Mifugo, Tixon Nzunda amesema uchumi wa viwanda umeanza kuonekana Nsimbo kupitia kiwanda hicho cha maziwa.

“Hongereeni sana kwakutekeleza mpango wa taifa wa 2020/2025  wa adhima ya viwanda hususani katika sekta ya uzalishaji wa mifugo na kuwa sehemu ya wawekezaji wa mwanzo katika sekta ya maziwa,” amesema Nzunda.

“Tunaamini mwanzo huu sekta ya mifugo na maziwa inaenda kukua, sisi kama serikali kupitia mkoa na halmashauri tutatoa ushirikiano wa dhati ili ufanikiwe katika mradi huu utakaobadilisha mfumo wa wafugaji wetu,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live