Kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote nchini Nigeria kimeanza kuuza bidhaa za petroli kwenye soko la ndani.
Hayo yamedokezwa na mtendaji mkuu wa kampuni hiyo, Devakumar Edwin ambaye amesema: " Bidhaa zinahamishwa kwa njia ya bahari na nchi kavu. Meli zinapanga mstari mmoja baada ya mwingine kupakia mafuta ya dizeli na ndege."
Kiwanda hicho cha kusafisha mafuta kimejengwa kwa gharama ya dola bilioni 20 na tajiri wa Nigeria Aliko Dangote na kinaweza kusafisha mafuta hadi mapipa 650,000 kwa siku (bpd). Kwa mujibu wa makadirio kiwanda hicho kinatarajiwa kuwa kituo kikubwa zaidi cha kusafisha mafuta Afrika na Ulaya kitakapofikia uwezo wake kamili.
Mwezi Januari Kiwanda cha kusafisha mafuta cha Dangote kilitangaza kuanza uzalishaji wa dizeli na mafuta ya usafiri wa anga, na hivyo kuashiria hatua kubwa katika shughuli zake na sekta ya petroli ya Nigeria kwa ujumla.
Mradi wa Kusafisha Mafuta na Petrokemikali wa Dangote, upo Eneo Huru la Kiviwanda na Kibiashara la Dangote jijini Lagos.
Kuna matumaini miongoni mwa Wanigeria kwamba kiwanda hicho kitachangia kupunguza bei ya bidhaa za petroli na uwezekano wa kubadlisha sekta ya nishati ya nchi hiyo katika miaka ijayo.
Ingawa Nigeria ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta ghafi ya petrol barani Afrika na pia ina uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, lakini nchi hiyo kwa sasa inategemea pakubwa mafuta ya petroli na dizeli kutoka nje kwa sababu ya ukosefu wa uwezo wa kusafisha.