Hatimaye Kiwanda cha Chai Mponde kilichofungwa kwa zaidi ya miaka 10 kimeanza rasmi kuchakata na kuzalisha majani mabichi ya chai.
Kiwanda hicho kilifungwa kutokana na mgogoro kati ya wakulima na Viongozi wa Chama cha Wakulima wa Chai (UTEGA) na mshirika wake, Kampuni ya Chai ya Lushoto inayokuwa ikiendesha kiwanda hicho, wakulima walidai kuchoshwa na kile walichokiita kunyonywa na mwekezaji hivyo wakaamua kuacha kupeleka majani mabichi ya chai kiwandani hapo na hivyo kiwanda kukosa malighafi na kufungwa.
Akizungumza na waaandishi wa habari wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro, Meneja wa Kiwanda hicho, Saane Kwilabya amesema majaribio ya uzalishaji yalianza Septemba 2 nakwamba hadi sasa wameshasaga tani elfu 27 huku uzalishaji kwa siku ukiwa tani sita hadi saba.
Meneja huyo amesema licha ya kuanza majaribio ya uzalishaji lakini tayari wameshapata soko la uhakika kutoka nchini Pakistan ambapo sampuri niliyopelekwa kwa mnunuzi imekubalika kutokana na ubora.
" Tumepata soko nchini Pakistan hivyo kwa sasa tunaendelea kukusanya majani taratibu ili kwenda kuingia sokoni lakini pia vibali vyote kutoka Osha na TBS tumeshapata," alisema Meneja huyo. Mkuu wa Wilaya hiyo ,Lazaro amesema kuwa kiwanda hicho kimefufuliwa na Serika kupitia mifuko ya hifadhi ya kijamii ya PSSSF na mfuko wa wafanyakazi. Lazaro Alieleza kuwa licha ya Serikali kutoa Sh4 billion kwa ajili ya ufufuaji na ukarabati wa kiwanda hicho hadi sasa fedha zilizotumika ni Sh700 milioni nakwamba kiwanda hicho kinamtaji wa Sh3 bilioni ambapo alisisitiza fedha hizo zilizobaki zitawasaidia katika matumizi mengine ikiwemo kununua vitendea kazi ikiwemo magari ya kubebea chai na kuni na kufufua shamba la miti linalomilikiwa na Kiwanda hicho pamoja. " Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuwekeza bilioni 4 kwaajili ya ufufuaji na ukarabati wa Kiwanda kilichofungwa Kwa zaidi ya miaka 10," amesema mkuu huyo wa Wilaya na kuongeza kuwa Halmashauri ya Bumbuli ina kata 18 kati ya hizo kata 15 zinalima zao la chai katika skimu tano zilizopo. Kwa upande wake, Richard Mbughuni ambaye ni mkulima na Diwani wa Kata ya Mponde amesema kuwa jumla ya wananchi zaidi ya 6,000 wanalima chai na kati yao wakulima 200 wameshapatiwa mikopo nafuu kwaajili ya kufufua mashamba yao. "Sisi wakulima tunaamini juhudi za Mbunge January Makamba zimefanya Rais wetu kutupatia fedha za kufufua kiwanda. Hivyo tunawaahidi hatutawaangusha, tumeamua kurudi shambani ili tusikitie hasara kwa sababu bila kupeleka malighafi ni hasara," amesema mkulima huyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Mponde.
Hata hivyo Makamu Mwenyekiti Halmashauri hiyo, Hozza Mandia amesema kuwa uchumi wa Bumbuli unategemea kwa asilimia kubwa zao la chai hivyo anaamini uchumi wao utaimarika kutokana na kuanza kwa uzalishaji wa kiwanda hicho.