Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kituo cha umeme Lemguru kuanza kazi Novemba

Umeme Ys (4).jpeg Kituo cha umeme Lemguru kuanza kazi Novemba

Sun, 22 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Arusha. Wakati kituo cha kupoza umeme kilichopo Arusha - Lemguru kikitarajiwa kuanza kazi Novemba mwaka huu, imeelezwa kuwa kitaweka urahisi kwa nchi kuwa na uwezo wa kununua umeme kutoka Ethiopia pindi kutakapokuwa na mapungufu.

Pia kukamilika kwa mradi huo kunatajwa kuwa msaada kwa nchi za kusini mwa Tanzania kuweza kusafirisha umeme zitakapokuwa zikihitaji kununua umeme.

Kituo hicho kimejengwa kwa zaidi ya Sh655 bilioni ikiwa ni fedha kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).

Meneja mradi wa vituo vya kupoza umeme mradi wa Kenya Tanzania, Timothy Mgaya amesema hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya kituo hicho umefikia takribani asilimia 99 na kinachofanyika sasa ni uthibitishaji wa vifaa vilivyofungwa kwa kuvipima kabla ya kuwashwa rasmi.

Amesema kukamilika kwa mradi huo utawezesha Tanzania kuwa na uwezo wa kununua umeme pindi kutakapokuwa na upungufu nchini na watu wa nchi za kusini wataweza kutumia mradi huo kupitisha umeme wao pindi wanapohitahi kununua Umeme kwa ajili ya nchi zao.

"Hii ni njia muhimu kwa nchi kwani itaweza kutusaidia katika namna zote, tukihitaji kununua umeme itakuwa rahisi au nchi za kusini zikitaka kununua umeme zitatumia njia yetu kwani watakapohitaji kupitisha watalipia," amesema Mgaya.

Mradi huo wa kusafirisha umeme unaounganisha Tanzania na Kenya kwa msongo wa kilovoti 400 pia utakuwa na uwezo wa kusafirisha megawati 2, 000.

Mgaya amesema lengo la mradi huo ni kusafirisha umeme kwa kushirikiana na Kenya kupitia East Afrika Power pool hadi Ethiopia sehemu wanayotegemea umeme huo kutoka na kwa upande wa kusini mradi huo ukiiunganisha Tanzania na Zambia kupitia South African Power Pool.

Katika upande wa uthibitishaji wa miundombinu unaofanyika sasa kabla ya mradi kuwashwa Mgaya alisema njia ya kutoka Singida hadi Arusha imeshathibitishwa baada ya kupimwa na kuwa tayari kwa matumizi.

"Njia iliyobakia ni kilomita 114 kutoka Arusha hadi mpaka wa Namanga ambao uko hatua za kuthibitishwa vifaa hivyo kwa kupimwa na kuwa tayari kwa matumizi," amesema Mgaya.

Tanzania inakamilisha mradi huu wakati ambao tayari Kenya imeshaanza kununua umeme kutoka Ethiopia kwa mkataba wa miaka 25 tangu Novemba mwaka jana.

Mkataba huo uliosainiwa baina ya nchi hizo mbili uliifanya Ethiopia kuiuzia Kenya Megawati 600 kutoka mradi wao wa umeme wa Megawati 2,000 wanaozalisha kwa maji.

Mbali na Kenya, nchi nyingine zinazonunua umeme kutoka Ethiopia ni Sudan na Djibouti.

Akiendelea kuelezea mradi huo, Mgaya amesema pia utakuwa na uwezo wa kuunganishwa na mradi wa Backbone ambao unaunganisha nchi ya Zambia kupitia Iringa.

Akifafanua zaidi kuhusu mradi wa Kenya- Tanzania amesema unahusisha ujenzi wa kilomita 510 wa njia za kusafirisha umeme kwa msongo wa 400kv kuanzia Singida hadi Arusha kabla ya kufika Kenya kituo cha Isinya.

Mradi huo una urefu wa kilomita 414 kwa upande wa Tanzania huku ukiwa na urefu wa Km96 kwa upande wa Kenya.

Kwa manufaa ya Arusha, kukamilika kwa mradi huo kutapunguza mzigo katika kituo cha kupoza umeme cha Njiro kwani watakuwa na 'feeder' nane ambazo zitakuwa zinalisha mkoa wa Arusha pekee.

Kwa upande wake Ofisa wa Mambo ya nje daraja la pili Ubalozi wa Japan, Tabochi Tomoyoshi amesema Japan kwa muda mrefu imekuwa ikiisaifia Tanzania katika utekelezaji wa shughuli za nishati huku akieleza kuwa mradi huo ni muhimu katika kufanya maendeleo ya nchi.

"Japan tunaheshimu sana umiliki wa shughuli zote chini ya mikono ya Afrika na katika ujenzi huu tunashirikiana na AfDB na tunatumaini kama nchi tutaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali," amesema Tomoyoshi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live