Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitendawili soko la Mabibo chatenguliwa!

Mabibo Sokoni Kitendawili.jpeg Kitendawili soko la Mabibo chatenguliwa!

Fri, 25 Aug 2023 Chanzo: Mwananchi

Nani kupewa hati ya kumiliki soko la Mabibo? Hilo ndilo linaweza kuwa swali kwa sasa baada ya kuvunjwa kwa uongozi wa soko uliokuwa unavutana na Halmashauri ya Ubungo jijini hapa.

Mvutano huo ulidumu kwa muda mrefu baada ya wafanyabiashara wa soko hilo kutaka wamilikishwe baada ya kupewa na Rais Hayati John Magufuli mwaka 2020.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alivunja uongozi wa soko hilo na kuamuru lisimamiwe na halmashauri hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha, huku akiwaagiza kulifanyia maboresho madogo kimiundombinu wakati wakisubiri kufanyika maboresho makubwa baadaye.

Wakati Chalamila akitoa maagizo hayo, bado kuna sintofahamu ya hatimiliki ya eneo hilo, ambalo ni sehemu ya Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, ambapo Serikali ya China inamiliki hisa kwa asilimia 5 huku Tanzania ikimiliki hisa asilimia 49.

Hata hivyo, hatima ya umilikishwaji huo, mpaka sasa upo chini ya ofisi ya Msajili wa Hazina kwa ajili ya majadiliano.

Pamoja na uamuzi huo, kwa upande wa wafanyabiashara wa soko hilo wamesema wamelikubali hilo kwa shingo upande kwa kile walichoeleza hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.

Tayari halmashauri hiyo imeeleza kutenga Sh600 milioni kwa ajili ya ukarabati huo, ikiwemo kujenga vizimba na kulifanya kuwa soko la kisasa.

Akizungumza Ofisa habari na Uhusiano wa Halmashauri hiyo, Joina Nzali alisema kiasi hicho cha fedha kitatumika kujenga mabanda, matundu ya vyoo na mifereji ya kupitishia maji, ujenzi ambao utaanza muda wowote kuanzia sasa.

Kwa muda mrefu soko hilo limekuwa likikabiliwa na ubovu wa miundombinu na kuwa kero, hususani kipindi cha mvua ambapo watu hulazimika kukodi au kuvaa mabuti maalumu ya kutembelea kwenye maji ili waweze kuingia sokoni humo kutokana na kuwepo kwa matope.

Changamoto kubwa iliyokuwa ikilikumba soko hilo ni kuliboresha kwa sababu sio wafanyabiashara wala halmashauri wote kilio chao kilikuwa kupata umiliki wa eneo hilo ili waweze kupaboresha.

Kwa wafanyabaishara ambao walikabidhiwa soko hilo na Hayati John Magufuli, mwaka 2020 alipokuwa katika mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Barafu Mabibo, walisema tangu wakabidhiwe kumekuwa na mvutano wa kupatiwa hati ili kulimiki kihalali na kueleza kuwa imetokana na halmashauri kulitaka.

Halmashauri wao katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC), waliyoifanya Machi mwaka huu, walipohojiwa kwa nini wanashindwa kukusanya mapato sokoni hapo, majibu yao nao yalikuwa ni hayo ya kutopatiwa hati.

Pia, mara ya mwisho Mwananchi ilipohojiana na aliyekuwa Kamshina wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Idrisa Kahyera kuhusiana na suala hilo, alisema limekaa kisiasa zaidi na lipo linajadiliwa katika ofisi ya msajili.

Kiini soko kurudishwa Halmashauri Hatua hiyo ya Chalamila ilikuja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba kumpa taarifa kuwa tangu kateuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Januari mwaka huu, moja ya changamoto alizozipokea kwa wafanyabiashara sokoni hapo ni miundombinu isiyoridhisha na hivyo kufanya shughuli zao katika mazingira magumu, hususan kipindi cha mvua.

Malalamiko mengine aliyoyapata mkuu huyo wa mkoa alisema ni uongozi wao kutowasomea mapato na matumizi na unyanyasaji wa wafanyabiashara, hasa pale wanapodai haki zao.

Alisema alifanya nao mkutano, kusikiliza kero hizo, lakini baadhi ya vitengo taarifa zao hazikuwa vizuri na wengine kutoonekana kabisa pale walipoombwa nyaraka.

Pia Komba alisema alimtuma mkaguzi wa ndani kufanya ukaguzi wa mahesabu kuanzia Januari hadi Desemba 2022, na kubainika Sh517 milioni zilikusanywa na uongozi, lakini alishindwa kupata uthibitisho wa wapi zilipo Sh47 milioni.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Chalamila alionyesha kukerwa na kitendo hicho na kutangaza kuvunja uongozi wa soko uliokuwepo, huku akiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi kuwasaka wahusika na kuwahoji.

Agosti 19 mwaka huu, Chalamila alisema ameunda kamati kwa ajili ya kubaini ubadhirifu katika masoko yote mkoani humo.

Uongozi wa Soko wafunguka Akizungumzia uamuzi huo, aliyekuwa mweka hazina wa soko hilo, Edwin Lyimo alisema wameridhika kuchukuliwa kwa soko hilo kwa shingo upande kwa kuwa tuhuma zilizoelekezwa dhidi yao hazina ukweli na hawakupewa muda wa kuzijibu.

Kuhusu tuhuma za kuwa hawajawahi kuwasomea wafanyabiashara mapato na matumizi, alisema hazina ukweli wowote kwa kuwa walishaomba hadi nyaraka za vikao na kuzipeleka Halmashauri, hivyo hawajui kwa nini Mkuu wa Wilaya aliamua kupotosha ukweli.

Soko la Mabibo lililoanzishwa mwaka 1988, mpaka sasa lina wafanyabiashara zaidi ya 10,000 na linahudumia watu zaidi ya 20,000 kwa siku, kwa mujibu wa uliokuwa uongozi wa soko hilo.

Takukuru watia neno Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, Ismail Suleiman alipoulizwa kama wameshaanza kuuhoji uongozi wa soko uliopita, kama RC Chalamila alivyoagiza, alisema wao walishafanya kazi hiyo tangu mwaka jana na matokeo ya hatua hiyo ya kuvunjwa kwa uongozi wa soko ni mapendekezo yao waliyoyatoa baada ya uchunguzi huo. Suleiman alisema walibaini kuwa viongozi waliopewa majukumu ya kukusanya mapato sokoni hapo, hawana mamlaka ya kufanya hivyo kwa kuwa hakukuwa na bodi ya soko iliyowateua na wala hakuna chombo ambacho kingeweza kuwahoji endapo wangefanya ubadhirifu na hivyo kushauri bora soko hilo lirudi kwa Serikali. “Viongozi hawakuwa halali kukusanya mapato, kwani hakukuwa na bodi ya soko wala Halmashauri ya soko iliyowateua isipokuwa walichofanya ni kuunda kikundi ambacho hakipo kisheria na hivyo kukiwa na upungufu kutakosekana mtu wa kumhoji, ikiwemo kujua ukweli kwamba kilikusanywa kiasi gani na kilitumika kufanya nini,” alisema.

Chanzo: Mwananchi