Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kitendawili kizito bei ya mafuta nchini....

Mafuta Dola Kwa Kina Kitendawili kizito bei ya mafuta nchini....

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bei za mafuta ya petroli na dizeli zimepanda tena nchini, huku mwenendo wa bidhaa hizo katika Soko la Dunia ukionyesha uwezekano mdogo wa kupungua ndani ya miezi michache ijayo.

Kwa sehemu kubwa gharama za mafuta zinazoshuhudiwa sasa zinatokana na changamoto ya upungufu na kupanda kwa thamani ya Dola za Marekani dhidi ya sarafu nyingine, pamoja na nchi wazalishaji wa mafuta kupunguza uzalishaji wa bidhaa hiyo, hali inayosababisha uhitaji kuwa mkubwa kuliko usambazaji.

Kwa kawaida Tanzania hutumia mafuta yaliyoagizwa miezi miwili nyuma, hivyo mafuta yanayotumika mwezi huu (Oktoba) yalinunuliwa Agosti na yatakayonunuliwa mwezi huu ni ya Desemba.

Katika Soko la Dunia bei za mafuta ya Septemba zilikuwa kubwa kuliko ya Agosti, hivyo uwezekano wa nishati hiyo kupatikana kwa bei nafuu mwezi ujao ni mdogo, labda kwa muujiza.

Kwa Septemba, bei ya chini ya mafuta ghafi kwa pipa ilikuwa Dola za Marekani 84.74 na kiwango cha juu kikiwa Dola 93.65, kiwango ambacho hakijafikiwa kwa zaidi ya miezi 10 iliyopita.

Agosti bei ya chini ilikuwa Dola za Marekani 78.59 na ya juu Dola 83.07, mafuta ambayo kuanzia jana yanauzwa kwa Sh3,281 kwa lita moja ya petroli na Sh3,448 kwa dizeli, mkoani Dar es Salaam.

Bei hizo ni ongezeko la Sh68 kwa lita moja ya petroli na Sh189 kwa dizeli, ikilinganishwa na bei za mafuta za mwezi uliopita, ambayo yalinunuliwa Julai, 2023.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ongezeko la bei kwa mwezi huu kumetokana na kupanda kwa gharama za bidhaa hiyo katika soko la dunia kwa hadi kufikia asilimia 4.21.

Vilevile Ewura imesema gharama za uagizaji wa mafuta hadi kufikia asilimia 17 kwa petroli, asilimia 62 kwa dizeli na asilimia 4 kwa mafuta ya taa zimechangia.

“Pia, uamuzi wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani (OPEC+) kupunguza uzalishaji na vikwazo vya kiuchumi ambavyo Russia imewekewa na mataifa ya magharibi (vimechangia),” ilielezea taarifa ya Ewura, iliyosainiwa na mkurugenzi wake mkuu, Dk James Mwainyekule.

Kwa kutazama mwenendo na viashiria mbalimbali, Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alisema uwezekano wa bei ya mafuta kuongezeka kwa Novemba na Deseamba ni mkubwa.

“Bado hatupo kwenye nafasi ya kupata unafuu, gharama za mafuta zinategemea gharama za usafirishaji, kwa sasa tunasubiri zabuni ya Desemba ambazo zitafunguliwa mwezi huu. Suala la bei ya mafuta bado halijatulia,” alisema Mgaya.

Alisema hata suala la viwango vya kubadilishia Dola (sarafu ambayo hutumiwa zaidi katika ununuzi wa mafuta na biashara za kimataifa), nalo lina athari, kwani kampuni zinazoagiza mafuta zinapata sarafu hiyo kwa gharama ya juu.

Hata hivyo, alisema Ewura imejitahidi kudhibiti ongezeko la bei ya mafuta mwezi huu, kwani laiti wangetumia gharama za sasa za kuyaagiza, hususan viwango vya kubadilishia fedha ambavyo si vya Benki Kuu ya Tanzania, bei ingekuwa kubwa zaidi.”

Alipoulizwa kuhusu hatua zaidi za kudhibiti hali hiyo, bosi wa Ewura aliliambia gazeti hili kuwa majadiliano yanaendelea ndani ya Serikali kuangalia namna ya kushughulikia unafuu huo.

Alisema anayo matumaini baada ya kupata wazabuni watakaoagiza mafuta kwa gharama pungufu kuliko Dola za Marekani 200 zinazotumika sasa kwa tani moja.

“Pia Benki Kuu ya Tanzania imesaidia kwa asilimia 79 ya mahitaji ya dola kwa manunuzi ya mwezi Oktoba, bado uwezeshaji unaendelea,” alisema Dk Mwainyekule.

Jinsi ya kutoka hapo

Kufuatia mtanziko huo wa bei, wadau wameshauri njia tano za muda mfupi zitakazosaidia watumiaji na wamiliki wa vyombo vya usafiri kupunguza makali yanayotokana na mabadiliko hayo kwenye Soko la Dunia.

Wapo wanaoshauri kupunguza safari zisizokuwa na ulazima, kutumia usafiri wa umma hususan mabasi yaendayo haraka, kutembea maeneo yenye umbali mfupi, kufunga mfumo wa matumizi ya gesi katika gari (CNG) au Serikali kuweka ruzuku katika petroli na dizeli ili kuepuka kupanda zaidi bidhaa na huduma.

“Hata kwa watu wanaoishi jirani wanaweza kuchangia gari moja kwa uelekeo mmoja, inasaidia unafuu. Watu waendelee kufunga CNG, ingawa sijui kwa nini Serikali inasuasua sana wakati gesi itasaidia ukali wa maisha na mahitaji ya dola,” alisema Dk Donath Olomi, mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara.

Aidha, njia za muda mrefu zinazoshauriwa ni kuwa na mpango mkakati wa madini ya nikeli kwa ajili ya uzalishaji betri za magari, uwekezaji mpana katika mifumo ya CNG, kuimarisha uwezo wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta pamoja na mradi kwa ajili ya magari ya umeme.

Akifafanua mipango ya kati na muda mrefu, Profesa Haji Semboja alisema anaamini suluhisho la kudumu ni uwekezaji wa kimkakati katika maeneo na mifumo ya huduma mbadala za nishati ya mafuta nchini.

“Tuweke mfumo imara wa kisera, kisheria na uwekezaji zaidi ya miundombinu ya gesi na madini ya nikeli, halafu tukajielekeze vyombo vya umeme kama SGR na magari au bajaji kwa kutumia umeme wa bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), tutapunguza sana mahitaji ya mafuta,” alisema Profesa Semboja.

Mikakati iliyopo

Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2023/24 Juni 15, mwaka huu, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema Serikali imesamehe ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa uwezo wa injini kwenye magari yanayotumia gesi (CNG).

Pili, Serikali imeingia makubaliano na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwezesha waunganishaji wa magari yanayotumia nishati ya umeme nchini, kuingiza magari ambayo hayajaunganishwa kwa ushuru wa forodha wa asilimia sifuri ili kuhamasisha uwekezaji huo nchini.

Katika ziara zake za mwanzo baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema ni muhimu kufikiri kimkakati ili kumaliza changamoto itokanayo na upatikanaji wa nishati muhimu kwa kuzingatia kuwa haizalishwi hapa nchini.

"Mkakati wa kukabiliana na changamoto hiyo ni matumizi ya gesi asilia (CNG) kwenye magari, Ewura hakikisheni magari yanayotumia nishati hiyo na vituo vya kujazia mafuta vinaongezeka ili tuhame kwenye mafuta na hilo linawezekana kama wote, kama Serikali tutakubali," alisema Biteko, alipofanya ziara Ewura.

Alisema wakati viongozi wakiwaambia wananchi watumie CNG, ni vyema kuanza na magari ya Serikali ambayo yanaweza kubadilishwa, hivyo kupunguza uhitaji wa mafuta na kupunguza hata mzigo wa kuagiza mafuta.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live