Wakati mfumuko wa bei wa jumla ukishuka kutoka asilimia 4.9 Januari 2023 hadi asilimia tatu Januari 2024, hali haikuwa hivyo kwa bidhaa za pombe na sigara.
Kwenye bidhaa hizo zinazotajwa kuwa ni za starehe, kulikuwa na ongezeko la mfumuko wa bei kati ya asilimia 0.6 hadi asilimia 4.1 katika kipindi kama hicho.
Takwimu hizo zimetolewa katika ripoti ya mwisho wa mwezi Februari 2024 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Loading...
Loading...
Pia, bidhaa nyingine ambazo mfumuko wake wa bei umepaa ndani ya kipindi hicho ni pamoja na nyumba, maji, umeme, gesi na vifaa vya nyumbani.
“Bidhaa hizo, mfumuko wake wa bei umepanda kutoka asilimia 2 Januari 2023 hadi asilimia 4.9 Januari 2024,” imeeleza ripoti hiyo ya BoT.
Pia, bidhaa za mahitaji binafsi, bima na ulinzi wa kijamii pamoja na huduma nyinginezo zilipaa kutoka asilimia 2.1 hadi asilimia 7.1.
Athari yake ni
Akieleza athari za mfumuko wa bei wa bidhaa za pombe na sigara, Mchumi Oscar Mkude amesema athari zake si kubwa kwa kuwa hizo ni bidhaa za starehe na hazina madhara makubwa kwa walaji.
“Pombe na sigara ni bidhaa za starehe, ndiyo maana Serikali inapandisha bei huko na huwezi kukuta mlaji anatishwa na bei zake,” amesema Mkude.
Pia, Mkude amesema watumiaji wa pombe na sigara kutokana na asili ya bidhaa hizo hawataacha kuzitumia kwa sababu ya hiyo, labda mfumuko wa bei uende kwa muda mrefu ndipo watalazimika kuacha pombe za viwandani na kutumia za kienyeji.
“Katika uchumi, mfumuko wa bei wa pombe na sigara athari zake ni ndogo, kwa sababu watumiaji wake wataendelea kutumia na mara nyingi hata wauzaji wakubwa au wazalishaji wanajua jinsi ya kuzuia athari.
“Bidhaa hizi zina faida kubwa sana, kwa hiyo ni vigumu kuona bei zake zinapaa sana, hata mfumuko wa bei ukiongezeka labda udumu kwa muda mrefu,”
Mkude ameongeza kuwa ikitokea mtumiaji akashindwa kutumia pombe au sigara za viwandani, atalazimika kuhamia katika bidhaa zinazoendana na hizo za kienyeji.
Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Kichina Afrika (CCS) ambaye pia ni Profesa wa Uchumi, Humphrey Moshi amesema mfumuko huo ni njia moja wapo ya Serikali kuongeza mapato yake kwa kuongeza kodi katika bidhaa hizo.
“Imekuwa hivyo kwa sababu Serikali huenda imeongeza kodi katika bidhaa hizo, ambazo pia zinachangia kuongeza kwa mapato yake na kusaidia katika uendeshaji wa Serikali.
“Kwa sasa hivi uchumi wetu umepanuka, tuna vyanzo vingi vya mapato,” amesema na kuongeza Profesa Moshi.
Hata hivyo, Profesa Moshi amekinzana na takwimu za kushuka kwa mfumuko wa jumla wa bei Januari 2023 ikilinganishwa na Januari 2024 huku akieleza sababu za kupinga kwake.
“Kwa ujumla haiingii akilini ukisema mfumuko wa bei umeshuka kwa kiasi hicho kwa sababu dunia nzima, mfumuko upo juu kutokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta na sababu nyingine ikiwamo mgogoro wa Ukraine na Russia,” amesema Profesa Moshi.
Maoni ya Mkude kuhusu kutoonekana kwa athari hizo, yanaungwa mkono na Janeth John mkazi wa Tabata Segerea ambaye anasema hajaona ongezeko lolote la bei ya pombe tangu mwaka jana.
“Mimi nakunywa bia lakini sijaona huo mfumuko wa bei tangu mwaka jana, bei ni ileile kuanzia Sh1, 700 hadi Sh2, 500 inategemea na aina ya bia," amesema Janeth.
Uzalishaji wa pombe na sigara
Wakati mfumuko wa bei kwenye pombe ukipaa, ripoti ya Tanzania in figures 2022 inaonyesha uzalishaji wa bia umeongezeka kwa asilimia 20 kutoka lita milioni 380 mwaka 2021 hadi lita milioni 456 mwaka 2022.
Hata hivyo, kabla uzalishaji huo kuongezeka, ulishuka kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2018 ambapo bia lita milioni 413 zilizalishwa na mwaka 2019 lita milioni 391, kabla ya kushuka tena mwaka 2020 hadi lita milioni 386.
Pombe nyingine aina ya konyagi uzalishaji wake ulisalia lita milioni 22 mwaka 2022 kama ilivyokuwa mwaka 2021.
Kwa upande wa sigara ambayo mfumuko wake wa bei umeongezeka, ripoti hiyo ya NBS inaonyesha uzalishaji wake umeongezeka kwa asilimia 73.8.
“Mwaka 2021 uzalishaji wa sigara ulikuwa ‘pisi’ bilioni 7.02 huku mwaka 2022 uzalishaji ukiongezeka hadi ‘pisi’ bilioni 12.2,”imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Bidhaa nyingine zilizoshuka
Mbali na kupanda kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa ikiwamo pombe na sigara, pia BoT imezitaja bidhaa ambazo mfumuko wake wa bei umeshuka ndani ya muda wa mwaka mmoja ikiwamo chakula na vinywaji visivyo na kilevi kutoka asilimia 9.9 Januari 2023 hadi asilimia 1.5 Januari 2024.
Huduma za usafiri zimesalia kuwa asilimia 1.8, bidhaa za habari na mawasiliano zimeshuka kutoka asilimia 1.7 hadi asilimia moja na huduma za elimu zimeshuka kutoka asilimia 2.7 hadi asilimia 2.5,” imeeleza ripoti hiyo.