Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kinachoifanya Bandari ya Dar es Salaam iwe kimbilio

Bandari Chachamaa Kinachoifanya Bandari ya Dar es Salaam iwe kimbilio

Mon, 8 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hatua ya Bandari ya Dar es Salaam kuwa chaguo la wawekezaji imetajwa kuchagizwa na maboresho ya miundombinu yaliyofanyika na ujuzi wa wafanyakazi.

Vingine vinavyowavutia wasafirishaji kutumia bandari hiyo kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ni uwepo wake katika jiografia sahihi na usalama wa mizigo.

Kwa mujibu wa TPA, huduma bora katika bandari hiyo ndizo zinazoifanya itumike kusafirishia vifaa mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ya Reli ya Kisasa (SGR).

Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Januari 7, 2024 na Meneja wa Shehena ya Mizigo Mchanganyiko katika Bandari ya Dar es Salaam, Abel Garlus alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali.

Garlus ametaja maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo ni kununuliwa kwa mitambo 98 ya kunyanyua mizigo (folklift) na mingine mikubwa miwili ya kisasa ya kushushia makasha (SSG).

“Vitendea kazi hivi vimefanya sasa tuwe na mitambo yenye uwezo wa kubeba mzigo wa hadi tani 200 kwa wakati mmoja na kuifanya bandari yetu ya Dar es Salaam kuwa ya kisasa na yenye uwezo zaidi,” amesema.

Amesema bandari hiyo imekuwa inahudumia kwa haraka, nafuu na ufanisi zaidi shehena ya mizigo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya kimkakati hapa nchini.

Ametaja vifaa vilivyopokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo kuwa ni vichwa vitatu vya treni ya SGR.

Vingine vilivyopokelewan ni tani 7,000 za reli ya kisasa kwa ajili ya ujenzi wa loti ya tano na mabehewa 27 ya abiria.

Mradi wa SGR unatarajiwa kuwa kiungo cha usafirishaji wa mizigo kutoka maeneo mbalimbali nchini kupeleka bandarini kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.

Desemba 31, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kuanza kufanya kazi kwa mradi huo itakapofika Julai 2024 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma.

Mbali na vifaa vya mradi wa SGR, Garlus alisema vifaa vingine vilivyipokelewa ni kwa ajili ya mradi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP).

Vifaa vilivyopokelewa ni mitambo mikubwa saba, kila mmoja ukiwa na wastani wa tani 50.

JNHPP ndiyo mradi unaotarajiwa kuwa suluhisho la changamoto ya umeme nchini. Utakapokamilika unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115 za nishati hiyo na hadi Desemba mwaka jana ujenzi wake ulifikia asilimia 94.78.

“Hivi karibuni Bandari ya Dar es Salaam imehudumia takribani tani 17,000 za mabomba kwa ajili ya mradi wa Bomba la Mafuta la Hoima, amesema Garlus na kuongeza kwamba kuna meli nyingine 16 zinakuja na shehena ya mabomba kama hayo,” amesema.

Kadhalika, amesema uwepo wa bandari hiyo katika eneo zuri la kijografia, ufanisi na ujuzi wa watendaji wake, umechangia kupunguza gharama za ujenzi wa miradi hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live