Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilombero yachakata tani 1.4 milioni za miwa

0690cee287e75e16901d2007a3388ce2 Kilombero yachakata tani 1.4 milioni za miwa

Thu, 15 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KAMPUNI ya Sukari Kilombero iliyopo mkoani Morogoro imechakata tani 1,409,995 za miwa katika msimu wa mwaka 2020/2021 uliomalizika hivi karibuni.

Asilimia 48 ya miwa hiyo ni ya wakulima wa Bonde la Kilombero. Takwimu hizo zinazidi zile za msimu uliopita za kuchakata takribani tani 290,000 za miwa.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kampuni hiyo ya Sukari Kilombero, Joseph Rugaimukamu.

“Hii ni mara ya kwanza viwanda vyetu kufanikisha kuchakata miwa kwa kiasi kikubwa kama hiki. Mara ya mwisho tuliyokaribia kufikia rekodi hii ni mwaka 2014 tulipochakata tani 1,356,549 za miwa,” alisema.

Alisema uchakataji wa miwa umeenda vizuri kutokana na kutokuwepo kwa mvua nyingi na kuchelewa kufunga msimu. Katika msimu wa uzalishaji wa mwaka 2019/2020, kiwanda hicho kilichakata tani 1,120,059 za miwa.

Uzalishaji wa msimu uliopita uliathiriwa na mvua kubwa zilizoanza Oktoba 2019 zilizosababisha mafuriko katika mashamba na kuharibu daraja dogo la kiwanda na miundombinu ya usafirishaji wa miwa kwenda kiwandani.

Kwa mujibu wa Rugaimukamu, katika msimu wa 2020/2021 uliofikia ukingoni hivi karibuni, Kampuni ya Sukari Kilombero ambayo ni mzalishaji mkubwa wa sukari nchini imezalisha tani 123,167.5 za sukari.

Alisema kiwango hicho kinakaribiana na lengo la uzalishaji sukari msimu huo ambalo lilikuwa ni tani 127,871 za sukari.

Alisema pamoja na kuchakata miwa mingi zaidi, kiwango cha sukari iliyozalishwa hakikuwiana na kiwango cha miwa iliyochakatwa kutokana na ubora wa miwa, ambayo ilikuwa na kiwango kidogo cha sukari kutokana na kukaa bila kuchakatwa tangu msimu uliopita wa 2019/2020.

Kwa msimu ujao unaotarajiwa kuanza Mei mwaka hiuu, Kampuni ya Sukari Kilombero inatarajia kuzalisha tani 125,096 za sukari.

Wakati huo huo, Menejimenti ya Kampuni ya Sukari Kilombero iko kwenye mchakato wa kupata kibali kutoka kwa wanahisa ili kuweza kufanikisha mradi wa upanuzi wa kiwanda.

Chanzo: www.habarileo.co.tz