Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilombero Sugar kuongeza uzalishaji kwa asilimia 100

57360 Pic+kilombero

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kimesema kinatarajia kutumia dola 250 milioni za Kimarekani (sawa na Sh575.1 bilioni za Kitanzania)kufanya upanuzi wa kiwanda ili kuongeza uzalishaji kwa asilimia 100.

Mwaka jana kiwanda hicho kilifikia uwezo wake wa juu wa uzalishaji kwa kuzalisha tani 134,000, na sasa kinataka kuzalisha maradufu na kuinua pia maisha ya wakulima wa Kilombero, ambao tayari wananufaika na uzalishaji wa sasa.

Mwenyekiti ya bodi ya wakurugenzi ya Kilombero Sugar, Balozi Ami Mpungwe alisema hayo wakati alipotembelea ofisi za Mwananchi Communications Ltd, ambao ni wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti na MCL Digital.

Pamoja na maswali mengine Mpungwe ambaye alikuwa balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, alizungumzia masuala kadhaa kuhusu kilimo cha miwa ambayo hutumika kuzalishia sukari.

yafuatayo ni mazungumzo baina ya Balozi Mpungwe na Mwananchi.

Jibu: Ni wazi kuwa uzalishaji haukidhi mahitaji ya soko na taarifa zilizopo ni kwamba uzalishaji ni takriba tani 300,000 wakati mahitaji ni tani 590,00, yaani nakisi ya kati ya tani 120,000 na tani 170,000. Hali bado ni hiyohiyo au imebadilika.

Pia Soma

Mimi si msemaji wa wazalishaji lakini upande wa Kilombero (Bwana sukari) tumezalisha tani 134,000 ikiwa ni takwimu ya msimu uliopita na huo ndio uwezo wa juu kabisa wa kiwanda chetu.

Kiwanda hiki, kabla hakijabinafsishwa kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 90,000 kwa mwaka, wakati kina binafsishwa mwaka 1998 kilikuwa na uwezo wa kuzalisha tani 28,000 tu. Sasa ndiyo kimefika uwezo wa tani 134,000 na hiki ndicho kikubwa kuliko wakati wote na kuliko viwanda vyote kati ya viwanda vinne. Hivyo ni wazi uzalishaji ni mdogo ukilinganisha na soko.

Swali: Fedha za maboresho ya kiwanda zitatoka wapi?

Jibu: Kuna fedha za akiba ya kampuni zitatumika, mikopo kutoka taasisi za kifedha na nyingine mimi kama mwenyekiti wa bodi ndiyo kazi yangu kubisha hodi kwa wanahisa wetu ili kutoa fedha ya kufanikisha hilo,”

Wanahisa ni Illovo ya Uingereza (inayomiliki) asilimia 55, kampuni ya ED&F Man ya Uingereza asilimia 20 na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 25.

Wanahisa wote wameonyesha nia ya kuongeza fedha za kuongeza uwezo wa kiwanda kuzalisha. Serikali yenyewe imekuwa ikituhamasisha kufanya hivyo. Endapo tukianza utekelezaji mpango huo utakamilika mwaka 2022.

Viwanda vyote vikiongeza uzalishaji kama ambavo Kilombero wanakusudia kufanya, basi sukari itakayozalishwa itatosheleza soko na pengine hata bei ya bidhaa hiyo inaweza kupungua.

Kwa ardhi ya Tanzania tunaweza kuwa wauzaji wakubwa wa sukari Afrika Mashariki, tena ni jambo la miaka michache tu (ijayo).

Swali; Ni eneo lipi upanuzi utafanyika na mkakati wa kuongeza mali ghafi?

Jibu: Eneo la viwanda litaendelea kuwa lilelile na malighafi zitapatikana kwa out growers ambao tunapenda kuwaita Kilombero growers (wakulima).

Hivi sasa asilimia 40 yote tunaichukua kwa Kilombero growers ambao wapo 8,000 kati yao 6,000 ni wakulima wadogo kabisa. Tukipanua kiwanda, tunatarajia kuwa na wakulima washirika 16,000 ambao watachangia asilimia 60 ya miwa yote. Sisi tutazalisha asilimia 40 tu.

Ni hatari kwa kiwanda kutegemea asilimia 60 ya malighafi, lakini tumesoma hali zote kama iwapo wakulima wataamua kuachana na kulima miwa. Lakini tuna imani kuwa hawataacha.

Kiwanda kwa kushirikiana na wadau wengine kuwawezesha wakulima kulima kwa tija na hata hali za maisha ya watu wanaozunguka kiwanda sasa zimebadilika sana.

Swali; Je kilimo cha miwa kinalipa?

Jibu: Kilimo kinalipa sana na kwa mwaka jana wakulima waliuza miwa yenye thamani ya Sh67 bilioni, kiasi ambazo hakijawahi kulipwa na kiwanda chochote ndani ya Afrika Mashariki na Sadc.

Hali za wananchi wa Kilombero zimebadilika sana. Natamani maeneo yote ya kijijini yangekuwa vile. Uwepo kwa kiwanda Kilombero katika eneo lile umetengeneza ajira mpya ambazo hazihusiani na kiwanda ambazo ni zaidi 2,000.

Swali: Kwanini sukari inayotoka nje ya nchi huuzwa bei ndogo kuliko ya ndani?

Jibu: Mara nyingi sukari ya nje ambayo huuzwa bei ndogo inakuwa haina ubora unaotakiwa. Lakini kuna nchi nyingine kama Brazil ambazo sukari ni bidhaa ya ziada wao wanatumia miwa kuzalisha ethanol.

Nchi nyingine viwanda vyao vina uwezo wa kufanya uzalishaji mkubwa hivyo gharama za uendeshaji zinakuwa ndogo pia.

Hata sisi kitu ambazo tunapaswa kupambana nacho hapa ni kupunguza gharama za uendeshaji tu na sio jambo jingine, tuongeze ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuzalisha kwa bei nafuu.

Rais John Magufuli ameonyesha nia thabiti ya kulinda viwanda vya ndani, hususani vya sukari hivyo mbeleni mambo yatakuwa mazuri.

Kwa sasa hakuna kiwanda kinachoshindana na kingine kwa sababu soko lililopo halijatosheleza mahitaji.

Pia, hata katika uagizaji wa sukari, tumekuwa tukisisitiza ufanyike wakati sahihi, kwa kuagiza kiasi sahihi, kutozwa kodi sahihi na ubora sahihi ili kulinda viwanda vya ndani kwani tofauti na hapo soko litakuwa holela.

Swali: Je, Tanzania kuna uzalishaji wa sukari ya viwandani?

Jibu: Kilombero imewahi kutengeneza sukari ya viwandani kwa miaka mitatu, lakini sasa imeacha baada ya soko kutoridhisha.

Kuna wakati tulikuwa tunatengeneza. Kampuni kama Coca-Cola na (Kampuni ya Bia) TBL waliipenda sana sukari yetu, lakini baadaye soko likaja kuharibika baada ya kuanza kuagizwaagizwa kwa sukari kutoka nje ya nchi na sisi tukaacha.

Swali: Kuna tofauti gani kati ya sukari ya kiwandani na ya matumizi ya nyumbani?

Jibu: Sukari ni sukari tu, tofauti ni kwamba moja ina rangi ( ya matumizi ya nyumbani) nyingine haina rangi (Rangi nyeupe). Viwandani wanapenda isiyo na rangi ili kama wanatengeneza vinywaji rangi ile isiathiri rangi ya vinywaji vyao.

Hata sukari ya kiwandani inaweza kutumika kwa matumizi ya kawaida, lakini kwa kuwa yenyewe inafuata mchakato zaidi bei yake ni ghali kuliko ya kawaida.

Lakini sasa kwa nini mtu aingie gharama wakati sukari ni sukari tu?

Chanzo: mwananchi.co.tz