Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilio kilekile kwa wafanyabiashara

87580 Pic+kilio Kilio kilekile kwa wafanyabiashara

Sun, 8 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kilio cha wafanyabiashara ni kile kile.

Utendaji katika Bandari ya Dar es Salaam, mwenendo mbaya wa biashara Kariakoo, utitiri wa tozo na Shirika la Wakala wa Meli (Tasac) kufanya kazi kama mdhibiti na pia kutoa huduma, ni baadhi ya mambo yaliyo katika kilio kilichotolewa tena jana na wafanyabiashara mbele ya mawaziri 13.

Kilio kama hicho kilitolewa Desemba 4 na wafanyabiashara wengine mkoani Morogoro walipokutana na timu hiyo ya mawazi ambayo inasikiliza kero zao kwa ajili ya kutafutia ufumbuzi.

Orodha hiyo ndefu ya kero inajumuisha pia baadhi ya hoja zilizowasilishwa na wafanyabiashara hao katika mkutano ulioitishwa na Rais John Magufuli Juni 7 uliohusisha viongozi wakuu wa nchi.

“Wafanyabiashara wamekuwa wakitoa maoni yao, lakini hayafanyiwi kazi,” alisema Angelina Ngalula ambaye ni kaimu mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

“Tozo hizi zitaua biashara.”

Ikiwa ni siku 182 zimepita tangu mkutano huo wa Rais John Magufuli alipokutana na wafanyabiashara na wawekezaji jijini Dar es Salaam, hali ilikuwa kama hiyo jana, huku mawaziri tisa waliohudhuria mkutano huo wakiahidi kwenda kufanyia kazi.

Kero nyingine ni pamoja na kuchelewa kutolewa kwa vibali, kukosekana kwa mfumo mzuri wa kulinda viwanda vya ndani na kutotabirika kwa sera kunakowasababishia hasara katika biashara zao.

“Tunaomba tutengeneze kamati ndogo ya kushughulikia suala la Kariakoo,” alisema Ngalula.

“Unakuta mfanyabiashara ametoka Rwanda kuja kuchukua gari lake bandarini. Akichukua gari anapita Kariakoo kununua vitu mbalimbali na kupakia kwenye gari. Watu hao wamekuwa wakisumbuliwa njiani, sasa hawaendi tena Kariakoo.”

Ngalula aliiomba Serikali kuunda kamati ndogo kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa biashara katika soko la Kariakoo ili kulinusuru kuporomoka kibiashara.

Ngalula alisema Kariakoo ni soko la kimataifa lakini hali iliyopo sokoni hapo inasikitisha. Alisema biashara imeporomoka kwa sababu hakuna mifumo ya kimataifa ya biashara kwenye soko hilo.

Alisema kuwa kero nyingine ni pamoja na utitiri wa tozo.

Pia, mwakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Elias Marwa alisema eneo la Kariakoo kwa sasa limejaa na linahitaji kupumua.

“Hakuna hata pa kukanyaga. Tunaomba mtupatie eneo jingine la ekari 20 barabara ya Morogoro kabla ya kufika Kibaha ili wafanyabiashara wajenge soko jingine,” alisema.

Uingizaji mizigo bandarini

Marwa pia alilalamikia utaratibu mbovu uliopo bandarini kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wanaoingiza mizigo kutoka nje na hata kufikia hatua ya kufilisika.

Alisema katika bandari hiyo yametengenezwa mazingira ya watu kutoa rushwa ili kuruhusu mizigo yao kupita kwa kodi kidogo.

“Pale bandarini shida inaanzia kwenye uthaminishaji, yaani mtoza kodi anaamua aseme kiasi gani hapa sasa ndiyo mazingira ya kuzungumza yanapoanzia,” alisema Marwa.

Suala kama hilo lilizungumzwa na rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (Taffa), John Urio aliyependekeza Serikali kuifanyia marekebisho sheria ya kuanzishwa kwa Tasac.

Urio alisema sekta binafsi haikushirikishwa katika uanzishwaji wa sheria hiyo, matokeo yake biashara bandarini imedorora.

“Ombi letu ni kwamba turudie mchakato wa kuorodhesha bidhaa ambazo zitasimamiwa na Tasac kwa mujibu wa sheria hiyo,” alisema.

“Kampuni za mafuta zinalipa pesa Tasac kupakua mafuta wakati nao tayari walikuwa na makubaliano na kampuni nyingine zenye utaalamu katika eneo hilo.”

Urio pia alisema kuna msongamano mkubwa wa meli na mizigo bandarini kwa sababu wahusika hawataki kushirikiana na sekta binafsi katika kutoa huduma.

“Hakuna bandari inayojivunia mizigo kujaa, bandarini kunatakiwa kuwa empty (tupu), mizigo ikija inatolewa, hiyo inaonyesha efficiency (ufanisi) wa bandari,” alisema Urio.

Kwa upande wake mwakilishi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Hussein Kamote alisema lengo la kufikia uchumi wa viwanda linaweza lisifikie endapo changamoto zilizopo hazitatafutiwa ufumbuzi.

Aliitaja mojawapo kuwa ni kukosekana kwa sera maalum ya kulinda viwanda vya ndani.

Sera nzuri ya kulinda viwanda

Kero kama hizo zilizungumzwa katika mkutano ulioitishwa na Rais uliohusisha wafanyabiashara watano kutoka kila wilaya nchini.

Kero nyingine ni pamoja na kuchelewa kutolewa kwa vibali, kukosekana kwa mfumo mzuri wa kulinda viwanda vya ndani na kutotabirika kwa sera kunakowasababishia hasara katika biashara zao.

Mkutano huo uliofanyika Ikulu ya Dar es Salaam Juni 7, pia ulihudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mawaziri watendaji wa Serikali pamoja na wakuu wa vyombo vya dola.

Katika mazungumzo yake siku hiyo, Rais Magufuli alizungumzia mambo yanayokwaza biashara, utitiri wa taasisi za kusimamia biashara, TRA, rushwa na Serikali kuwa chanzo cha kukwamisha biashara. Pia aliwakosoa wafanyabiashara kwa ukwepaji wa kodi na benki nyingi kuwa mijini badala ya maeneo ya wananchi.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema wakati mwingine, Serikali inakuwa chanzo cha mazingira ya biashara kutokuwa rafiki kutokana na utitiri wa taasisi zake zinazogongana katika kutoa huduma na kuweka tozo.

Alisema kwamba anataka kuona mazingira ya biashara yanakuwa rafiki ili siku atakapoondoka madarakani angalau aache wafanyabiashara mabilionea zaidi ya 100.

Hoja ni ileile Morogoro

Kero kama hizo zilitolewa Jumatano iliyopita mkoani Morogoro ambako timu hiyo ya mawaziri ilipokutana na wafanyabiashara na wawekezaji.

Wafanyabiashara walielezea kuwa kinachowakwamisha katika shughuli zao ni utitiri wa kodi na masuala mengine.

Mwakilishi wa wamiliki wa hoteli mkoani Morogoro, Mittah Muria alisema kwamba bado suala la ushuru limekuwa likiwakandamiza wakati bado wanalipa VAT na kwamba namna ya ukokotoaji imekuwa haina maelezo ya kutosha.

“Kodi ya hoteli (levy) bado si rafiki kwa mfanyabiashara na tunaomba iangaliwe,” alisema Muria.

Chanzo: mwananchi.co.tz