Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kilio chatawala uhaba vituo vya kujazia gesi za magari

Gesi Magari Tanzania Kilio chatawala uhaba vituo vya kujazia gesi za magari

Wed, 3 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati idadi ya watu wanaofunga mifumo ya matumizi ya gesi kwenye magari ikiongezeka, vituo vya kujaza nishati hiyo bado kilio kikubwa kwa watumiaji hao.

Mpaka sasa waliofunga mifumo hiyo ni zaidi ya watu 1,000 huku vituo vya kujazia gesi vikisalia viwili Dar es Salaam, kimoja eneo la Ubungo Maziwa na kingine Tazara.

Wakati magari hayo yakiongekeza, pia upo mkakati wa kuanza kufunga mifumo hiyo kwenye bajaji, jambo ambalo litaongeza mahitaji ilhali vituo vya kujazia vikisalia vichache.

Ufungaji wa mifumo katika magari unazidi kushika kasi ikiwa ni hatua za kubabiliana na bei ya mafuta ambayo inazidi kuongezeka, huku vita vinavyoendelea kati ya Rusia na Ukraine na madhara ya Uviko-19 vikitajwa miongoni mwa sababu.

Wakati vituo vya kujaza gesi vikiwa kilio, idadi ya watumiaji wa nishati hiyo katika magari inazidi kuongezeka, hasa baada ya kampuni zinazofunga mifumo hiyo kwenye magari kuongezeka hadi tatu.

Mhandisi Dorah Ernest kutoka Idara ya Mafuta na Gesi katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), amesema ingawa kampuni nyingi zimeonyesha nia ya kufunga mifumo ya gesi kwenye magari, zilizosajiliwa hadi sasa ni tatu.

“Hadi sasa ni kampuni tatu ndizo zilizosajiliwa rasmi ikiwemo Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), BQ, Anric Gas Technologies,” alisema Dorah.

Kampuni ya BQ ndani ya miezi mitatu imefunga mifumo hiyo katika magari 168 lakini kwa sasa imesimamisha huduma kutokana na kuishiwa vifaa.

Ofisa Mtendaji Mkuu, Profesa John Bura amesema kampuni iliyopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam licha ya watu kuongezeka, shida itakuwa vituo vya kujazia gesi katika magari.

“Kutokana na hilo tuko katika mpango pia wa kujenga kituo cha kujazia gesi katika magari ili kupunguza msongamano,” alisema.

Hali hiyo imewafanya waliobadilisha mifumo ya magari kupaza sauti zao ili Serikali ifanye kila linalowezekana kukabiliana na hali hiyo.

Wameomba vianzishwe vituo hususani katika barabara ambazo zinatumiwa na idadi kubwa ya magari.

Akizungumzia suala hilo, Dorah alisema tayari TPDC imefanya mazungumzo na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuweka utaratibu wa kuwawezesha wamiliki wa vituo vya mafuta kuanza kutoa huduma za ujazaji wa gesi.

“Kwa sasa (vituo vya mafuta) vinaruhusiwa kutoa huduma hiyo. Kampuni 19 zimejitokeza (kuomba kujaza gesi) na nusu yake ni vituo vya mafuta, sasa wanaangalia utaratibu wa kuweka miundombinu ya gesi kwenye vituo vyao,” alisema.

Ingawa alisema bado hawajaanza kujenga, wapo kwenye hatua za mwanzo wa kufuata taratibu za kuanza ujenzi,” alisema Dorah.

Gharama kubadili mifumo

Kuhusu gharama za kufunga mifumo wa kutumia gesi asilia Dorah alisema ni kati ya Sh1.5 milioni hadi Sh2 milioni na ukubwa wa gharama unatokana na vifaa vingi kuagizwa nje ya nchi na havina msamaha wa kodi.

Meneja Mawasiliano Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji EWURA, Titus Kaguo alisema Ewura ipo tayari kuwaruhusu watu wanaotaka kujenga vituo vya gesi wakifuata utaratibu.

“Kwa malengo ya baadaye vituo vyote vya mafuta vitatakiwa kuwa na eneo la kujaza gesi asilia,” alisema Kaguo.

TPDC kwa upande wake ilisema hadi Machi mwakani itakuwa imekamilisha ujenzi wa vituo vinne vya gesi asilia ndani ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya magari na matumizi ya mbalimbali ikiwemo majumbani.

Kati ya vituo hivyo, kikubwa kitakuwa eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambacho kitakuwa kikizalisha gesi iliyoshindiliwa (CNG) kwa ajili ya kujaza katika magari na kuhudumia vituo dada vitatu.

Vituo dada vitakavyohudumiwa na kituo hicho vitajengwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), eneo la Kiwanda cha Kairuki Kibaha na katika eneo la Soko Kuu la Samaki la Feri.

Mbali na kujenga vituo vya CNG, Shirika pia litajenga karakana ya kisasa, itakayowezesha kufunga vifaa vya kuwezesha magari kutumia gesi asilia, itakabidhiwa kwa chuo kwa ajili ya uendeshaji.

Wakati haya yote yakifanyika, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alisema wako tayari kufanya uwekezaji kwenye vituo vya gesi.

“Kwa sababu hili lina faida, litasaidia kupunguza matumizi ya dola 400 milioni kila mwezi katika kuagiza mafuta,” alisema Mgaya.

Bajaji kuanza kufungwa gesi

Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imetangaza matumaini mapya kuanza kufunga gesi hiyo kwenye bajaji.

Kulingana utafiti wa kuangalia faida za kutumia gesi asilia kwenye bajaji uliofanywa mwaka 2020 na DIT kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Punjab cha Pakistan, umeonyesha iwapo bajaji 50,000 tu zitatumia gesi asilia zitaleta faida nyingi za kiuchumi na kimazingira.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live