Mtu anapotaka kusafirisha mzigo wake kwa kutumia lori aina ya Fuso kwenda sehemu tofauti ndani ya nchi akiwa jijini Dar es Salaam, basi wazo litakalokuja kichwani juu ya wapi anaweza kupata gari kwa haraka jibu litakuwa ni Jangwani.
Hiyo ni kwa sababu, eneo hilo kwa zaidi ya miaka 20 sasa limekuwa likitumiwa na wasafirishaji wa mizigo kwa kutumia Mafuso, licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Pamoja na kuwa eneo hilo si rafiki kwa afya ya binadamu mvua zinaponyesha kutokana na kutapakaa tope, maji yaliyotuama na wakati mwingine mafuriko, lakini bado ni moja ya sehemu zinazoleta mapato kwa halmashauri ya jiji.
Hiyo ni kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kila siku jiji hutoza Sh10,000 kwa kila gari linalolala au kuwapo katika eneo hilo wakati ushuru unapokusanywa kwa siku husika.
Ikiwa na maana kuwa kama magari yako 50 hadi 60 kwa siku husika, basi Sh500,000 hadi Sh600,000 hukusanywa kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Jangwani Mafuso Transport Co-operative, Aburahani Temba.
Temba anaeleza kuwa mazingira hayo si salama kwa jamii kutokana na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo, licha ya jitihada za kuchimba mto unaopita karibu yao ili kuzuia eneo hilo kujaa maji pindi mvua inaponyesha kufanyika.
“Tungeomba Serikali watuboreshee eneo hili tulilopo ambalo tunatoa huduma za usafirishaji wa mizigo,” alisema Temba.
Alisema umoja wao una jumla ya wanachama 130, huku walio hai ni 89 ambao wanafanya shughuli zao kila siku. Shughuli hizo hufanyika kwa kutimiza matakwa yote ya Serikali, ikiwemo kulipa kodi.
“Hapa tulipo kuna watu wanazunguka wanachukua ushuru wanapeleka halmashauri, ni Sh10,000 kwa kila gari iliyopo eneo hili, iwe imelala au haijalala eneo hilo inalipiwa,” alisema Temba.
Alisema kabla ya halmashauri kuanza kukusanya ushuru eneo hilo, kama chama kilikuwa kikitoza Sh2,000 kwa kila gari, pesa ambayo ilikuwa ikitumika katika ukarabati mdogomdogo wa eneo hilo.
Temba anaeleza kuwa, halmashauri ilipoweka nia ya ukusanyaji wa ushuru eneo hilo, waliingia makubaliano kuwa wataendelea kupewa Sh2,000 katika Sh10,000 wanayochukua.
“Tulipewa kama takribani miezi mitatu au minne hivi, baadaye ikatoweka, lakini bado wanachukua ushuru na kupeleka (halmashauri), tukajaribu kufuatilia hadi kwa Mkurugenzi ili tuone tunafanyaje, alituambia ile ni haki yenu andikeni barua ili muanze kupewa hizo asilimia mlizokuwa mnalipwa.”
Uwepo wao hatihati
Novemba 4 mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itajenga soko kubwa la wafanyabiashara ndogondogo maarufu wamachinga eneo la Jangwani.
Rais Samia alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Coco Beach, alipokwenda kuwatembelea akitokea kukagua daraja la Tanzanite linalokatiza katika Bahari ya Hindi.
Licha ya mpango huo wa Serikali, Temba anaeleza kuwa wamehakikishiwa kuwa wataendelea kuwapo eneo hilo.
Alisema wameshafuatilia ili kujua hatima yao, huku akieleza kuwa jitihada hizo zilianzia ngazi ya chini hadi kufika kwa Mkurugenzi, huku akiwaahidi kuwa kwa sababu wapo hapo kwa muda mrefu basi watasimamia ili kuhakikisha kuwa wanaendelea kubaki.
Ujenzi wa soko
Akizungumzia suala hilo, Shauri alisema bado hajajua kama eneo wanalofanyia shughuli wasafirishaji hao litaguswa na ujenzi wa soko la wamachinga kwa kuwa hawajajua mchoro wa jengo husika utakuwaje.
Licha ya kuwa bado na matumaini ya kusalia katika eneo hilo lakini wanabainisha kuwa imekuwa ni changamoto kwao wakati wa masika, kwani baadhi ya wafanyabiashara, hususan mama lishe wamekuwa wakipoteza vitu vyao.
Ibrahim Mlula alisema soko la wamachinga litakapojengwa eneo hilo itakuwa ni fursa kwao, kwani wanategemeana katika utendaji.
“Wao watakapokuwa wanachukua mzigo dukani wataleta kwetu tusafirishe sehemu tofauti, ujio wao utafanya idadi ya watu kuwa kubwa, jambo litakalochochea biashara, kutakuwa kuna ujirani mkubwa,” alisema Mlula.
Abdul Msangi ambaye ni dereva alisema kwa miaka yote aliyokaa eneo hilo anafanya kazi katika mazingira yasiyo salama.
“Tuboreshewe hapa, kama ushuru unachukuliwa, kwa nini tusitengenezewe mazingira, vyoo tunavyotumia si salama kwa afya zetu na hela tunazoingiza ni nyingi,” alisema Msangi.